NA MWANDISHI WETU, DAR ES SALAAM
JUMUIYA ya Ulaya (EU) imeonesha kuridhishwa na hatua ambazo Serikali ya Tanzania imekuwa ikizichukua katika kuboresha masuala ya haki za binadamu, demokrasia, uhuru wa kuongea na utawala bora.
Hayo yamebainishwa na mabalozi wanaoziwakilisha nchi za Umoja wa Ulaya (EU) nchini Tanzania wakati wa majadiliano ya kisiasa kati ya Tanzania na EU yalifanyika Jijini Dar es Salaam.
Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki, Dk Stergomena Tax amesema katika majadaliano hayo EU imeoneshwa kuridhishwa na hatua mbalimbali ambazo Serikali ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania imekuwa ikizichukua kuboresha masuala ya haki za binadamu, demokrasia, uhuru wa kuongea na utawala bora.
“EU wamefurahishwa na hatua iliyofikiwa na Tanzania katika kuboresha haki za binadamu na demokrasia, …..tumeeleza hatua mbalimbali zinazochukuliwa na Serikali na wenyewe hata kabla ya kuwafahamisha tayari walishaona na wameridhika kuwa tumepiga hatua katika eneo hili, kwa kuimarisha haki za binadamu, demokrasia, uhuru wa kuongea na mengine mengi waliyoeleza ambayo yanaonesha kuwa Tanzania tumepiga hatua kubwa kwenye eneo hili,” amesema Dk Tax
Dk Tax amesema pamoja na mambo mengine, wamejadili masuala ya uchumi wa buluu, mazingira, ushiriki wa Tanzania katika shughuli za Kikanda na Kimataifa na jinsi gani Tanzania inaweza kufanya kazi kwa pamoja na EU ili kuhakikisha yale yote yanayofanyika Kikanda na Kimataifa yanakuwa na manufaa kwa pande zote mbili.
Aidha, Dk Tax ameongeza kuwa wamejadili masuala ya kuimarisha uhusiano wa Kimataifa, biashara na uwekezaji, kuboresha urari wa biashara kati ya Tanzania na EU kuwa chanya, mabadiliko ya tabia nchi, ushiriki wa Tanzania katika nyanja za kikanda na kimataifa, vita ya Urusi na Ukraine na athari zake.
Kwa Upande wake Balozi wa Umoja wa Ulaya nchini, Manfredo Fanti amesema kuwa mkutano wa majadiliano ya kisiasa kati ya Tanzania na EU umekuwa muhimu kwa kuwa umetoa picha ya masula ya kisiasa zaidi na kupata uelewa wa kisiasa nchini Tanzania.
“Kupitia mkutano wa majadiliano ya kisiasa wa leo tumeridhishwa na mazingira ya siasa nchini Tanzania,” aliongeza Balozi Fanti
Naye Mkurugenzi wa Kitengo cha Mawasiliano Serikalini, kutoka Wizara ya mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki, Balozi Mindi Kasiga amesema katika mjadala wa kisiasa ulijikita katika makundi matatu ambayo ni ushirikiano wa uwili (bilateral cooperation) kati ya Tanzania na Umoja wa Ulaya, masuala yanayohusiana na Kikanda (kanda ya Jumuiya ya Afrika Mashariki na Jumuiya ya Maendeleo Kusini mwa Afrika (SADC), na mambo yanayoendelea duniani.
“Makundi yote matatu na agenda zake yalijadiliwa kwa kina, masuala yaliyojadiliwa kwa upande wetu Tanzania ni masuala ya mabadiliko ya mabadiliko ya tabianchi……………. biashara na uwekezaji, stratejia mbalimbali zinazotolewa na nchi za umoja wa ulaya,” amesema Balozi Kasiga
Mkurugenzi wa Kitengo cha Mawasiliano Serikalini, Wizara ya Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki, Balozi Mindi Kasiga akiongoza majadiliano ya kisiasa kati ya Tanzania na Umoja wa Ulaya Jijini Dar es Salaam