NA MWANDISHI WETU, DAR ES SALAAM
WAZIRI MKUU Kassim Majaliwa ameahidi ushirikiano zaidi baina ya Serikali na Sekta Binafsi katika utoaji elimu ya ufundi na mafunzo ya ufundi stadi ili kuzalisha wataalamu wenye ujuzi wa kutosha unaohitajika katika sekta mbalimbali.
Aidha , Waziri Mkuu ametoa wito kwa waajiri wote nchini waendelee kushirikiana na Serikali katika kuhakikisha malengo ya kukuza ujuzi na kuongeza soko la ajira yanafanikiwa kwa mustakabali wa maendeleo ya Taifa.
Ameyasema hayo februari 24, 2023 katika hafla kati ya Baraza la Taifa la Elimu ya Ufundi na Mafunzo ya Ufundi Stadi (NACTVET) na wadau kutambua mchango wa uzalishaji wa rasilimali watu yenye ubora kwa soko la ajira.
”Maendeleo ya uchumi wa nchi yoyote yanategemea sana ngazi ya ujuzi wa nguvukazi uliyokuwa nayo. Hivyo, mchango wa wadau ni muhimu.”
Mbali ya hayo, Waziri Mkuu amewapongeza waajiri kwa kutoa nafasi za mafunzo kwa vitendo (field practical), uanagenzi, utarajali pamoja na namna wanavyoshiriki wenu katika kuandaa mitaala inayotumika kwenye vyuo na taasisi za Elimu ya Ufundi na Mafunzo ya Ufundi Stadi.
Amesema ushirikiano huo ni muhimu sana katika kuendeleza ujuzi kwa ajili ya kujenga uchumi wa viwanda.
“Nataka nitumie fursa hii kuwapongeza lakini Serikali inatambua na inathamini juhudi mnazozifanya katika utoaji wa ajira kwa wahitimu wetu, tunawapongeza sana.”
Akizungumzia kuhusu kauli mbiu ya mwaka huu inayosema ‘Kuimarisha Elimu ya Ufundi na Mafunzo ya Ufundi Stadi kwa Uzalishaji wa Wafanyakazi Wenye Ujuzi Nchini Tanzania’ Waziri Mkuu amesema kauli hiyo ni thabiti kwani inaweka msisitizo katika ujenzi wa rasilimali watu yenye ujuzi.
“Ni ukweli usiopingika bila ujuzi hakuna maendeleo yoyote yanayoweza kupatikana. Ujuzi unahitajika kwenye nyanja mbalimbali za uzalishaji hapa nchini kwani mataifa yote yaliyopiga hatua kubwa za maendeleo yamefanikiwa kwa kuweka kipaumbele katika kuongeza rasilimali watu yenye ujuzi.”
Amesema maeneo yaliyowekewa msisitizo ni sekta za kipaumbele, kuimarisha mafunzo kwa vitendo kwa wanafunzi wa vyuo vya elimu ya juu na kati ili kuhakikisha vijana wanaohitimu wanapata maarifa na ujuzi wa kazi utakaowawezesha kujiajiri na kuajirika.
“Hii ni pamoja na kuimarisha mifumo na kuongeza kasi ya kurasimisha ujuzi ili nguvukazi ya Taifa itumike ipasavyo katika soko la ajira la ndani na nje.”
Amesema kwa kutambua umuhimu wa kukuza na kuendeleza ujuzi, Serikali ya awamu ya sita inayoongozwa na Mheshimiwa Rais Dk Samia Suhulu Hassan inatekeleza kwa vitendo dhamira yake ya dhati ya kuwasaidia vijana hapa nchini kupitia mipango na mikakati mbalimbali ukiwemo Mpango wa Tatu wa Taifa wa Maendeleo wa Miaka Mitano (2021/2022 – 2025/2026), unaolenga kukuza ujuzi kwa Watanzania wapatao 681,000.
Waziri Mkuu amebainusha kuwa, kulingana na utafiti wa nguvu kazi wa mwaka 2021, nguvu kazi ya vijana ni milioni 14.2 sawa na asilimia 55 ya nguvu kazi yote nchini, ambapo vijana milioni 12.5 sawa na asilimia 87.8 ya nguvu kazi ya vijana nchini wameajiriwa au kujiajiri.
Aidha, Waziri Mkuu amesema kupitia utekelezaji wa Program ya Kitaifa ya Kukuza Ujuzi Nchini, vijana 22,899 wamepatiwa ujuzi unaowawezesha kujiajiri au kuajiriwa. Kati ya hao, vijana 14,440 wakiwemo vijana wenye ulemavu 349 wamepatiwa mafunzo ya uanagenzi katika fani mbalimbali.
Naye, Waziri wa Elimu, Sayansi na Teknolojia Profesa Adolf Mkenda amesema kuwa Serikali itaendelea kusimamia utekelezaji wa Makakati wa Taifa wa Uendelezaji wa Ujuzi wa Mwaka 2016/17-2025/26 ambao moja ya malengo yake ni kuwa na ushirikiano kati ya waajiri, wadau na vyuo au taasisi za elimu.
Kwa upande wake Katibu Mtendaji wa Baraza la Taifa la Elimu ya Ufundi na Mafunzo ya Ufundi Stadi (NACTEVET) Dk Adolf Rutayuga amesema Mafunzo yanayotolewa kwenye Vyuo na Taasisi za Elimu ya Ufundi na Mafunzo ya Ufundi Stadi, yanaongozwa na mahitaji ya soko la ajira, hivyo, ushirikishwaji wa waajiri na wadau mbalimbali katika maandalizi ya mitaala ni muhimu sana.
“Baraza linatenga muda kama huu ili kukutana na waajiri hao na wadau wetu wa elimu va ufundi na mafunzo ya ufundi stadi. Kukutana huku, kunatufanya kuwa karibu na kuwa na mahusiano mazuri na wadau wetu ambapo tunakumbushana kuhusu nafasi yao katika kukuza ujuzi, na hivyo kuwaonesha kwamba wao ndio wanatakiwa kuamuru nini kinatakiwa kufundishwa katika vyuo na taassi zetu”. ameeleza Dk Rutayuga.
Amesema ili kupata Waajiri Bora wa mwaka 2023, zoezi la uchakataji wa takwimu lilifanyika kwa kuwagawa katika makundi matatu; waajiri wakubwa (waajiriwa 100 na zaidi), Waajiri wa kati (waajiriwa 50-99) na Waajiri wadogo (waajiriwa 5-49).
Mtendaji Mkuu wa Chama cha Waajiri Tanzania (ATE), Suzanne Ndomba-Doran amesema ili Tanzania iweze kushiriki kikamilifu katika soko shindani la Afrika Mashariki na dunia ni lazima hatua za maksudi zichukuliwe katika kukuza ujuzi hususani kwa vijana.
“Katika kutimiza azma hii, Chama Cha Waajiri tunaamini waajiri wana nafasi kubwa katika kufikia malengo tuliyojiwekea kama nchi.”
“Mfano, kupitia Mpango wa Taifa wa Maendeleo wa miaka mitano, awamu ya tatu (the National Five-Year Development Plan-Phase three), tumelenga kupunguza ukosefu wa ajira kutoka asilimia 9 (mwaka 2019) kufikia asilimia 8 ifikapo mwaka 2025/26. Kukuza ujuzi ni kati ya mipango iliyobainishwa na Serikali ili tufikie lengo na kuongeza idadi ya wahitimu waliopata mafunzo mahala pa kazi ni njia mojawapo ya kukuza ujuzi nchini kwa vijana wetu.”
Amesema wao wanatarajia kuongeza idadi ya wahitimu wenye mafunzo ya uanagenzi kufikia 231,000 ifikapo mwaka 2025/26 kutoka 46,000, mwaka 2019/20, vivyo hivyo na kwa mafunzo tarajari, lengo ni kufikia wahitimu 150,000 ifikapo mwaka 2025/26 kutoka 30,000, mwaka 2019/20.