NA EDNA BONDO, HANDENI
MJUMBE wa Halmashauri Kuu ya Chama Cha Mapinduzi Taifa (NEC) Richard Kasesela amesema haoni haja ya uchaguzi ujao wa mwaka 2025 kusimamisha wagombea wengine wa Urais badala yake nguvu ielekezwe kwa Wagombea Ubunge.
Amesema hakuna haja ya kupoteza muda na gharama kwa kile alichokiita kwamba Rais Ssmia anaupiga mwingi.
Aidha ameeleza kuwa hilo limedhihirika leo Machi 8, 2023 ambapo Rais Samia yupo mkoani Kilimanjaro akiandika historia kuwa mgeni rasmi kwenye mkutano wa Bavicha.
Kasesela ambaye pia aliwahi kuwa Mkuu wa Wilaya Iringa, ameyasema hayo katika ibada ya Mazishi ya Baba Mzazi wa Mkuu wa Mkoa wa Rukwa Queen Sendiga, Marehemu Cathbert Sendiga yaliyofanyika katika Kijiji cha Kumwenda , wilayani Handeni Mkoa wa Tanga.
Kasesela amesema 2025 twende na Mama kwasababu sifa anazomwagiwa kuhusu kuupiga mwingi inaonesha dhahiri shahiri kwamba Mama anatosha.
Katika hatua nyingine Kasesela ametumia gursa hiyo kutoa pole kwa wafiwa kwa niaba ya Chama cha Mapinduzi.
“ Natoa pole sana kwako Mkuu wa Mkoa wa Rukwa kwa kufiwa na baba yetu Mzee Cuthbert Sendiga kwa niaba ya chama cha Mapinduzi tunakupa pole, nimefurahi kumuona Katibu Mkuu wa chama cha ADC ambaye pia kasema Mama Dk Samia ana upiga mwingi “
“Mimi naona kama kweli sifa hizi anamwagiwa Mama yetu Dk Samia naendelea kuleta ombi kwenu 2025 vyama vya siasa visiweke mgombea wa Urais tupambane kwenye ubunge ili gharama kubwa za ugombea Urais zifanye kazi ya maendeleo.”