Simba wataondoka watu
-Mgunda, Chama, Manula watajwa
Na Wiliam Kapawaga na Abdallah Mensah
BAADA ya Klabu ya Simba kuanza kwa vipigo viwili katika michuano ya Klabu Bingwa Afrika, wadau wa soka nchini wameibuka na kutoa maoni yao ili wekundu hao wa Msimbazi wafanye vyema.
Baadhi yao wamesema kuwa, pengine angeachiwa timu Mgunda katika hatua hii ya makundi inawezekana wangepata matokeo mazuri na kujiweka sawa katika mbio za kutinga robo fainali.
Pia, wamekaririwa wakiamini kwamba kitendo cha Kocha Roberto Oliveira ‘Robertinho’ kumhamisha Clatous Chama kwenda pembeni, nacho ni sehemu ya kupunguza uwezo wa mchezo huyo kutengeneza nafasi za kufunga.
Wanadai kwamba, uwezo wa kocha unaonekana kuharibu mfumo wa Simba walioanza nao katika hatua ya awali chini Mgunda jambo ambalo linatakiwa kufanyiwa kazi mapema na kama itaendelea hutua hii ndio mwisho wake.
Pia, kauli mbiu ya kwamba kwa Mkapa hatoki Mtu inaelezwa nayo ni sehemu iliyoharibu akili ya wachezaji wakiamini kuwa wanaweza kushinda mchezo wowote wakiwa nyumbani jambo ambalo si kweli.
Kwa sasa Simba tayari inashika mkia katika kundi lake, hivyo inaanza kutafuta alama katika mchezo ujao Februari 25 nchini Uganda dhidi ya Vipers, hivyo ni vema wakaanza kujipanga vema.
Mshambuliaji wa zamani wa Simba, David Mihambo alisema pamoja na matokeo mabaya waliyoyapata timu yake bado wanaweza kusahihisha makosa iwapo watafanya vizuri mechi zilizobaki.
Alisema, Simba ikifanikiwa kuifunga Vipers ya Uganda kwa mechi zote mbili watafufua matumaini ya kufuzu robo fainali hivyo kinachotakiwa ni kocha mkuu kushirikiana vema na msaidizi wake Juma Mgunda kuhakikisha wanafanikiwa.
“Ingawa naamini Kocha Mgunda alitakiwa kuaminiwa katika hatua hii ya makundi na baada ya kuongezewa wachezaji katika dirisha dogo na ninaamini angefanikiwa,” alisema.
Pia, wachezaji wanatakiwa kutojisikia wanyonge na waangalie zaidi michezo ya mbele na kusahau matokeo dhidi ya Raja baada ya kukubali kipigo cha mabao 3-0 kwa maana Simba hii si ya miaka miwili iliyopita.
Nyota huyo, aliyekuwa katika kikosi cha mwaka 1993 kilichoingia fainali ya Kombe la CAF, ameushauri uongozi kufanya usajili wa wachezaji bora wenye ushindani hasa wa kucheza michuano mikubwa ya kimataifa.
Pia, Mkurugenzi wa Mashindamo wa Shirikisho la Soka Tanzania (TFF), Salum Madadi alisema hatua ambayo wamefika Simba ni kubwa, hivyo wanatakiwa kuwa makini .
“Simba ni timu kubwa, hivyo inapaniwa na timu nyingi kubwa Afrika kwa kila mchezo wanaocheza wanatakiwa kufanya nia kutobweteka wacheze kama fainali,” alisema.
Madadi, alisema kuwa Simba isijiamini na kauli yao ya kwa Mkapa Hatoki Mtu ambayo imekuwa ikiwaaminisha wana Simba.
Alisema kuwa, iwapo Simba haitofanikiwa kutinga robo fainali uongozi na benchi la ufundi wanatakiwa kukijenga kikosi ili kiwe imara kama ilivyo miaka miwili ya nyuma.
Kwa upande wa beki wa zamani wa klabu hiyo ,Boniface Pawasa, alisema Simba izungumziwe kwa ujumla wake na wala si kwa mchezaji mmoja mmoja ama kuwalinganisha makocha.
Pawasa alisema, malengo ya Simba kufika nusu fainali, inatakiwa kufika uwezo wa Raja aliodai ni bora kuanzia kwenye muunganiko wa timu na viwango vya wachezaji wake.
“Mwalimu anaweza akawa sahihi linapokuja suala la ufundishaji, lakini je, wachezaji wanaendana na kiwango cha mashindano husika? Hapo hata kama kocha angekuwa Mgunda, kwa kikosi cha Raja Simba bado isingefanya chochote,” alisema Pawasa.
“Simba walikosea kwa kutowaheshimu Raja, waliishi kwa mazoea ya kwamba kwa Mkapa Hatoki Mtu na mazoea hayo ndio yaliyowaponza. Lakini pia niseme, Simba inatakiwa ijifunze kwa Raja kama inatamani mafanikio ya kufika fainali au nusu fainali badala ya kuendeleza mazoea.”
Alisema kuwa, ukitazama aina ya wachezaji, kujiamini kitimu, muunganiko na ubora bado Simba ni timu nzuri ila inapaswa kuangalia wachezaji wa kwenda kucheza nao kwenye Klabu Bingwa.
“Simba ikubali ikatae, ilikosea kwenye usajili. Huwezi kumpoteza mtu kama Luis Miquissone anayekupa magoli 21 na assist 42, ukaenda kumnunua mchezaji kama Banda au Sakho ambao hawakufishi kwa Miquissone, halafu bado una ndoto ya kufika nusu fainali.”
Pawasa aliendelea kusema kuwa, Simba pamoja na timu zote za Tanzania zinatakiwa zijifunze kutoka kwa Raja kuanzia uwekezaji wao na namna ilivyofanya hadi kufanikiwa licha ya kwamba iliwahi kupotea miaka minne nyuma.
Kadhalika, mwanachama mwingine wa Simba, Salum Ndoka alisema kuwa anafikiri ilikuwa ni sahihi kumuacha Kocha Juma Mgunda kuendelea kubaki kwenye benchi la ufundi, hasa kwa kuwa wachezaji walishaanza kumuelewa.
Naye, Mwanachama wa klabu hiyo ambaye ni mdau wa kuinua vipaji vya soka wilayani Temeke, Mustafa Said ‘Musti’ alikosoa mipango ya Kocha kumuacha benchi Phiri na kuamua kumuanzisha, John Bocco.
“Ifike wakati pia lazima tumuamini Beno Kakolanya na tumpumzishe, Aishi Manula kwasababu amekuwa akijisahau mara kwa mara na kujiamini kupita kiasi, ambapo imefikia hatua anafanya makosa ya kizembe,” alisema Musti.
Mwanachama mwingine wa klabu hiyo kutoka Tawi la Simba SC Mwajasi Machimbo Vikindu, Pwani, Godfrey Mshiu, alisema bado timu haina kikosi bora cha kuifikisha timu nusu fainali ya michuano ya Klabu Bingwa Afrika kwa sasa.
“Tumefungwa mechi ya kwanza, tumejua kosa lilipo halafu bado tunakuja tena kupigwa mechi ya pili! Simba na Yanga haziwezi kufika mbali kwa usajili wa kuungaunga.. angalia namba sita wa Raja leo (juzi), alivyoupiga mwingi, halafu uje umfananishe na Putin au Sawadogo wajiangalie msimu ujao anaweza kuondoka mtu hata kabla ligi kuisha,” alisema Mshiu.