NA TALIB USSI, PEMBA
KIONGOZI wa Chama cha Alliance for Change and Transparency (ACT-Wazalendo), Zitto Kabwe ameendelea kuibua madudu yanayofanywa na Serikali ya Mapinduzi Zanzibar (SMZ) kupitia Mamlaka ya Viwanja vya Ndege Zanzibar (ZAA) ikiwa ni pamoja na kuilipa kampuni ya Dnata kiasi cha shilingi milioni 170 kila mwezi kama gharama za uendeshaji wa uwanja wa ndege.
Ameyasema hayo wakati akizungumza na maelfu ya wanachama wa chama hicho kisiwani Pemba waliofurika katika Viwanja vya Tibirinzi Chakechake Mkoa wa Kusini Kisiwani hapa leo Machi 4, 2023.
Zito amesema viongozi wanatakiwa waseme ukweli ambao wananchi wa Zanzibar wajue maana fedha zinazolipwa kwa kampuni ya uwanja wa ndege zijulikane kwa nini ni kwa upande wa Zanzibar tu.
Amesema ni lazima waendelee kufanya wajibu wao wa kutaka kufanya haki kwa wananchi wote na kuachana na porojo za viongozi na badala yake wafuate sheria.
“Haiwezekani kampuni itoke nje ije hapa badala ya kuilipa Serikali, lakini leo Serikali kupitia Mamlaka ya viwanja vya ndege inalipa ampuni hiyo fedha hizo nyingi” ameeleza Zitto
Sambamba na hilo Zitto ameendelea kuitaka SMZ kufanya ushindani katika uchumi ambao alieleza huleta faida na maendeleo bora ya nchi hivyo serikali inahitajika kufanya marekebisho hayo kwa manufaa ya wananchi.
Sambamba na hilo kiongozi huyo amesema nyumba zilizopo Mbweni, Zanzibar zilizojengwa kwa Mfuko wa Hifadhi ya Jamii imebainika kuwa nyumba tatu zinamilikiwa na watu wa ikulu Zanzibar na hawalipi kodi ambayo ni zaidi milioni 700/-hivyo Chama hicho wamewataka wawakilishi kulisemea na kutaka kujua kwa ufafanuzi juu ya suala hilo.
KUHUSU URAIA PACHA
Kwa upande wa uraia pacha Zitto alifahamisha kuwa chama chao kinaunga mkono watanzania wanaoishi nje na wale wenye asili, kupewa haki yao ya uraia kwani wanapata shida wanapotaka kurudi kwao.
“Nchi nyingi za Afrika zimekuwa zikiwatendea haki wananchi wake ambao wana asili ya nchi zao kwani hupatiwa uraia licha ya kuwa raia wa nchi nyingine, kwa nini Tanzania tusifanye” ameeleza Zitto
Amewataka wananchi waliopo nje waendelee kuwa karibu na ndugu zao na chama hicho kinaendelea kufuatilia kupata haki zao za msingi za makazi.
“Tunaiomba Serikali ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania washuhghulikie tatizo la makazi na kuwawekea mazingira mazuri ya kurudi makwao kwa wale wote ambao walipata majanga ya kuondoka katika kipindi cha vurugu sa siasa” amefafanua Zitto