NA MWANDISHI WETU
JUMUIYA ya Wazazi ya Chama Cha Mapinduzi (CCM) Mkoa wa Dar es Salaam imeunda Kamati ndogo za Jumuiya hiyo ili kuhakikisha dira ya Mkoa inasimamiwa na kutekeleza mipango kazi ambayo wamejiwekea kwa miaka mitano.
Kamati ambazo zimeundwa na kutangazwa ni Kamati tano ambazo ni Kamati ya Miradi, Uchumi na Maendeleo, Kamati ya Utamaduni, Michezo na Mazingira, Kamati ya Elimu, Afya na Malezi, Kamati ya Nidhamu na Maadili pamoja na Kamati ya Habari za Jumuiya.
Akizungumza katika hafla ya kuwakabidhi barua za uteuzi Wanakamati mwishoni mwa wiki jijini Dar es Salaam, Mwenyekiti wa Jumuiya ya Wazazi (CCM) Mkoa Dar es Salaam, Khadija Said alisema anategemea ushirikiano mkubwa kutoka kwenye Kamati zilizoundwa na kuhakikisha kazi za Jumuiya ya wazazi ndani ya mkoa wa Dar es salaam zinafanyika vizuri.
Kuhusu Kamati ya Elimu, Afya na Malezi, Khadija alisema wao kama Jumuiya
ya Wazazi, malezi ni ajenda yao kitaifa, ndiyo maana wanakuja na Kaulimbiu ya ‘Malezi bora kwa Mtoto’, Faraja ya Kesho ya Mzazi na Taifa’, ambapo Kamati hiyo ina Wataalamu ambao wataenda kufanya mafunzo kwa viongozi wa ngazi ya kata, pia Kamati hiyo ina viongozi wa kiroho.
“Kamati hii inaenda kusimamia mambo ya msingi sana ya malezi na maadili lakini pia suala zima la elimu kuhakikisha ufaulu wa Mkoa wa Dar es Salaam wa
Watoto wa Shule za Msingi na Sekondari unaongezeka, lakini tunaenda kuanzisha Shule za awali ambayo kupitia hii Kamati wataweza kutuanzishiaumuhimu wa Shule za awali katika ngazi ya Kata, Wilaya lakini kuhakikisha kwamba jumuiya ya wazazi inasimamia Elimu katika ubora wake na afya vilevile,” alisema Said
Aidha, alisema Kamati ya Miradi, Uchumi na Maendeleo inaenda kusaidia kwa kiwango kikubwa ndani ya mkoa kwani katika sera za Siasa na Uchumi lazima kuwe na Miradi ambayo iko katika hali sahihi na watafanya kazi katika miradi ambayo Jumuiya ya Wazazi itaweza kubuni.
Pia alisema kusimamia na kuiongoza kuhakikisha wanabadilisha hali ya wanajumuiya wake katika ngazi ya Kata, Wilaya na Mkoa lakini pia kufanya miradi ambayo inapeleka jumuiya na Chama cha Mapinduzi moja kwa moja na wananchi katika kuongeza kipato chao.
Pamoja na hayo, miongoni mwa Kamati ambazo zimeundwa, kuhusu Kamati ya
Utamduni, Michezo na Mazingira, amesema kuwa katika kujenga mahusiano yetu lazima tuingie kwenye michezo, kwahiyo watakuwa na timu za wazazi katika kata zao, watakuwa na mashindano ya michezo mbalimbali katika kata, wilaya na katika ngazi ya mkoa.
“Tunategemea kama tukifanya vizuri kuingia na kwenda hata nje ya nchi kupitia timu zetu , na hii ni kwaajili ya kupanua wigo wa mahusiano kati ya Chama lakini pia na wananchi wake kwahiyo michezo ndio sehemu peke yake watu wanakutana kwa pamoja”,
“Na sisi jumuiya ya wazazi tutafanya kazi na mtu yoyote mwenye nia njema naTanzania, hasa katika kuhakikisha malezi ya watoto na vijana wetu yanapewa kipaumbele. Ndio maana kamati hizi zimejumuisha makundimbalimbali ya kijamii, sio kamati za kishabiki.” alisema.
Kwa upande wake, Mjumbe wa Kamati ya Elimu, Afya na Malezi, Ismail Sadick (Suma Lee) alisema atajitahidi kushirikiana na wajumbe wengine kuhakikisha suala la elimu na malezi linakuwa bora katika Mkoa wa Dar es
Salaam kwasababu katika Kamati hiyo wapo viongozi wa kiimani ambao pia
ataenda kushirikiana nao.