NA MWANDISHI WETU, DAR ES SALAAM
UCHAGUZI wa kuziba nafasi ya aliyekuwa Mwenyekiti wa Chama cha Tanzania Labour Party ( TLP ) Hayati Augustine Mrema, umeshindwa kufanyika leo Machi 6, 2023 kwa kile kinachodaiwa kuwepo kwa viashiria vya rushwa, maelewano mabaya baina ya wagombea.
Machi 5 mwaka hui, Halmashauri Kuu ya TLP ilipitisha majina ya wagombea watano akiwemo katibu mkuu wa chama hicho, Richard Lyimo, Mhandisi Aivan Jackson, Stanley Ndamgoba, Felix Elias na Abuu Changawe.
Demokrasia iliweka kambi katika ukumbi wa Mrina uliopo Manzese ulipotakiwa kufanyika mkutano huo, lakini hakukuwa na dalili za kufanyika mkutano huo.
Akizungumza lkatika makao makuu ya chama hicho Magomeni Dar es Salaam Richard Lyimo amesema ukumbi haukuwa rafiki kwa wajumbe.
Amesema hali hiyo iliwalazimu baadhi yao kuandika barua inayoshauri kusitisha uchaguzi kwa sababu za kiusalama na haki za wajumbe kuonekana kupotea.
“Walivyotuletea barua tukakubaliana nao na wakapeleka nakala kwa msajili kwa kulinda heshima ya chama,” amesema Lyimo.
Mbali na ukumbi kutokuwa rafiki, Katibu Mwenezi wa TLP, Geofrey Stephen amesema kuna wagombea walionesha viashiria vya rushwa kwa kuwakodishia hoteli wajumbe waliotoka mikoani.
“Kwanza niwaombe radhi wanachama wetu waliotoka sehemu mbalimbali nchini kwa kupata usumbufu lakini niwatoe shaka kwani sekretarieti itakaa na itapanga muda mwingine na uchaguzi utafanyika mapema iwezekanavyo na wagombea ni walewale,” amesema Stephen
Hata hivyo, baadhi ya wajumbe waliozungumza na Demokrasia walipinga maelezo hayo wakiutuhumu uongozi wa chama hicho kung’ang’ania madaraka.
“Katibu anagombea uenyekiti ilihali hajavua madaraka aliyonayo hii kikatiba ya chama si sawa vilevile suala la rushwa ni uongo hakuna madai ya rushwa sababu alizozitoa Katibu sio za kweli bali yeye ameahirisha uchaguzi baada ya kuona anazidiwa kete na wagombea wenza” amesema Anna Benedict Mwenyekiti wa TLP ambaye mkoa wa Singida
Kwa upande wake Justous Silungwe kutoka Dodoma amesema kinachoendelea ni kuwahadaa watanzania kuwa uchaguzi umeandaliwa wakati matokeo walikuwa nayo mkononi baada ya kuona mambo yanaenda ndivyo sivyo wakatafuta sababu za kuahirisha uchaguzi.
Naye Abuu Changawe mmoja wa wagombea amesema kilichosababisha hadi uchaguzi uhairishwe ni sababu zisizoeleweka ambazo zipo kinyume na katiba ya chama na akatupia lawama ofisi ya katibu.
Mgombea mwingine Mhandisi Ivan Maganza ambaye pia ni Mwenyekiti wa vijana TLP Taifa amesema shida kubwa ipo kwenye ofisi ya katibu kwasababu hajashirikishwa kiongozi yeyote na hakuna taarifa rasmi inayobainisha kuhairishwa kwa uchaguzi.
“Inasemekana ametelekeza wajumbe wa mkutano mkuu wapo makao makuu hawana nauli, hela ya kula wala posho,” amesema Maganza.
Alipotafutwa kwa njia ya simu Kaimu Mwenyekiti wa TLP aliyesimamia mkutano wa halmashauri mkuu Hamad Mkadam, hakupatikana.
Msajili wa vyama vya Siasa nchini, Jaji Francis Mutungi alipoulizwa kwa simu alisema huo ni uchaguzi wa ndani ya chama na ofisi ya Msajili haihusiki.
“Mkutano wao sio wa mwaka bila shaka ni mkutano tu wa kuziba pengo la mwenyekiti hayo ni mambo yao ya ndani sisi hatuingilii na wala hatuwapangii wanapanga wao,” amesema Jaji Mutungi.
Alipoulizwa kuhusu barua ya kuhairisha mkutano mkuu amesema kwa sasa yupo Dodoma kikazi kwa hiyo hajui kama barua imefika ama la.