NA MWANDISHI WETU, KILIMANJARO
MAHAKAMA ya Wilaya ya Siha mkoani hapa imewahukumu kifungo cha nje cha miezi kumi na miwili Watumishi wawili wa Halmashauri ta Wilaya ya Siha Mohamed Bakari Mhasibu wa Mapato na Laurent Mgonja Mkusanya Ushuru.kwa makosa ya uhujumu uchumi (12) pamoja na kurejesha fedha walizofanya ubadhirifu kiasi cha Sh. 12,000,000/-
Hukumu hiyo ilitolewa Aprili 2,2026 ambapo Mshtakiwa wa kwanza Bakari ambaye alikuwa Mhasibu wa Mapato wa Halmashauri hiyo kwa kushirikiana na mshtakiwa wa pili Mgonja ambaye alikuwa Mkusanya Ushuru walifikishwa katika Mahakama ya Wilaya ya Siha Novemba 27, 2025 mbele ya Hakimu Elibahati Petro.
Washtakiwa hao wawili walikuwa wakikabiliwa na makosa matatu ambayo ni Matumizi Mabaya ya Madaraka chini ya kifungu cha 31 cha Sheria ya Kuzuia na Kupambana na Rushwa Na. 11/ 2007 ikisomwa pamoja na aya ya 21 ya jedwali la kwanza na vifungu vya 57(1) na 60(2) vya Sheria ya Uhujumu Uchumi sura ya 200 marejeo ya mwaka 2019
Kosa la pili ni Ufujaji na Ubadhirifu chini ya kifungu cha 28(1) cha Sheria ya Kuzuia na Kupambana na Rushwa Na. 11/ 2007 ikisomwa pamoja na aya ya 21 ya jedwali la kwanza na vifungu vya 57(1) na 60(2) vya Sheria ya Uhujumu Uchumi sura ya 200 marejeo ya mwaka 2019 .
Aidha kosa la tatu la washtakiwa hao wawili ni Kuisababishia Serikali hasara ya Sh.Milioni 12/-ambapo ni kinyume na Aya 10(1) ya jedwali la kwanza na kifungu 57 (1) na 60(2) vya Sheria ya Uhujumu Uchumi sura ya 200 marejeo ya mwaka 2019.
Fedha hizo Sh. 12,000,000/- zimetokana na ukusanyaji wa ushuru wa mazao katika eneo la Makiwaru ambapo wahusika walipaswa kuziweka katika akaunti ya Halmashauri ila hawakufanya hivyo na badala yake walizitumia kwa matumizi yao binafsi.
Shauri hilo lilikuwa likisimamiwa na Wakili wa Serikali kutoka Taasisi ya Kuzuia na Kupambana na Rushwa( TAKUKURU) Suzan Kimaro.

