Na Mwandishi Wetu
SAKATA la Mkazi wa Kata ya Mtibwa, Wilaya ya Mvomero mkoani Morogoro, Benjamin Shinda (26) kupigwa risasi na mwajiri wake linazidi kuchukua sura mpya.
Inadaiwa kuwa tukio hilo lilitokea Januari 12 mwaka huu ambako mtu anayefahamika kwa jina la Polycarp Mashelle alimpiga risasi ya mguu Shinda alipokwenda nyumbani kwake.
Shinda alisema Mashelle alimpa trekta kwa ajili ya kulima kwenye mashamba ya wakulima, na mara ya mwisho alienda nalo vijijini likawa linasumbua.
“Siku ya kwanza baada ya kuona linasumbua nikarudi nalo kwa mzee akaninunulia vifaa na kulitengeneza halafu nikarudi tena huko kijijini. Nimekaa kama siku nne hivi nikaona bado linasumbua na sikufanikiwa kulima hata eka moja.
“Sasa siku ya tukio nikafika mpaka nyumbani kwa huyo mzee nikapaki trekta nje na kuingia ndani, nilivyofika nikamuelezea kwamba nimeshindwa kulima kwasababu trekta ni bovu linasumbua ‘hydrolic system’ ambapo haliwezi kunyanyua jembe…akaniambia haiwezekani siku zote hizo niwe sijafanya kazi hivyo akataka nimpe sh. 400,000,” alisema na kuongeza:
“Nikakwambia ni kweli sina hela maana sikuweza kulima kabisa, akasema unanitania, akamwambia kijana wake akafunge geti…akaingia akatoka na bunduki akanipiga risasi ya mguuni. Kuna ndugu zake walikuwepo pale ikabidi wamshike na kumnyang’anya ile bunduki.
“Mimi nikaendelea kugalagala pale chini maana sikuweza tena kutembea na damu zikawa zinavuja. Baada ya muda mchache yule mzee akatoka tena nje na kumwita yule kijana wake na kumwambia anipandishe kwenye pikipiki anipeleke duka la dawa na akifika asiwaambie kwamba nimepigwa risasi, akampa shilingi 20,000 akamwambia apite njia za vichororoni ili watu wasione,”.
Shinda aliongeza kuwa baada ya kufika duka la dawa alimwambia huyo kijana amuache hapohapo, akaomba apewe huduma ya kwanza ya kuzuia damu kuendelea kutoka.
“Baada ya yule kijana kuondoka nikapiga simu kwa ndugu zangu ambapo alikuja mjomba wangu tukaenda kwanza Kituo cha polisi Mtibwa tukapewa PF3 tukaenda hospitali ya Bwagala wakanitoa risasi mbili kisha nikalazwa siku tatu kabla ya nikaruhusiwa.
“Baada ya kutoka hospitali zikapita kama siku mbili hivi polisi wakaja nyumbani walinikuta nipo na baba wakaomba kunichukua niende nao kituoni. Kufika kituoni wakanipa fomu nisaini nikawauliza zinahusu nini maana ziliandikwa Kiingereza na mimi nimeishia darasa la saba hivyo sielewi…akanijibu nisaini tu ili suala liende mbele zaidi,” alisema Shinda na kuongeza:
“Nikampigia kaka yangu yeye anaishi Dar es Salaam akaniambia nimsomee kilichoandikwa nikamwambia sielewi akasema nisisaini. Nikapata taarifa kuwa polisi walienda kwa daktari katika ile hospitali niliyotibiwa na kuchukua zile risasi.
“Baada ya siku chache yule mzee alinipigia akaniambia kwa kuwa nimekataa kusaini zile karatasi basi anasitisha matibabu,”.
Alisema kuwa anacholalamika ni kwamba tangu tukio limetokea polisi wamekuwa wakiwazungusha bila kesi kupelekwa mahakamani.
“Ukiwauliza mara wanakwambia suala liko Kituo cha Polisi Dakawa hivyo tufatilie huko na kuna wakati nilienda hadi kwa RPC Morogoro akaniambia suala hilo halijafika kwake,” alisema Shinda.
Akizungumza na Demokrasia, Mashelle ambaye anadaiwa kumpiga risasi Shinda alisema hawezi kuzungumzia suala hilo kwasababu tayari liko mahakamani.
“Kwa habari zaidi wasiliana na diwani wa hapa pamoja na polisi wa kituo cha Mtibwa, na hii inshu tayari iko mahakamani,” alisema Mashele.
Mkuu wa upelelezi wa Kituo cha Polisi Mtibwa, Dominick Paschal alisema kutokana na sheria suala hilo anatakiwa kulizungumzia Mkuu wa Kituo.
“Kiplotokali mimi siwezi kulizungumzia hili suala kiundani zaidi mwenye mamlaka hayo ni Mkuu wa Kituo ila tu nikwambie kwamba hilo tukio nalijua na mimi ndiye nilikuwa nachunfuza na kesi tayari ipo mahakamani lakini bado haijatajwa.
“Hata juzi alinipigia (Shinda) nikamwambia tayari kesi ipo mahakamani asubirie atapewa summons (wito) wa kwenda mahakamani. Kutokana na kesi ilivyo yeye anasimama kama shahidi na serikali ndiyo inakuwa kama mlalamikaji. Mwambie asiwe anasumbua kama kuna kitu hakielewi afike kituoni kuuliza,” alisema.
Alipoulizwa kama anafahamu suala la kesi hiyo kufika mahakamani, Shinda alisema alisikia tu juu juu.
“Kuna namba nilipewa niongee nayo sijui ni OCD akaniambia kesi tayari iko mahakamani, mimi si nilikataa kusaini akasema na imeshatajwa Jumatatu na itatajwa tena tarehe 27 jambo ambalo lilinifanya nisiamini kwasababu kesi itasomajwe na mimi ndo muhusika mkuu,” alisema Shinda.
Wadau wazungumza
Demokrasia liliwasiliana na Wakili Dickson Matata ambaye alisema ni sawa katika kesi hiyo ambayo ni ya jinai, serikali inakuwa mlalamikaji na mtendewa anakuwa kama shahidi namba moja lakini anapaswa (Shinda) kwenda kufatilia mahakamani kujua kesi hiyo ni namba ngapi na ipo kwa hakimu gani.
“Wanaweza wakawa wanasema hivyo tu lakini kumbe wanadanganya kesi bado haijafika mahakamani, kwahiyo wanatakiwa wawe makini sana katika kufatilia,” alisema Wakili Matata.