NA JANETH JOVIN, DAR ES SALAAM
CHUO cha Mafunzo ya Ulinzi wa Amani Tanzania (TPTC) kwa kushirikiana na Umoja wa Mataifa (UN), kupitia taasisi ya Serikali ya Uswisi inayojulikana kama Geneva Centre for Security Sector Governance (DCAF), kimeanza mafunzo maalum ya ukufunzi yenye lengo la kubaini sababu na vikwazo vinavyowakwamisha wanajeshi wanawake kushiriki kikamilifu katika operesheni za ulinzi wa amani.
Akizungumza na Waandishi wa Habari jijini Dar es Salaam leo wakati wa ufunguzi wa mafunzo hayo, Mkufunzi Mkuu wa TPTC, Kanali Deogratius Mulishi, amesema mafunzo hayo ya siku tano yanayoanza Januari 26 hadi 30, 2026, yanalenga kufanya tathmini ya kina kuhusu changamoto zinazokwamisha ushiriki wa wanawake wanajeshi katika operesheni hizo muhimu.
Amesema washiriki wa mafunzo hayo ni Maofisa na askari kutoka Jeshi la Wananchi wa Tanzania (JWTZ), Ofisi ya Taifa ya Takwimu (NBS), Chuo Kikuu cha Dar es Salaam (UDSM), pamoja na maofisa kutoka Shirika la Umoja wa Mataifa linaloshughulikia masuala ya wanawake, UN Women.
“Mafunzo haya yamelenga kuongeza ushiriki wa wanawake wanajeshi katika operesheni za ulinzi wa amani. Imebainika kuwa idadi ya wanajeshi wanawake wanaoshiriki katika operesheni hizo ni ndogo, hivyo tunatafuta sababu, vikwazo na vipingamizi vinavyokwamisha kundi hili,” amesema Kanali Mulishi.
Ameongeza kuwa katika maeneo yenye migogoro na machafuko, waathirika wakubwa huwa ni wanawake na watoto, na mara nyingi askari wanawake huaminika zaidi katika ulinzi wa amani kutokana na uwezo wao wa kuwafanya wananchi wajisikie huru kutoa taarifa na kueleza changamoto zao.
“Wananchi waliokumbwa na machafuko huwa na uhuru zaidi wa kujieleza kwa askari wa kike kuliko wa kiume, hali inayoongeza ufanisi katika operesheni za ulinzi wa amani,” amesema.
Kanali Mulishi amesisitiza kuwa Umoja wa Mataifa umeweka viwango vinavyotaka nchi wanachama kufikia asilimia fulani ya ushiriki wa wanawake katika operesheni za kulinda amani. Ameeleza kuwa Tanzania imefikia asilimia 11 pekee, hali inayoonesha kuwa bado malengo hayajafikiwa, hivyo mafunzo hayo yatasaidia kubaini chanzo cha changamoto hizo.
Kwa upande wake, Mwakilishi wa UN Women, Katherine Giffold, amesema mradi huo wa mafunzo ni hatua muhimu katika safari ya muda mrefu ya ushirikiano kati ya UN Women, JWTZ, Wizara ya Ulinzi na Jeshi la Kujenga Taifa, NBS pamoja na UDSM.
Amesema mradi huo unaonesha dhamira ya pamoja ya wadau wote katika kuimarisha ushiriki wa wanawake katika masuala ya ulinzi na amani, huku akibainisha kuwa mafanikio yake yametokana na ushirikiano wa karibu kati ya taasisi mbalimbali.
“Mradi huu wa mafunzo unatumia mbinu za kimataifa kuchambua maeneo kumi ya utendaji, yakiwemo vigezo vya upelekwaji kazini, mifumo ya mafunzo, maendeleo ya taaluma na mazingira ya kazi, ili kubaini vikwazo vinavyowakwamisha wanawake katika vyombo vya ulinzi kushiriki operesheni za ulinzi wa amani,” amesema Giffold.
Aidha, ameipongeza Serikali ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania kwa kuzindua Mpango wa Kitaifa wa Wanawake, Amani na Usalama (WPS NAP) Agosti mwaka huu, akisema ni ushahidi wa dhamira ya serikali katika kuimarisha usawa wa kijinsia ndani ya sekta ya ulinzi na usalama.
Ameongeza kuwa taasisi za kitaalamu za NBS na UDSM ni washirika muhimu katika kuhakikisha ukusanyaji wa takwimu sahihi, uchambuzi wa kina na ufuataji wa viwango vya kimataifa katika utekelezaji wa mradi huo.
“Tanzania ni miongoni mwa nchi zinazotoa mchango mkubwa katika operesheni za kulinda amani za Umoja wa Mataifa. Hata hivyo, bado kuna haja ya kuweka mikakati madhubuti ya kuongeza ushiriki wa wanawake, hususan katika nafasi za uongozi na maamuzi,” amesema.
Kwa upande wake, Mwakilishi wa DCAF, Inka Lilsa, amesema wadau wa kimataifa wataendelea kuunga mkono vyombo vya ulinzi duniani kwa lengo la kujenga sekta ya usalama iliyo wazi, jumuishi na yenye uwajibikaji, huku mkazo ukiwekwa katika usawa wa kijinsia na usalama.
Amesema DCAF tayari imeisaidia zaidi ya nchi 20 duniani kufanya tathmini kama hiyo, na kwamba Tanzania itaungana na kundi la nchi zinazochangia wanajeshi na polisi katika operesheni za kulinda amani ambazo zimefanya tathmini ya kina ya kitaalamu.
Ameongeza kuwa licha ya ongezeko la idadi ya wanawake katika vyombo vya ulinzi, bado wanakabiliwa na changamoto nyingi katika utekelezaji wa majukumu yao, hali inayofanya tathmini hiyo kuwa ya umuhimu mkubwa.




