NA DENIS SINKONDE SONGWE
BAADA ya wafanyabiashara wadogo wadogo maarufu kama machinga kuitaka serikali kuharakisha ujenzi wa soko la Majengo halmashauri ya mji wa Tunduma wilayani Momba mkoani hapa katibu Tawala Happiness Seneda ameuagiza uongozi wa halmashauri hiyo kutumia wiki mbili kumaliza ujenzi huo.
Seneda ametoa maagizo hayo baada ya kufanya ziara ya kushitukiza kujionea mwenendo wa ujenzi wa soko hilo huku akisema imekuwa ni mara ya tatu kufika hapo na kukuta ujenzi hauendelei.
Seneda amesema soko hilo likamilike mapema ili kuwa rahisishia wafanyabiashara kufanya kazi zao kwenye mazingira rafiki na salama kwa walaji.
“Nimekuja hapa mara mbili na hili staki lijirudie tena ndani ya wiki mbili majengo yakamilike ,hivyo nakuja baada ya hizo wiki mbili kama mtakuwa hamjakamilika sitakuwa na msamalia mtume”, amesema Seneda.
Mkuu wa wilaya hiyo Faki Lulandala amesema kuanzia sasa atakuwa anashinda eneo la ujenzi kwa kushirikiana na kamati ya ulinzi na usalama kuhakikisha ujenzi wa soko hilo linaisha kwa wakati na kuanza matumizi kwa wafanyabiashara.
“Timu inayosimamia mradi inatakiwa ishinde eneo la mradi ili kuhakikisha kasi inaenda haraka pamoja na fundi kuongeza vibarua ili kazi iende kwa kasi,: amesema Lulandala.
Mkurugenzi mtendaji wa halmashauri ya mji wa Tunduma Philemon Magesa amemhakikishia Katibu Tawala kuwa watamchukulia hatua fundi endapo atashindwa kukamilisha ujenzi huo ndani ya wiki mbili ikiwa ni pamoja na kumpeleka mahakamani na kurudisha fedha alizopewa.
“Serikali kuu imetenga fedha shilingi bilioni 6 kwa ajili ya ujenzi wa mradi huo na hadi sasa wamepokea fedha shilingi milioni 383 na tayari wamejenga majengo manne ikiwepo ofisi ya mtendaji kata na ofisi ya wamachinga, stoo, vyoo, jingo la huduma za kifedha, nyumba ya kuuziz vinywaji na nyumba ya mlinzi”, amesema Magesa.
Katibu wa wafanyabiashara kwenye soko hilo Elizabeth Mwasandumbe amesema ujenzi wa soko unaenda haraka ili wahamie.
“Kitendo cha ujenzi kusuasua unatuchanganya kwani wameelezwa serikali imetoa kiasi kikubwa cha fedha lakini kiwango hicho na hadhi ya ujenzi ni vitu viwili tofauti”, amesema Mwasandumbe.
Sophia Mkamba mjasiriamali wa mboga mboga amesema miezi kadhaa imepita tangu watangaziwe kujenga soko hilo lakini ujenzi umekuwa ukisuasua lakini ukubwa wa fedha na hali ya ujenzi ulivyo ni vitu ambavyo haviendani.
James Samweli mfanyabiashara wa samaki amesema kwa muda mrefu sasa wamekuwa wakipanga bidhaa kwa kutandika karatasi chini, pembezoni mwa barabara ya Tunduma kwenda Sumbawanga.