NA MROKI MROKI, NEC
TUME ya Taifa ya Uchaguzi (NEC) ilitangaza uchaguzi Mdogo wa Ubunge katika Jimbo la Mbarali na kata sita za Tanzania Bara ambao kwa mujibu wa ratiba utafanyika Septemba 19, 2023. Miongoni mwa watu muhimu ambao watashiriki katika uchaguzi huu ni mawakala wa vyama vya vya siasa.
Wakala wa chama cha siasa ni mwakilishi anayeteuliwa na chama baada ya kupata ridhaa ya mgombea kwa ajili ya kusimamia maslahi ya chama na mgombea.
Kwa mujibu wa kifungu cha 57(1) na (2) cha Sheria ya Taifa ya Uchaguzi, Sura ya 343, na kifungu cha 58(1) na (2), cha Sheria ya Uchaguzi ya Serikali za Mitaa, Sura ya 292, chama cha siasa kinaruhusiwa baada ya kupata ridhaa ya mgombea au wagombea kuteua na kuwasilisha kwa Msimamizi wa Uchaguzi orodha ya majina ya mawakala wa kupiga kura siku saba (7) kabla ya siku ya uchaguzi.
Orodha hiyo itawasilisha pia majina ya mawakala mbadala ambao watatumika iwapo wakala aliyepangwa atapata dharura.
Aidha, kwa mujibu wa kanuni ya 50(4) ya Kanuni za Uchaguzi wa Rais na Wabunge za mwaka 2020, na kanuni ya 43(4) ya Kanuni za Uchaguzi wa Serikali za Mitaa (Uchaguzi wa Madiwani) za mwaka 2020, mawakala wa kupiga kura wanatakiwa kuapa kiapo cha kutunza siri mbele ya Msimamizi wa Uchaguzi siku saba kabla ya Siku ya Uchaguzi kwa kujaza Fomu Na. 6.
Pia, kiapo hiki kitawahusu mawakala mbadala.
Kwa uchaguzi unaotarajiwa kufanyika katika Jimbo la Mbarali na kata sita mawakala wa Vyama vya Siasa na mawakala mbadala wataapa kiapo cha kutunza siri mbele ya Msimamizi wa Uchaguzi Septemba 12, 2023.
Msimamizi wa Uchaguzi huvitaka vyama vya siasa kuwasilisha kwa maandishi majina ya mawakala wa kupiga kura, anuani na vituo walivyopangiwa kufanya kazi.
Kwa mujibu wa kanuni ya 50(6) ya Kanuni za Uchaguzi wa Rais na Wabunge za mwaka 2020 na kanuni ya 43(6) ya Kanuni za Uchaguzi wa Serikali za Mitaa (Uchaguzi wa Madiwani) za mwaka 2020, Vyama vya siasa huwasilisha barua za utambulisho wa kila wakala na kuainisha kituo alichopangiwa kwa Msimamizi wa Uchaguzi.
Barua ya utambulisho wa kila wakala itakayowasilishwa na chama iainishe kituo alichopangiwa na iambatishwe na picha mbili zenye ukubwa sawa na picha iliyopo kwenye pasi ya kusafiria (passport size) zilizopigwa si zaidi ya miezi mitatu.
Kifungu cha 57(3) cha Sheria ya Taifa ya Uchaguzi, Sura ya 343 kimeeleza kuwa chama kitaruhusiwa kuteua wakala mbadala endapo aliyeteuliwa awali amefariki au ameshindwa kutekeleza majukumu ya uwakala.
Sambamba na orodha ya mawakala wa vituo vyama vitawasilisha majina mawili ya mawakala wa ziada kwa Kata ambao watatumika kama wakala mbadala iwapo itahitajika.
Vilevile, endapo wakala hana picha anaweza kuwasilisha nakala mbili za mojawapo ya vitambulisho vifuatavyo ambavyo Tume inavitambua ambavyo ni Kadi ya Mpiga Kura, Kitambulisho cha Taifa, Leseni ya Udereva na Pasi ya Kusafiria.
Siku ya kugawa vifaa vya uchaguzi kwa watendaji wa vituo, Msimamizi wa Uchaguzi atawapatia watendaji hao orodha ya mawakala wa kupiga kura kwa kila kituo husika ambayo itapaswa kubandikwa nje ya vituo vya kupigia kura kabla ya kuanza kwa zoezi la kupiga kura.
Aidha, Msimamizi wa kituo cha kupigia kura hatoruhusiwa kuwaomba Mawakala utambulisho mwingine wa ziada wanapofika katika vituo walivyopangiwa siku ya uchaguzi.
Kuna aina tatu za mawakala kwa mujibu wa majukumu wanayotekeleza.
Mawakala hawa ni Wakala wa kupiga kura; ambaye atashiriki katika zoezi zima la kupiga kura kituoni.
Aidha, wakala wa kupiga kura mara baada ya zoezi hilo kukamilika atabadilika kuwa wakala wa kuhesabu kura.
Wakala wa kuhesabu kura anawajibika kushiriki katika zoezi zima la kuhesabu kura mahala pa kuhesabu kura na Wakala wa kujumlisha kura anawajibika kushiriki zoezi la kujumlisha kura.
Katika kituo cha kupigia kura wakala wa chama cha Siasa atakuwa na wajibu wa kumtambua mpiga kura anayetaka kupiga kura kama ndiye mwenye jina lililoandikwa katika Daftari la Kudumu la Wapiga Kura.
Ikumbukwe kuwa, inashauriwa mawakala watoke katika maeneo ya karibu na vituo watakavyofanyia kazi hiyo ya uwakala.
Wakala anapokuwa kituoni anatakiwa kumwakilisha na kulinda maslahi ya mgombea au wagombea na chama.
Pia, anatakiwa kushirikiana na Msimamizi wa Kituo na Msimamizi Msaidizi wa Kituo katika kuhahikisha kwamba mwenendo wa kupiga kura kituoni unazingatia masharti ya Sheria na taratibu zilizowekwa na atatakiwa kujaza fomu Na.14 na 16 kituoni, kwa mujibu wa Sheria za Uchaguzi.
Aidha, wakala anatakiwa kukiwakilisha chama chake kwenye zoezi la kuhesabu kura baada ya kukamilika kwa zoezi la kupiga kura kwani wakala wa kupiga kura ndiye atakuwa wakala wa kuhesabu kura.
Kila mpewa jukumu au kazi hupewa na mipaka ya utekelezaji wa majukumu husika.
Mawakala wa vyama vya siasa nao wanamipaka ya utekelezaji wa majuku yao wawapo katika vituo vya kupigia kura au kuhesabia kura.
Mawakala wa vyama vya siasa hawaruhusiwi kuorodhesha majina ya wapiga kura kituoni.
Wapo mawakala huacha kufanya kazi zao za msingi vituoni na badala yake huorodhesha majina ya wapiga Kura waliofika katika kituo, jambo ambalo ni kinyume na sheria.
Mbali na hiyo, Mawakala wa vyama vya siasa hawaruhusiwi kutumia simu za mkononi ndani ya vituo vya kupigia kura, kuhesabu kura na kujumlisha kura.
Katika uchaguzi huu mdogo Wagombea 13 kutoka vyama vya siasa 14 vyenye usajili kamili waliteuliwa kuwania kiti cha ubunge Jimbo la Mbarali.
Wagombea walioteuliwa kuwania Ubunge Jimbo la Mbarali na vyama vyao kwenye mabano ni Halima Magambo (AAFP), Osward Mndeva (DP), Zavely Seleka (UDP), Exavery Mwataga (CCK), Mary Daudi (UPDP), Modestus Kilufi (ACT-WAZALENDO), Morris Nkongolo (TLP), Hashim Mdemu (ADC), Fatuma Ligania (NLD), Mwajuma Milambo (UMD), Bahati Ndingo (CCM), Husseni Lusewa (ADA-TADEA) Bariki Mwanyalu (DEMOKRASIA MAKINI).
Mgombea wa Chama cha NRA, Makuke Makuke hakurejesha fomu za uteuzi, hivyo, alikosa sifa za kuteuliwa.
Aidha vyama vya siasa 17 vilijitokeza kuchukua fomu kwaajili ya kuwania nafasi za Udiwani katika kata sita za Tanzania Bara ambapo jumla ya wagombea 45 waliteuliwa kuwania nafasi hizo.
Kata zinazofanya uchaguzi mdogo ni Nala iliyopo Halmashauri ya Jiji la Dodoma, Mfaranyaki iliyopo Halmashauri ya Manispaa ya Songea, Mwaniko iliyopo Halmashauri ya Wilaya ya Misungwi, Old Moshi Magharibi iliyopo Halmashauri ya Wilaya ya Moshi, Marangu Kitowo iliyopo Halmashauri ya Wilaya ya Rombo na Mtyangimbole iliyopo Halmashauri ya Wilaya ya Madaba.
Vyama vyote vinavyoshiriki uchaguzi huu mdogo wa jimbo la Mbarali na Kata sita za Tanzania Bara vinatarajiwa kuweka mawakala katika kila kituo. Ikumbukwe kuwa kukosekana kwa wakala kituoni hakubatilishi zoezi la kupiga kura.
Ni mategemeo ya Tume kuona mawakala waliopewa dhamana na wagombea na vyama kuwawakilisha katika vituo vya Kupigia Kura, kuhesabia kura na hata Kujumlishia kura basi wakifanya kazi yao kwa weledi kwa kufuata sheria, kanuni na taratibu zilizowekwa na Tume.
Kukosekana kwa weledi miongoni mwa mawakala kunaweza kuchochea vurugu na kufanya uchaguzi usiwe huru na wa haki.