NA AZIZA MASOUD
SHIRIKA la ndege ya ATCL limekanusha madai yaliyotolewa na Kiongozi Mkuu wa chama cha ACT-Wazalendo Zitto Kabwe kuwa ndege sita kati ya 12 zilizonunuliwa na serikali hazifanyi kazi kwakuwa zina kutu pamoja na kwamba zilinunuliwa mpya.
Akizungumza jijini Mkurugenzi Mkuu wa ATCL Mhandisi Ladislaus Matindi amesema habari hizo si za kweli kwakuwa shirika hilo halina ndege mbovu.
“Ndege mpya zilizonunuliwa na serikali ni 11,ndege ya 12 ilirithiwa kutoka ATCL ni ya zamani,ndege hiyo ilisimamishwa siku nyingi kutokana na masuala ya usalama sasa ipo Macca kwa matengenezo makubwa ambapo mwezi Machi au Aprili itakuwa ikemalizika,”amesema Mhandisi Matindi.
Amesema ndege hiyo haifanyi kazi kwa muda mrefu sasa tangu mwwka 2016 au 2017.
Kwa mujibu wa Muhandisi Matindi kuhusu ndege 11 zilizobaki mchanganuo wake ni kwamba kuna ndege tano ambazo watu wanaziita Bombadier,zipo nne ambazo ni ni Airbus na mbili kubwa za Dreamliner.
“Dreamliner kwa sasa zinafanya safari nne zinaenda India kwa wiki na safari moja kwenda China ,”amesema Mhandisi Matindi.
Amesema kuhusu ndege za kati ambazo ni nne zina matatizo ya injini,watengenezaji wa ndege hizo waligundua kuwa kuna matatizo kwa hiyo baada ya muda injini hizo lazima zifanyiwe maboresho,zinapopelekwa kiwandani yule mtengenezaji anatakiwa atuletee injini za ziada,”amesema Mhandisi Matindi.
Amesema changamoto iiyopo ni kuwa mtengenezaji hana injini za ziada kwakuwa alitengeneza chache na watumiaji wakawa wengi hivyo suala hilo si la ATCL peke yake ni la mashirika mengi.
“Hivyo kati ya ndege nne za saizi ya kati,moja inafanya kazi,mbili zina matatizo ya injini,moja ndio hiyo iliyokamatwa Uholanzi ambayo ni nzima ilienda kwa ajili ya matengenezo wakati inarejea ikakamatwa kutokana na masuala ya kisheria Mwanasheria Mkuu alishalitolea ufafanuzi Bungeni,”amesema Mhandisi Matindi.
Ufafanuzi huo wa ATCL umetolewa baada ya kauli ya Zitto aliyoitoa juzi katika mkutano wa hadhara uliofanyika Mbagala Zakheem ambapo alisema katika miaka saba wananchi walikuwa waambiwa wanajenga nchi serikali ilikuwa inatumia mabilioni ya fedha kununua ndege .
Alisema serikali ilikuwa imatumia Sh. Bilioni 300/- kwa mwaka kwa miaka saba kwa ajili ya ununuzi wa ndege.
“Tuliokuwa bungeni tulikuwa tunahoji serikali ikahamishia suala hilo la ununuzi wa ndege Ofisi ya Rais ili ukihoji uonekane unahoji masuala ya usalama wa Taifa, hivi tunavyozungumza katika ndege 12 za ATCL ndege sita hazifanyi kazi kwa sababu zina kutu kutokana na manunuzi mabovu,”alisema Zitto.