NA MWANDISHI WETU, MWANZA
JESHI la Polisi Mkoa wa Mwanza limetangaza operesheni maalum wa kudhibiti tabia ya baadhi ya madereva wa magari madogo ya abiria maarufu kama daladala kukatisha safari.
Pamoja na usimamizi na utekelezaji wa sheria na kanuni za usalama barabarani, hatua hiyo pia inalenga kulinda maslahi ya abiria ambao wakati mwingine hulazimika kulipa nauli mara mbili kwa safari moja kutokana na daladala kutofika mwisho wa safari.
Akizungumza wakati wa kikao kazi kati ya Jeshi la Polisi na madereva wa daladala jijini Mwanza leo Alhamisi Machi 30, 2023, Kamanda wa Polisi Mkoa wa Mwanza, Wilbroad Mutafungwa amesema madereva watakaonaswa kwa kosa hilo watatozwa faini na watakaorudia watanyang’anywa leseni.
Kamanda Mutafungwa ametangaza uamuzi huo baada ya kupokea malalamiko ya daladala kukatisha safari kutoka kwa baadhi ya abiria waliokuwepo Kituo cha mabasi cha Natta jijini Mwanza.
Njia zinazodaiwa kukithiri kwa tabia ya daladala kukatisha safari ni Kisesa – Nyashishi, Airport -Nyashishi na Ilalila -Nyashishi.
Katika operesheni hiyo, Kamanda Mutafungwa amesema Jeshi la Polisi Kitengo cha Usalama barabarani kitashirikiana na maofisa wa Wakala wa Usimamizi Usafiri Ardhini (Latra).
“Kuanzia sasa tutabandika namba za viongozi wa Jeshi la Polisi katika daladala zote kuwezesha wananchi kutoa taarifa za uvunjifu wa sheria na kanuni za usalama barabarani,” amesema Kamanda Mutafungwa
Ofisa wa Latra Mkoa wa Mwanza, Vitalino Ngonyani amewataka wamiliki wa daladala kusimamia utendaji kazi wa madereva wao ili kuepusha magari yao kufutiwa leseni za usafirishaji pindi yatakapobainika kuhusika kwenye makosa yanayojirudia.
Ametaja adhabu kwa kosa la kukatisha safari kuwa ni Sh.100, 000 kwa mujibu wa kanuni ya leseni ya usafirishaji magari kwa abiria kifungu cha 24 d (e).
Ramadhan Twaha, mmoja wa madereva wa daladala jijini Mwanza amefichua sababu za baadhi ya daladala kukatisha safari kuwa ni kusalia na abiria wachache kabla ya kufika mwisho wa safari.
Mwenyekiti wa Madereva wa daladala Jijini Mwanza, Mjarifu Manyasi ameahidi kuwa umoja huo utashirikiana na mamlaka za Serikali kusimamia nidhamu na utii wa sheria miongoni mwa wanachama wake huku akiwataka madereva wote kuzingatia sheria na kanuni za usalama barabarani bila shurti.
Mkuu wa Kikosi cha Usalama barabarani Mkoa wa Mwanza, Sunday Ibrahim amesema utekelezaji wa maagizo hayo unaanza rasmi leo na kuwataka madereva wote mkoani Mwanza kutii sheria bila shurti huku akionya kuwa Jeshi la Polisi halitakuwa na muhali kwa watakaokwenda kinyume.