NA MWANDISHI WETU, DAR ES SALAAM
IMEELEZWA kuwa ni muhimu kwa kundi la wanawake nchini kutumia teknolojia ya kidijitali katika kazi zao mbalimbali ikiwemo ujasiriamali kwani itawasaidia kuinua uchumi wa familia na jamii nzima kwa ujumla.
Hayo yalibainishwa jijini Dar es Salaam jana na Mkurugenzi wa taasisi hiyo ya Zaina Foundation , Zaituni Njovu wakati wa mafunzo ya siku moja kwa waandishi wa habari wanawake, watetezi wa haki za binadamu, wanasheria na watu wenye ulemavu ikiwa ni sehemu ya kuadhimisha siku ya wanawake duniani ambayo huadhimishwa Machi 8 ya kila mwaka.
Njovu alisema kuwa kwa sasa wapo katika ulimwengu ambao teknolojia ni muhimu kwa kila mtu hivyo wanawake wanapaswa kuamka na kuitumia mitandao ya kijamii ambayo ni moja ya njia kubwa ya mawasiliano duniani kote inayorahisisha kukutana na kundi kubwa la watu kwa wakati mmoja.
Hata hivyo alisema licha ya elimu mbalimbali inayotolewa bado wanawake wanaonekana kuachwa nyuma katika matumizi ya intaneti na hiyo inatokana na wengi kuwa na kipato kidogo na kukosa elimu ya kutosha juu ya umuimu wa jambo hilo katika maendeleo ya maisha yao ya kila siku.
“Ili kuwa kidijitali huwezi kuepuka matumizi ya intaneti lakini sasa kwa takwimu za kidunia kuna watu Bilioni saba ila wanaotumia intaneti ni bilioni nne, hivyo kuna watu bilioni tatu duniani hawatumii kabisa intaneti kwa takwmu za Mamlaka ya Mawasiliano Tanzania (TCRA) hadi Desemba mwaka jana tulikuwa na watu milioni 31 tu ambao watumiaji intaneti na kati ya hao asilimia 18 tu ni wanawake.
“Kwahiyo hapa unaona wazi kuwa bado kuna nguvu kubwa inapaswa kutumika kuhakikisha wanawake wanatumia teknolojia na masuala yote ya kidijitali, wakitumia hivi vitu italeta faida katika masuala ya kiuchumi na kijamii,” amesema Njovu
Aidha Njovu amesema wazazi wanapaswa kuwalea watoto wao katika mazingira ya kuona umuhimu wa kutumia teknolojia za kidigitali katika kujikwamua kiuchumi.
Kwa upande wake Ofisa Tehama kutoka Chama cha Waandishi wa Habari Wanawake (TAMWA), Godwin Assenga amesema sababu ya wanawake kushindwa kutumia interneti ni umasikini, unyanyasaji na ukatili wa kijinsi wanaofanyiwa katika mitandao mbalimbali ya jamii hali inayowafanya kujisikia wanyonge na kuacha kabisa kutumia mitandao hiyo.
“Ili kuweza kupunguza kunatakiwa utoaji wa elimu kwa wanawake hawa hasa namna ya kuweza kukabiliana na mashambulizi na unyanyasaji katika mitandao uongezeke, wajifunze matumizi sahihi ya mtandao yanaanza na wao binafsi waelewe kitu chochote wanachoweka kwenye mtandao iwe picha, ujumbe au sauti vinapaswa kuzingatia maadili,” amesema Assenga
Naye Meneja wa Programu Zaina Foundation, Farida Nchimbi amesema taasisi hiyo itaendelea kuwa na miradi na kutoa mafunzo mbalimbali kwa wanawake kwa lengo la kuweza kupigania haki ya kidijitali hapa nchini.