NA MWANDISHI WETU, DAR ES SALAAM
BENKI Kuu ya Tanzania (BoT) imewaasa wananchi wanaotumia huduma ndogo za Fedha (Microfinance) kuacha kukopa fedha kwenye taasisi zisizosajiliwa na Benki hiyo.
Aidha BoT tayari imeshatoa mwongozo kwa watoa huduma ndogo za fedha kufanya usajili wa huduma hiyo kwani imeweka kiasi cha asilimia 3.5 kwa mwezi kama kiasi cha riba kwa mtoa huduma ndogo ndogo za mikopo ya fedha (microfinance).
Hayo yamesema na Kaimu Msimamizi wa Huduma Ndogo za fedha (BoT), Mary Ngasa wakati akijibu maswali ya wahariri wa vyombo vya habari mara baada ya kumaliza kuwasiisha mada ya Usimamizi wa Huduma Ndogo za Fedha, (Microfinance Supervision) katika Mkutano uliowakutanisha wahariri hao na BoT uliofanyika Februari 27,2023 kwenye ukumbi wa Benki hiyo Jijini Dar es Salaam.
“Ni kwa mujibu wa Benki Kuu (BoT) anayetoza riba zaidi ni mhalifu na anapaswa kuchukuliwa hatua za Kisheria”,amesema na kuongeza
“Tunawaomba wananchi kuzingatia usalama wa taasisi hizi wanazokwenda kukopa, msikope kwa mtu asiye na leseni ya BoT, na msikubali kukopa bila ya kujua masharti ya mkopo hususani suala la riba kuepusha kuzidishiwa makato,” amesisitiza Mary.
Aidha amewataka watoa huduma ndogo za Fedha (Microfinance) kujisajili katika Halmashauri zao ili waweze kupatiwa leseni za kutoa huduma hiyo kwani kutofanya hivyo watachukuliwa hatua za kisheria