NA MWANDISHHI WETU, CHAKE CHAKE, PEMBA
Makamu Mwenyekiti wa ACT-Wazalendo Zanzibar, Mheshimiwa Othman Masoud Othman, amesema Chama hicho kitaendelea kuwa Sauti ya Pekee ya kuwatumikia na kuuwatetea Wananchi wa Unguja na Pemba katika kupigania haki na kuyaepuka madhila yanayowakabili siku hadi siku, hapa Nchini.
Mheshimiwa Othman ambaye pia ni Makamu wa Kwanza wa Rais wa Zanzibar ameyasema hayo leo akihutubia Mkutano wa Hadhara wa Chama chake, hapo katika Viwanja vya Jadida Wete, Mkoa wa Kaskazini, Pemba.
Amesema kuwa hiyo ndiyo ahadi ya msingi kama ambavyo Chama hicho na Viongozi wake wanaamini, pamoja na ukweli kwamba upeo wa ndoto ya wananchi, waliozama katika dimbwi la umasikini hapa Visiwani, ni pamoja na kuiona Zanzibar iliyochakaa, ikirudi katika hadhi, heshima, maendeleo, na mamlaka yake kamili ya kujitawala, pasi na utegemezi wala hali ya kumezwa iliyopo sasa, chini ya kivuli cha Muungano wa Tanzania.
Amefahamisha kuwa nje ya Umoja na Mamlaka yake Kamili, Nchi hii itabaki kuwa dhalili, ombaomba na iliyodumaa kimaendeleo, nyuma ya hata ‘vijinchi vidogo’ ambavyo si lolote si chochote mbele ya hadhi iliyokuwa nayo Zanzibar hapo zamani.
Ameeleza kuwa kukosekana kwa yote hayo, ndiko kunakopelekea Zanzibar kudumaa kimaendeleo, huku Wazanzibari wakiendelea kushuhudia Nchi yao ikizidi kuendeshwa kwa misingi ya chuki, ubaguzi, ubinafsi, maonevu na maafa kila kipindi cha chaguzi kwa sababu ya kuwapatia watu wachache madaraka.
Ametolea mfano kukosekana kwa Mamlaka Kamili ya Zanzibar na athari zake, ni mithili ya mtu ambaye ameng’olewa meno na ufizi wake, kwani kwa sasa Serikali hapa Visiwani imepoteza kila kitu katika uhuru wake kwa kisingizio cha Muungano, kuanzia wa kujiendesha, kukusanya kodi, na hata uwezo wa kukopa.
Hivyo amesema kuwa Chama chake kimedhamiria kutekeleza azma hiyo, na kinaihamasisha kwa makusudi, kupitia Mfululizo wa takriban Mikutano Kumi na Mbili, ya kuitangaza pia Sera yao ya sasa ya ‘Zanzibar Mpya, Zanzibar Moja, yenye Mamlaka Kamili,’ kote Unguja na Pemba.
“Sisi tunasema chini ya Mamlaka kamili hakuna mwananchi wa Zanzibar atakayedhulumiwa haki yake na lazima afaidi matunda ya raslimali zilizomzunguka katika Nchi hii”, amefahamisha Mheshimiwa Othman akisisitiza mtazamo wake juu ya namna ya kuinua pato linalotokana na Zao la Biashara la Karafuu ambalo ni mashuhuri hapa, kwa wazalishaji wake.
Akiweka msisitizo juu ya madhara ya ubaguzi na ukandamizaji katika Nchi, Mheshimiwa Othman, ambaye katika Ziara yake ya takriban Siku Nne kisiwani hapa, ameambatana na Mke wake, Mama Zainab Kombo Shaib, amefahamisha akisema “leo mwenye elimu ananyimwa fursa ya kuajiriwa kwasababu ya itikadi yake: na hata baadhi wanakoseshwa fursa ya kuwekeza kutokana na asili ya anakotokea”.
Hivyo amesema kuwa ahadi ya Chama chake ni kuendeleza dhamira ya kuipigania mamlaka ya Nchi, ambapo wananchi hawana budi kuungamkono juhudi hizo, ili kuyakomesha hayo.
Naye, Kaimu Naibu Katibu Mkuu wa ACT-Wazalendo Zanzibar, Bw. Salim Bimani, amepaza Sauti kwa Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar, kufanya huruma kwa kuwapatia Wananchi wa kisiwa cha Pemba, Usafiri wa uhakika, ili kuepusha kile alichokitaja kuwa ni kuepusha maafa ya mara kwa mara yanayowapata, pale wanaposafiri katika mwelekeo wa maeneo mbali mbali yakiwemo ya Mkoa wa Tanga Tanzania Bara, kwa kutumia njia ya bahari.
Kwa upande wake, Mjumbe wa Kamati Kuu ya ACT-Wazalendo, Bw. Ismail Jussa Ladhu amekumbusha heshima ambayo Wilaya ya Wete imeiweka kihistoria kuwa ndicho Kitovu cha Vuguvugu la Siasa za Upinzani, ndani ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania.
Amehimiza kuwa, jambo la muhimu ni kuendelea kuenzi juhudi za Waasisi wa Vuguvugu hilo, ambalo lilikuja kuweka msingi wa kuitetea na kuilinda Nchi, akiwemo aliyewahi kuwa Makamu wa Kwanza wa Rais wa Zanzibar, na Kiongozi wa Chama hicho, Marehemu Maalim Seif Sharif Hamad.
Jussa amelaumu kile alichobainisha kuwa ni mapungufu yanayodhoofisha maendeleo ya Nchi yakiwemo ufisadi, ubadhirifu wa mali ya umma na ubaguzi, hali inayozidisha ugumu wa maisha akisema, “hayo hayakubaliki na kwa hali hii hakuna linalokuwa”.
Viongozi mbali mbali wa Chama hicho wamehudhuria katika Mkutano huo akiwemo Mratibu wa ACT-Wazalendo kisiwani Pemba, Mhe. Said Ali Mbarouk; na Mwenyekiti wa Mkoa wa Wete Kichama, Bw. Juma Khamis.
Mkutano huo ni muendelezo wa Mikutano ambayo Chama hicho kimeitambulisha kuwa ni ‘Darasa’ la kuwaelimisha na kuwaeleza wananchi juu ya changamoto na masaibu ambayo yanawakabili, na wajibu wa kuendelea kuyapazia sauti ndani ya Nchi yao, sambamba na kuifikisha ile dhana ya ”Zanzibar Mpya, Zanzibar Moja yenye Mamlaka Kamili”, kwa watu wote.
Vikundi mbali mbali vya burudani vimetumbuiza katika Mkutano huo, kikiwemo Kikundi cha Ngoma ya Asili ya Msewe, kutoka Kijiji cha Mchangamdogo kisiwani Pemba.