NA MWANDISHI WETU, ARUSHA
KIONGOZI wa Kanisa la Ngurumo ya Upako lililopo Kisongo Jijini Arusha Nabii Mkuu Dk GeorDavie amemwaga machozi madhabahuni wakati akielezea safari aliyopitia katika utumishi wake wa zaidi ya miaka 40
Nabii Dk GeorDavie alisema alianza huduma akiwa na waumini wa kimaasai 120 ambapo alikuwa akikusanya sadaka ya sh.3500/- tu.
Nabii Mkuu Dk GeorDavie aliyasema hayo mwishoni mwa wiki katika maadhimisho ya mwaka mmoja wa uamsho wa injili ya Kinabii iliyofanyika kanisani kwake.
Alisema amekuwa katika utumishi kwa zaidi ya miaka 40 huku huduma ikiwa na miaka 32 na kanisa lake likiwa na miaka 24.
Nabii Mkuu ambaye pia ni Balozi wa Amani alisema alipoanzisha kanisa walikuwa wanakaa sebuleni kwake huku yeye akiwa kiongozi baada ya ibada aliwasalimu kila muumini mmoja mmoja.
Aidha Nabii Mkuu Dk GeorDavie alisema kutokana na aliyopitia hana budi kumshukuru Mungu na ndio maana anaendelea kuwabariki na kuwasaidia watu katika kile alichombariki
Alibainisha kuwa yeye haangalii wingi wa watu bali ubora wa watu unaokuja katika kanisa lake .
Hivyo anapofikisha mwaka mmoja wa uamsho wa injili ya Kinabii (Hii imetokea toka alipotoa tamko la Uamsho wa Injili ya kinabii) amesema ataendelea kutoa misaada na huduma ili Mungu azidi kumuheshimisha.
Aidha Nabii Mkuu Dk GeorDavie alielezea shukrani zake kwa Mungu kwa kumtambulisha kwa watumishi mbalimbali licha ya kuwepo wachache ambao wanapambana katika kumchafua lakini amesisitiza kuwa Mungu anamtambua.
Katika hatua nyingine baadhi ya wafanyabiashara wa soko la Samunge ambao walipewa mtaji wa kiasi cha sh mil 100/- na Nabii Mkuu Dk GeorDavie walimzawadia Nabii huyo Mbuzi mmoja na sh.2, 000, 000 ikiwa ni shukrani na sadaka yao kwa mtumishi huyo
Naye Nabii Mkuu aliwashukuru wajasiriamali hao na kuwaombea baraka katika ya kuinuliwa na Mungu katika biashara zao na kuahidi kuendelea kusaidia jamii kadri Mungu atakavyomuongoza na kumbariki.
Ikumbukwe kuwa Nabii Mkuu Dk GeorDavie amekuwa akitoa misaada mbalimbali ya kijamii kwa waumini na wasio waumini ambapo miongoni mwa wanufaika ni pamoja na Jeshi la Magereza mkoani hapa ambao walipewa Sh .Mil 20/-wajasiriamali, waandishi wa Habari sambamba na wasanii mbalimbali.