NA MWANDISHI WETU
NAIBU Waziri wa Nishati, Stephen Byabato amesema sasa Tanzania imefanya vizuri katika sekta ya gesi kwa kuwa asilimia 60 hadi 70 ya umeme unaozalishwa nchini ambao unafikia megawati 1,900 unatokana na gesi hali inayoifanya nchi kuwa mfano wa kuigwa Afrika Mashariki na Kati.
Byabato amesema hayo katika mkutano maalum wa wadau wa nishati kwa nchi za Afrika Mashariki unaotarajiwa kufanyika Uganda kuanzia Mei 7 hadi 11 mwaka huu, ambapo pia alitumia fursa hiyo kueleza kuwa mwezi ujao wa Aprili, Serikali kupitia wizara yake inatarajia kusaini mkataba wa kuanza Mradi wa Kuchimba Gesi Asilia (LNG) katika eneo la Bahari Kuu Kusini mwa Tanzania.
Amesema mradi huo ni habari njema kwa nchi wanachama wa Jumuiya ya Afrika Mashariki (EAC) zitakapokutana katika Kongamano la Mafuta na Gesi la Afrika Mashariki litakalofanyika Mei 9 hadi 11, mwaka huu nchini Uganda.
Byabato ametumia fursa ya kikao hicho na wadau mbalimbali wa sekta ya mafuta na gesi kilichojadili namna Tanzania itakavyoshiriki na kunufaika katika kongamano hilo kueleza mikakati wa Serikali katika eneo hilo.
“Jambo kubwa tunaloenda nalo katika mkutano huo ni kuwapa taarifa njema za maendeleo ya mradi wetu wa LNG tunaoufanya katika eneo la Bahari Kuu, ambapo tukiivuna ile gesi tutaileta katika eneo linaitwa Likong’o pale Lindi kwa ajili ya kuichakata,” ameeleza Byabato.
“Tunaamini mwezi unaokuja Mwenyezi Mungu akijalia tutasaini mkataba kati yetu na wabia ambao tulikubaliana nao kutekeleza mradi huu na tutakamilisha jambo hili la majadiliano na kuingia ‘site’ na kuanza kuchimba gesi hiyo,” ameongeza Byabato.
Amesema Shirika la Maendeleo ya Petroli Tanzania (TPDC) na wadau wengine kama Mamlaka ya Udhibiti wa Mkondo wa Juu wa Petroli (PURA), Mamlaka ya Udhibiti na Utafutaji wa Mafuta na Gesi asilia Zanzibar (ZPRA) watakuwa na jukumu la kutangaza fursa zitokanazo na mradi huo mkubwa wenye thamani ya Sh trilioni 70 kwa wawekezaji na wafanyabiashara kutoka katika mataifa mbalimbali barani Afrika.
Amesema mbali na mradi huo mkubwa, Tanzania itaendelea kuwavutia nchi wanachama wa EAC kwenye sekta ya gesi na kuongeza kuwa taifa limejipanga kupeleka gesi kwa nchi zilizoonesha kuvutiwa na gesi hiyo kama Kenya, Rwanda, Zambia na Uganda.
Amebainisha kuwa, Tanzania ni nchi ya amani hivyo uchimbaji na usafirishaji wa nishati hiyo ni salama kiasi mataifa yote hayatakiwi kujiuliza mara mbili kuhitaji nishati hiyo. Mwakilishi wa Katibu Mkuu Wizara ya Nishati, Joyce Kisama alisema mbali na kongamano la Uganda, Tanzania ina nafasi nyingine nzuri ya kunadi miradi mbalimbali ya gesi katika kongamano litakalofuata mwakani ambalo litafanyika Tanzania.
Mdau na msafirishaji wa mafuta ambaye pia ni Mkurugenzi wa Kampuni ya MOIL, Altaf Manson aliwataka wafanyabiashara na wawekezaji wa Tanzania kuchangamkia fursa zinazotokana na kongamano hilo.
Amesema kwa watanzania ambao wataona uwezo wao ni mdogo ni bora waungane ili wapate nguvu ya kushiriki. Mwakilishi wa Mkurugenzi Mtendaji wa ZPRA, Abdulkadir Mahmoud Juma alisema wamejipanga kushiriki kikamilifu kongamano hilo kwa kuwa wana malengo ya kuifungua Zanzibar katika sekta ya mafuta na gesi.
Amejinasibu kuwa, yapo maeneo ya Bahari Kuu yanatakiwa kufunguliwa kwa kutangazwa kuwavutia wawekezaji na wafanyabiashara kuja kuwekeza katika visiwa hivyo.