NA MWANDISHI WETU, DAR ES SALAAM
SIKU chache baada ya kutangazwa kwa mabadiliko ya kanuni utambuzi na usajili ili kuruhusu kuondoa ukomo wa matumizi wa Vitambulisho vya Taifa ( Nida ) kwenye gazeti la serikali , Waziri wa Mambo ya Ndani, Hamad Masauni amesema wamefanya mabadiliko ya kanuni ya kuondoa ukomo huo.
Aidha Waziri Masauni amezitaka benki na Taasisi mbalimbali zinazohitaji vitambulisho vya Nida kutoka kwa raia inatakiwa kutambua mabadiliko hayo .
Masauni ametoa kauli hiyo leo Jumanne wakati akizungumza na wanahabari Jijini Dar es Salaam, kuhusu Mamlaka ya Vitambulisho vya Taifa (Nida) na hali ya utolewaji wa vitambulisho.
Waziri huyo, amesema marekebisho ya kanuni yamekamilika na zimeshaanza kutumika baada ya kutangazwa rasmi katika gazeti la Serikali la Februari 17, 2023.