Waziri wa Fedha na Mipango,Dk Mwigulu Nchemba na Mkurugenzi Mkazi wa Benki ya Dunia, Nathan Belete wakisaini Mikataba miwili ya mkopo wenye masharti nafuu wa dola za Marekani milioni 550 (sh. trilioni 1.264) na msaada wa dola za Marekani milioni 29.93 (shilingi bilioni 68.51) kwa ajili ya kuboresha sekta za maji na usafi wa mazingira mijini na vijijini na mradi wa kuboresha afya ya mama na mtoto, Tanzania Bara na Zanzibar, wakishuhudiwa na Naibu Waziri wa Afya, Dk.Godwin Mollel (kulia), jijini Dar es Salaam.
NA MWANDISHI WETU, DAR ES SALAAM
WAZIRI wa Fedha na Mipango Dk. Mwigulu Nchemba leo februari 28, 2023 ametia saini makubaliano ya mikataba miwili ya mikopo yenye masharti nafuu katika ofisi za wizara ya fedha jijini Dar es salam
Waziri Dk Mwigulu ametiliana saini na Mkurugenzi Mkazi wa Benki ya Dunia, Nathan Belete ya mkopo wa dola za Marekani milioni 550 sawa sh. trilioni 1.264 za kitanzania na msaada wa dola za Marekani milioni 29.93 (sawa na shilingi bilioni 68.51) .
Akizungumzia mkopo huo wa masharti nafuu Dk Mwigulu amesema itasaidia kuboresha sekta za maji na usafi wa mazingira mijini na vijijini .
Aidha Dk Mwigulu amebainisha kuwa pia mikopo hiyo itasaidia mradi wa kuboresha afya ya mama na mtoto, Tanzania Bara na Zanzibar.
Makubaliano ya kusaini mikataba hiyo miwili imeshuhudiwa na Naibu Waziri wa Afya, Dk Godwin Mollel .
Waziri wa Fedha na Mipango, Dkt. Mwigulu Nchemba (Mb) (Katikati), Mkurugenzi Mkazi wa Benki ya Dunia, Nathan Belete (Wapili kushoto), Naibu Waziri wa Afya, Dk Godwin Mollel (Watatu kulia), Katibu Mkuu Wizara ya Fedha na Mipango, Dk Natu Mwamba, wa pili kulia na Naibu Wake Amina Shaaban, pamoja na Mkurugenzi Mkuu-Wizara ya Afya Zanzibar Dk Amour Mohamed (kushoto) mstari wa mbele, wakiwa katika picha ya pamoja na ujumbe wa Tanzania na Benki ya Dunia baada ya kusaini Mikataba miwili ya mkopo wenye masharti nafuu wa dola za Marekani milioni 550 (sh. trilioni 1.264) na msaada wa dola za Marekani milioni 29.93 (shilingi bilioni 68.51) kwa ajili ya kuboresha sekta za maji na afya, Tanzania Bara na Zanzibar, Jijini Dar es Salaam.