NA MWANDISHI WETU,DAR ES SALAAM
KAMISHNA Jenerali wa Uhamiaji nchini, Dk. Anna Makakala, leo Julai 6 ,2026 ametembelea Banda la Ubalozi wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania nchini China katika Maadhimisho ya Miaka 50 ya Maonesho ya Kimataifa ya Biashara ya Dar es Salaam (Sabasaba), yanayoendelea katika Viwanja vya Mwalimu Julius Nyerere, Temeke jijini Dar es Salaam.
Katika ziara hiyo, Kamishna Jenerali Makakala alipokelewa na Balozi wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania nchini China, Dk. Suleiman Haji Suleiman ambaye pamoja na mambo mengine alimuelezea kuhusu shughuli mbalimbali zinazotekelezwa na Ubalozi katika kuimarisha uhusiano wa kidiplomasia na kiuchumi kati ya Tanzania na China.
Kamishna Jenerali Makakala alimpongeza kwa hatua hiyo ambayo ni mwendelezo wa uhusiano mzuri uliopo kati ya nchi hizo mbili lakini pia uhusiano wa kibiashara ambao unamuinua mtu mmoja mmoja na taifa kwa ujumla katika sekta ya biashara.
Kwa upande wake Balozi Dkt. Suleiman alieleza mchango wa Ubalozi katika kuvutia uwekezaji, kukuza biashara, utalii, elimu, uhamishaji wa teknolojia na fursa nyingine za maendeleo kupitia ushirikiano wa kimkakati kati ya Tanzania na China.
Banda la Ubalozi wa Tanzania nchini China linaendelea kuwa kitovu cha utoaji elimu na taarifa kuhusu fursa za uwekezaji na biashara, likiwahudumia wananchi, wafanyabiashara, wawekezaji, wanafunzi na wadau mbalimbali wanaotembelea Maonesho ya Miaka 50 ya Sabasaba.

