NA JANETH JOVIN, DAR ES SALAAM
WAZIRI wa Uchukuzi, Profesa Makame Mbarawa amewataka Wanafunzi wanaondelea na masomo, kusoma kwa bidii na kuepuka kuingia kwenye makundi yanayolenga kuvuruga amani ya nchi.
Mbarawa ameyasema hayo leo Disemba 19, 2025 katika Mahafali ya 41 ya Chuo cha Taifa cha Usafirishaji (NIT) yaliyofanyika chuoni hapo Mabibo, jijini Dar es Salaam ambapo zaidi ya wahitimu 4,000 wamehitimu masomo Yao katika ngazi mbalimbali
Amesema wanafunzi hao wanapaswa kuhakikisha wanayaepuka makundi hayo ambayo yanalenga kuvuruga amani ya nchi huku akiwataka wakumbuke kuwa bila amani na utulivu hakutakuwa na mazingira mazuri ya kusomea na kujifunzia.
”Nawapongeza wahitimu wote kwa jitihada mlizofanya kipindi chote cha masomo yane hadi kufikia hatua hii muhimu ya kutunukiwa vyeti, Ushauri wangu, endeleeni kuwa Wazalendo kwa nchi yenu, hakikisheni mnalinda amani ya nchi yetu, bila amani hata utaalamu huu mlioupata hautakuwa na maana kwa kuwa hakutakuwa na utulivu,” amesema
Mbarawa amewataka wanafunzi hao kuendelea kutafuta maarifa ya juu zaidi ili Taifa liwe na wataalam wa kutosha na wenye sifa stahiki katika sekta ya uchukuzi na usafirishaji.
Aidha amesema kwenye zama hizi ambapo kuna mabadiliko makubwa ya teknolojia, ubunifu ni muhimu sana kwa nchi katika kujenga uchumi imara na stamihilivu hivyo wanafunzi wanaoendelea na masomo amewataka wawe wabunifu ili wanapomaliza masomo yao wapate maarifa na ujuzi wa kutosha.
Amesema maarifa na ujuzi huo ambao wataupata wanafunzi hao pindi watakapomaliza masomo yao utawawezesha kujiajiri pasipo kutegemea sana kuajiriwa.
”Aidha kwa upande wa wafanyakazi wa Chuo, Wahitimu hawa ni matunda ya kazi yenu nzuri, kwa hiyo dumisheni na kulinda jitihada hizi katika kufikia malengo ya kuwapata wahitimu bora kwa mahitaji ya nchi yetu. Bila ushirikiano wenu, Mahafali haya yasingekuwepo. Rai yangu ni kwamba ongezeni bidii kwa kuendelea kujifunza zaidi hasa mabadiliko ya sayansi na teknolojia ili mafunzo mnayotoa yaendane na kasi ya mabadiliko ya Dunia ya sasa kwa maendeleo endelevu ya nchi,” amesema Mbarawa.
Kwa upande wake Mkuu wa Chuo hicho, Profesa Prosper Mgaya amesema tangu walipoanza rasmi kutoa mafunzo ya urubani mwezi Julai 2025 tayari wanafunzi 20 wamejiunga.
Mgaya amesema kati ya hao 10 wamemaliza mafunzo ya awali (ground school) na saba kati ya hao wamefikia hatua nya kuweza kurusha ndege angani bila ya usimamizi.
Pia amesema wameendelea kutoa mafunzo kwa taaluma nyingine katika usafiri wa anga ikiwemo wahudumu wa ndege na wataalam wa ukarabati wa ndege.
Ameeleza kuwa yote yamewezekana kutokana na serikali kuwekeza kutokana na serikali kuwekeza fedha takribani bilioni 57 katika kituo cha umahiri cha usafiri wa anga.
“Kwa muda mrefu taifa letu limekuwa likitegemea mafunzo ya wataalamu wa usafiri wa anga kutoka nje ya nchi, serikali imekuwa ikitumia fedha nyingi kusomesha wataalamu kutoka nje ya nchi kuanzishwa kwa mafunzo hayo kutasaidia kupunguza gharama hiyo iliyokuwa ikitumika”amesema.
Alitumia fursa hiyo kutoa wito kwa Watanzania wenye ndoto ya kuwa marubani kupata mafunzo hayo hapa nchini kwani yanatolewa na wataalam waliyobobea na wenye uzoefu.









