NA MWEHA MSEMO, DAR ES SALAAM

NI majira ya saa tano asubuhi, jua tayari linawaka katika viunga vya mtaa wa Mshikamano, Mbezi Louis, Dar es Salaam.
Katikati ya taka zilizochanganyika, kijana Dunstan Mazinge (29) anachambua chupa za plastiki akitafuta zile anazoweza kuuza.

“Mimi hizo nyeusi huwa sizichukui, hazina pesa,” anasema
Kijana Mazinge hukusanya zaidi chupa zisizo na rangi za Polyethylene Terephthalate (PET), zinazotumika kuhifadhia vinywaji.

Pia hukutana na plastiki ngumu za High-Density Polyethylene (HDPE), zinazotumika kutengeneza ndoo,madumu na viti, lakini huzipata mara chache zaidi.

Ingawa baadhi ya plastiki za HDPE zinaweza kuuzwa kwa bei kubwa zaidi kwa kilo kuliko PET, kwa Mazinge kinachoamua anachokusanya ni thamani yake sokoni na upatikanaji wa mnunuzi bei inaamua kinachochukuliwa.
Zuberi Shekazi (53) hununua plastiki kutoka kwa waokota taka kama Mazinge na kuziuza kwa wanunuzi wakubwa.
“Nikiuza kilo moja ya plastiki isiyo na rangi kwa Sh. 700, ile nyeusi inaweza kuuzwa Sh. 300 tu. Unaweza kuwa na mzigo mkubwa, lakini mwisho wa siku pesa huioni,” anasema.
Kwa mujibu wa Henry Kazula, Mratibu wa Chama cha Wachakataji wa Taka Tanzania (TARA), chupa za PET zisizo na rangi zinaweza kutumika kutengeneza bidhaa nyingi zaidi baada ya kurejelewa kuliko zile zenye rangi.
“Sababu kuu ni kwamba kemikali ya rangi kwenye chupa hizo haiwezi kuondolewa kwa urahisi katika michakato ya kawaida ya urejelezaji. Hii inafanya PET zisizo na rangi kuwa na thamani zaidi kwa wachakataji kwakuwa hazitumii gharama kubwa kuchakatwa” anasema Kazula.
Shekazi anasema baadhi ya plastiki hukataliwa na viwanda, ingawa hajui sababu zote.
Wakati mwingine humchukua zaidi ya mwezi kukusanya tani moja, huku waokota taka wakishindania plastiki zenye bei nzuri.
“Kwa sasa tuko wengi tunaofanya kazi hii, na plastiki zenye bei nzuri tunalazimika kuzishindania huko mitaani,” anasema.
BEI YA PLASTIKI HUTEGEMEA SOKO LA VIWANDA VINAVYONUNUA
Ramadhani Kamote, meneja wa Cheng Xin Investment Co. Ltd, anasema kiwanda hicho hununua PET kwa Sh. 500 hadi 600 kwa kilo, ingawa wakati mwingine bei hushuka hadi Sh. 200.
“Inategemea na msimu tu. Kipindi cha joto plastiki zinakuwa nyingi na bei inaweza kuwa ndogo, na wakati wa baridi chupa zinaweza kuadimika hivyo bei ikapanda,” anasema.
Kiwanda hicho huchakata aina mbalimbali za plastiki, zikiwemo za rangi, na kuuza malighafi kwa wazalishaji ndani na nje ya nchi.
Kamote anakadiria kuwa hukusanya takriban tani 150 za plastiki kwa mwezi.Kwa hiyo, plastiki inapokuwa na bei ndogo sokoni, ukusanyaji wake unaweza kukosa faida ya kutosha kwa waokota taka.
Baadhi ya plastiki huishia kubaki kwenye mkondo wa taka, hata kama zinaweza kuchakatwa.
GHARAMA YA TAKA ZA PLASTIKI
Kwa mujibu wa tathmini ya Umoja wa Kimataifa wa Uhifadhi wa Mazingira (IUCN), Tanzania ilizalisha wastani wa tani 315,000 za taka za plastiki mwaka 2018.
Ni asilimia 34 pekee iliyokadiriwa kukusanywa,huku karibu tani 29,000 zikikadiriwa kuishia baharini, kwenye mito na maziwa.Madhara ya taka hizo yanaonekana katika maisha ya kila siku.
Rashida Awadhi, mkazi na mfanyabiashara wa chakula Kimara Temboni, anasema taka huziba mitaro na kuchangia mafuriko wakati wa mvua.
“Yaani hapa ikifika kipindi cha mvua unajiuliza haya makopo yote yametoka wapi, maana maji yanafurika kila mahali, mitaro inapozibwa na haya makopo. Si tu kwamba yanatuletea kero kwenye biashara zetu, maana hata wateja wakiona hali ya uchafu hawaji,” anasema Awadhi.
Reinhard Kidali, mtumiaji wa ufukwe wa Msasani, maarufu kama Beachmavi, anasema taka za plastiki zinaharibu mazingira ya fukwe na kuibua wasiwasi kuhusu usalama wa watoto wanaozitembelea.
“Unaweza kuja hapa na familia halafu ukakuta kuna uchafu wa kila aina, hasa hizi plastiki, hadi unajiuliza zinatokea wapi na unaanza kupata wasiwasi kama umeleta watoto sehemu salama kwa afya zao,” anasema.
Abdi Khalifa, mratibu wa mradi kutoka shirika la Human Dignity and Environmental Care Foundation (HUDEFO), tatizo ni pengo kati ya kiasi cha plastiki kinachoingia sokoni na uwezo wa mfumo wa kukusanya na kuchakata taka hizo.
“Tatizo si plastiki tu ambazo hazina thamani sokoni. Tatizo ni pengo kati ya kiasi cha plastiki kinachoingia kwenye matumizi kila mwaka na uwezo wa mfumo wa kukusanya, kuchakata na kuzirudisha kwenye uzalishaji,” anasema.
Utafiti wa Benki ya Dunia wa mwaka 2023, uliochapishwa chini ya mpango wa PROBLUE, ulikadiria kuwa uchafuzi wa plastiki katika maeneo ya pwani ya Dar es Salaam ulisababisha hasara ya kiuchumi ya Dola za Marekani milioni 10.33 mwaka 2019.
Zaidi ya nusu ya hasara hiyo ilihusishwa na utalii. Gharama za kiafya zilikadiriwa kuwa Dola milioni 2.2, huku vifo 41 vya mapema vikikadiriwa kuchangiwa na uchafuzi wa plastiki.
Ripoti ya Mdhibiti na Mkaguzi Mkuu wa Hesabu za Serikali (CAG) iliyotolewa mwaka 2025 kuhusu utekelezaji wa mapendekezo ya ukaguzi wa udhibiti wa uchafuzi wa taka za plastiki ilibaini kuwa takribani asilimia 25 ya mapendekezo yaliyotolewa hayakuwa yametekelezwa.
Ripoti hiyo ilihimiza Ofisi ya Makamu wa Rais, serikali za mitaa na Baraza la Taifa la Hifadhi na Usimamizi wa Mazingira (NEMC) kuimarisha utekelezaji na ufuatiliaji.
WAJIBU WA WAZALISHAJI
Hata hivyo, mbali na wajibu wa mamlaka za umma, kampuni zinazoweka bidhaa zilizofungashwa kwa plastiki sokoni zinapaswa kuwajibika baada ya bidhaa hizo kutumika.
Kanuni ya 29 ya Kanuni za Usimamizi wa Mazingira (Marufuku ya Mifuko ya Plastiki na Lakiri za Chupa za Plastiki) za mwaka 2022 inaweka wajibu kwa watengenezaji au wasambazaji wa bidhaa zilizofungashwa kwenye chupa za plastiki kuanzisha, kuendesha au kushiriki katika mfumo wa kukusanya chupa hizo baada ya matumizi, kwa ajili ya urejelezaji au utupaji.
Kanuni hiyo pia inasema kuwa huduma hiyo haipaswi kutozwa bei ya ziada.Hata hivyo, mfumo huo si sawa na uwajibikaji mpana wa mtengenezaji baada ya bidhaa kuwa taka (Extended Producer Responsibility — EPR).
EPR inaweza kuwapa wazalishaji wajibu wa kusaidia kugharimia ukusanyaji, urejeshaji na urejelezaji wa bidhaa zao.
Mhandisi Luhuvilo Mwamila, meneja wa utekelezaji wa sheria wa NEMC, anasema mfumo wa sasa una mapungufu katika kufuatilia kiasi cha plastiki kinachoingizwa sokoni na kila mzalishaji, pamoja na kiasi kinachokusanywa au kuchakatwa baadaye.
“Mfumo imara zaidi wa uwajibikaji wa wazalishaji unapaswa kuweka wazi kiasi ambacho mzalishaji ameweka sokoni, kiasi anachotakiwa kukusanya, nani analipia ukusanyaji na urejelezaji, na utekelezaji wa wajibu huo unathibitishwaje?” anasema.
KWA WAOKOTA TAKA SUALA LA NANI LA ANAYELIPIA UKUSANYAJI WA MOJA KWA MOJA NA KIPATO CHAO?
Tina Mfanga wa Mtandao wa Waokota Taka Dar es Salaam (MTAWADA) anasema wanahitaji mfumo wa uhakika wa kuwalipa wanaokusanya bidhaa za wazalishaji mitaani.
“Lakini pia ni muhimu sana wazalishaji wawe na vituo vya kuchakata bidhaa wanazozalisha, ili kile wanachoweka sokoni kiweze kuchakatwa,” anasema.
Katika soko la PET, PETpro ni mfano wa mpango wa hiari unaofadhili ukusanyaji wa plastiki baada ya matumizi.
Utafiti wa HUDEFO kuhusu EPR unaeleza kuwa mpango huo, ulioanzishwa mwaka 2022, ulitoa fedha kwa wakusanyaji kununua chupa za PET zenye rangi na kuzisafirisha hadi vituo vya urejelezaji.
Nicholaus Ambwene, mratibu wa PETpro, anasema wajibu wa wazalishaji hauishii chupa inapouzwa.“Ni wajibu wa wazalishaji kukusanya na kurejeleza chupa za PET baada ya matumizi,” anasema.
Hata hivyo, PETpro ni mpango wa hiari, si mfumo wa lazima wa EPR.
Tathmini ya Shirika la Umoja wa Mataifa la Maendeleo ya Viwanda (UNIDO) ya mwaka 2026, iliyotumia taarifa zilizotolewa na PETpro, inaeleza kuwa mpango huo ulikusanya tani 21,000 za chupa za PET zenye rangi kati ya Februari na Machi 2025.
Kati ya mwaka 2022 na 2025, ulikusanya pia tani 45,000 za chupa zisizo na rangi, ambapo tani 32,000 zilirejelewa.
Chupa zilizokuwa bado kiwandani wakati taarifa zilipokusanywa hazikujumuishwa.
UNIDO ilieleza kuwa haikuthibitisha taarifa zote zilizotolewa na PETpro.
Tathmini hiyo ilikadiria kuwa wanachama wanane wa PETpro kwa pamoja waliwakilisha asilimia 80 hadi 85 ya soko la chupa za PET za vinywaji nchini Tanzania mwaka 2025.
Wanachama hao ni Nyanza Bottling, Coca Cola Kwanza, Bonite Bottlers, SBC Pepsi, Sayona Drinks, Cool Blue, A-One Products & Bottles Ltd – MeTL, na SilAfrica Ltd.
Hata hivyo, sehemu kubwa ya soko haimaanishi moja kwa moja kuwa kampuni inakusanya kiasi kikubwa cha taka zinazotokana na bidhaa zake.
Utafiti uliofanywa Julai 2026 na wataalamu wa taasisi ya utafiti ya Norway (NORCE), kwa kushirikiana na Chuo Kikuu cha Dar es Salaam, ulichunguza taka za plastiki zenye alama za wazalishaji katika maeneo 69 kandokando ya mwambao wa Tanzania wa Ziwa Victoria, Tanganyika na Nyasa.
Utafiti huo ulichapishwa katika jarida la Environmental Science and Pollution Research.
Watafiti walibaini kuwa Jambo Group of Companies, Bakhresa Food Products Ltd na MeTL Group zilihusishwa na asilimia 52.9 ya taka za plastiki zenye alama za wazalishaji zilizochunguzwa.
Kwa ujumla, wazalishaji 29 walihusishwa na asilimia 95.1 ya taka hizo.
Matokeo hayo yanaonesha kampuni ambazo bidhaa zake zilitambuliwa kwenye taka zilizokusanywa katika maeneo yaliyofanyiwa utafiti.
Hata hivyo, takwimu hizo pekee hazionyeshi kiasi ambacho kila kampuni ilikusanya au kuchakata kupitia mifumo yake.Kwa Khalifa, kipimo kingine muhimu ni kama kiwango cha urejelezaji kinaendana na kiasi cha plastiki kinachoingizwa sokoni.
“Swali la msingi ni: je, wanachakata taka wanazozalisha, na wanazichakata kwa kiwango kinachoendana na kiasi wanachozalisha? Hapa ndipo ninapoona kuna udhaifu,” anasema.
KAULI YA WAZALISHAJI
Joseph Ouma, mratibu wa mazingira wa Azam EPR Scheme, anasema Bakhresa Group inaendesha mpango wa majaribio wa kukusanya plastiki katika wilaya tano za Dar es Salaam.
“Chupa ambazo tumeweza kukusanya kwa kipindi cha Septemba 2024 hadi Septemba 2025 zilikuwa tani 100. Na kwa kipindi cha kuanzia Septemba 2025 hadi sasa, tukielekea kwenye tathmini, tayari tunaona zimeongezeka na kufikia tani 130,” anasema Ouma.
Anasema mpango huo ulianza kwa kukusanya chupa za PET zenye rangi, kutokana na msisitizo wa mamlaka kuhusu chupa hizo.
Kampuni hukusanya pia plastiki za wazalishaji wengine, ikishirikiana na wanunuzi wa kati.
“Lengo letu tukianza rasmi ni kuhakikisha ndani ya miaka mitatu tuna uwezo wa kukusanya angalau asilimia 40 ya kile tunachokizalisha,” anasema.
Ouma hakutoa kiasi cha plastiki ambacho kampuni huzalisha kwa mwaka, akisema ni taarifa za ndani.
Alieleza kuwa lengo la asilimia 40 litategemea kiasi cha bidhaa kinachowekwa sokoni, maeneo yanayofikiwa na uwezo wa ukusanyaji.
Jambo Group ilitafutwa kwa simu na mwandishi wa makala hii kati ya Septemba 22 na Oktoba 5, huku Watercom, mzalishaji wa maji ya chupa, ikitafutwa kati ya Septemba 25 na Oktoba 12 ili kutoa maoni.
Kampuni hizo hazikujibu hadi makala hii inachapishwa.
NINI KINAFUATA?
Mapema Julai 2026, NEMC na IUCN ziliomba maoni ya wadau kuhusu rasimu ya kanuni za EPR.
NEMC ilisema mfumo unaopendekezwa utaweka wajibu kwa wazalishaji kusimamia taka zinazotokana na bidhaa zao.
Hata hivyo, bado haijulikani kanuni hizo zitakamilika lini.
Kwa waokota taka, changamoto ni kuhakikisha wajibu huo unatekelezwa na gharama za ukusanyaji haziwaachii mzigo watu wanaotegemea kuuza plastiki ili kujipatia kipato.
Katika mtaa wa Mshikamano,Mazinge ataendelea kuchambua taka zilizo mbele yake,Chupa ambazo ana uhakika wa kuziuza ataziweka kwenye gunia lake na nyingine ataziacha hapo hapo.

