NA MWANDISHI WETU, IRINGA
WATU wawili ambao bado hawajafahamika majina yao wamepoteza maisha katika ajali iliyohusisha malori mawili ya kubebea mizigo yenye namba za usajili T286 CKG na jingine KBE 492K kugongana februari 24,2023 eneo la Inyororo wilaya ya Mufindi mkoani hapa
Waliopoteza maisha katika ajali hiyo ni dereva wa gari lenye namba za usajili namba T286 CKG ambaye bado hajafahamika jina lake pamoja na mwanamke ambaye mwili wake umekutwa umeungua na moto ambaye pia jina lake halijafahamika.
Kwa mujibu wa mashuhuda waliokuwepo eneo la tukio wamesema chanzo cha ajali hiyo ni gari lenye namba za usajili T286 CKG kupoteza mwelekeo na kusababisha ajali hiyo.
Kufuatia tukio hilo Mkuu wa Wilaya hiyo Dk Linda Salekwa alifika eneo la tukio na kuwahakikishia usalama wananchi wa eneo hilo kwani gari lililosababisha ajali hiyo lilibeba kemikali aina ya salfa ambapo pia amewaasa madereva kuwa makini pindi wanapokuwa barabarani.
Dk. Salekwa amesema miili ya marrhemu hao imehifadhiwa kwenye hospitali ya mji wa Mafinga kwa ajili ya kusubiri kutambuliwa na ndugu zao.