NA TALIB USSI, ZANZIBAR
KIONGOZI wa Chama cha ACT Wazalendo, Zitto Kabwe amekosoa uendeshaji masuala yanayohusu uchumi Zanzibar na kusema chama hicho hakikubali kuwa sehemu ya serikali inayoshindwa kuongoza kimaendeleo.
Zitto amekosoa uendeshaji huo katika mkutano wa chama chake uliofanyika februari 26, 2023 visiwani hapa.
“Serikali ya Umoja wa Kitaifa ambayo ACT ni washirika haiwezi kuwa ya wizi, hapana. Tunataka serikali inayosikia na kuendesha mambo kwa mujibu wa taratibu za kisheria kwa maslahi ya wananchi wa Zanzibar.” amesema.
Zitto ametoa msimamo huo kwenye mkutano mkubwa wa hadhara wa chama hkcho uliofanyika kijijini Nungwi, Wilaya ya Kaskazini A, Mkoa wa Kaskazini Unguja. Huo ni mkutano wa kwanza kuitishwa na ACT Wazalendo kwa Unguja tangu amri haramu ya kupiga marufuku mikutano ya hadhara ilipotolewa mwezi uliopita na Rais Samia Suluhu Hassan.
Kiongozi wa ACT Wazalendo ambaye ni mtaalam wa uchumi mkubwa aliyesomea nchini Ujerumani, alisema uongozi wa Serikali ya Mapinduzi Zanzibar chini ya Dk. Hussein Ali Mwinyi, unafanya makosa kwa kuendesha mambo kwa kuvunja sheria kama ilivyofanya kuruhusu kampuni moja kupewa ‘haki ya kipekee’ ya kutoa huduma za kupokea na kuhudumia ndege kwenye Uwanja wa Kimataifa wa Abeid Amani Karume (AAKIA) uliopo Kisauni, nje kidogo ya mji wa Zanzibar.
Zitto akiwa kiongozi wa mwisho kuhutubia umati uliohudhuria mkutano huo, amesema sheria za masuala ya usafiri na usafirishaji kwa njia ya anga za Tanzania na Zanzibar zinakataza utaratibu wa kampuni moja kupewa haki ya kipekee ( exclusivity right).
Hata sheria za kimataifa za sekta hiyo zinazosimamiwa na Shirika la Kimataifa dla Usafiri wa Anga (ICAAO), haziruhusu utaratibu huo, badala yake zinahimiza ushindani.
Akigusia sheria za Tanzania, amesema utaratibu unaokubaliwa ni wa kampuni ya kigeni inayotaka kuwekeza kwenye sekta hiyo, basi inalazimika kumiliki asilimia isiyozidi 65 ya hisa huku asilimia 35 iliyobaki ikimilikiwa na kampuni inayomilikiwa na wenyeji (wazawa).
“Tunaitaka Mamlaka ya Viwanja vya Ndege iondoe haki hii (ya kipekee) kwa kampuni waliyoipa mkataba ili kuruhusu ushindani. Kama wanao watu wanaowataka kutoa huduma uwanja wa Abeid Karume basi waruhusu ushindani,” amesema.
Hapohapo, Zitto aliyewahi kuwa Mwenyekiti wa Kamati ya Hesabu za Mashirika ya Umma (PAC) kupitia Bunge la Jamhuri ya Muungano, alitaka Mamlaka ya Kuzuia na Kupambana na Rushwa na Uhujumu Uchumi Zanzibar (ZAECA) kufanya uchunguzi wa kina kubaini ni nani hasa anayemiliki hisa 35 kwenye kampuni hiyo.
Maelezo ya Zitto yanalenga kuibana kampuni ya DNATA, yenye makao makuu yake jijini Abu Dhabi, ambayo ndiyo iliyokabidhiwa mkataba wa haki ya kipekee” kutoa huduma kwenye uwanja huo uliokamilika hivi karibuni baada ya ujenzi uliogharimu Dola Milioni 20.
Kampuni hiyo ilianza kazi rasmi mwezi uliopita baada ya kusaini mkataba wa utoaji huduma chini ya ZAA, mamlaka ambayo ilishikilia kuendelea na mkataba huo licha ya malalamiko mengi kutoka kwa watoa huduma kwenye ndege wlaiotishia hata kushtaki.
Walifungua kesi mahakama ya utatuaji migogoro ya kibiashara iliyoko Uingereza lakini DNATA inayosifika kwa ubora wa huduma zake, inaendelea kufanyakazi huku kukiwa na madai ya kukosa ajira kwa waliokuwa wafanyakazi wa kampuni ya ZAT inayomilikiwa na mfanyabiashara mzawa wa Zanzibar, Mohamed Raza,
Ismali Jussa , mjumbe wa Kamati Kuu ya ACT Wazalendo anafahamika kwa kuwa mstari wa mbele kupinga uamuzi wa SMZ kuipa DNATA mkataba wa haki ya kipekee kwa maelezo kuwa ni kinyume na sheria za nchi na utawanyima ajira mamia ya wafanyakazi wa Kizanzibari.
Katika hatua nyingine, Zitto ametoa tahadhari kuwa Shirika la Hifadhi ya Jamii la Zanzibar (ZSSF) linaweza kukosa uwezo wa kutimiza majukumu yake kutokana na kuendeshwa vibaya.
Amesema maamuzi yanayofanywa katika nyanja ya uwekezaji yanaacha nyufa nyingi kwamba itafika siku shirika hilo litashindwa kulipa pensheni kwa wanachama wake wanaostaafu.
Ili kukinga na hatari ya mfuko huo kufilisika, amesema inafaa sasa Mdhibiti na Mkaguzi Mkuu wa Hesabu za Serikali (CAG) wa Zanzibar kufanya uchunguzi maalum kubaini kama kuna matatizo ya matumizi mabaya ya madaraka.