NA JANETH JOVIN, DAR ES SALAAM
SERIKALI imeeleza kuwa maboresho ya sera na sheria katika sekta ya viwanda na biashara yameanza kuzaa matunda, yakiongeza uzalishaji, ajira na ushindani wa bidhaa za Tanzania katika masoko ya ndani na nje ya nchi.
Akizungumza na Waandishi wa Habari jijini Dar es Salaam leo Desemba 18, 2025, Waziri wa Viwanda na Biashara, Judith Kapinga amesema mwelekeo wa sasa unaonesha sekta hiyo ikibadilika kutoka utegemezi wa bidhaa za nje kwenda uzalishaji wenye tija na thamani iliyoongezwa.
Kapinga amesema mchango wa sekta ya viwanda katika Pato la Taifa umefikia zaidi ya asilimia 7.3 huku biashara ikichangia asilimia 8.6 mwaka 2024, hali aliyoitaja kuwa ishara ya kuimarika kwa mazingira ya biashara na upanuzi wa masoko.
Aidha amebainisha kuwa mauzo ya nje ya bidhaa na huduma yameongezeka hadi kufikia zaidi ya dola za Marekani bilioni 16.8, yakichangiwa na bidhaa za viwandani na kilimo zilizoongezewa thamani.
Aidha Waziri huyo ameongeza kuwa uzalishaji mkubwa wa ndani umeifanya Tanzania kuanza kuuza nje bidhaa kama saruji, mabati na vioo, baada ya kuzidi mahitaji ya soko la ndani.
Akizungumza kuhusu uanzishwaji wa viwanda, Kapinga amesema idadi imeongezeka kwa kasi katika mikoa mbalimbali, akitaja Mkoa wa Pwani pekee kuwa na zaidi ya viwanda 2,000 vilivyoanzishwa ndani ya miaka minne.
Amesema mafanikio hayo yametokana na uhuishaji wa sera muhimu ikiwemo Sera ya Taifa ya Biashara, Sera ya Maendeleo Endelevu ya Viwanda na Sera ya Uendelezaji wa MSMEs ili kuendana na ushindani wa kimataifa.
Kapinga ameongeza kuwa serikali imehuisha pia sheria zaidi ya 13 na kanuni zake, hatua iliyopunguza gharama na muda wa kuanzisha biashara pamoja na kuimarisha udhibiti wa viwango na vipimo.
Ameongeza kuwa, maboresho hayo yamesababisha ongezeko la usajili wa makampuni, majina ya biashara, alama za biashara na leseni za viwanda kupitia mifumo ya kisasa ya kidijitali.
Amesema sekta binafsi imeendelea kuwa injini ya ukuaji wa uchumi, huku serikali ikijikita katika kuweka mazingira rafiki yanayozingatia ushiriki wa vijana, wanawake na watu wenye ulemavu.
Kuhusu masoko ya kimataifa, Kapinga amesema Tanzania inanufaika na fursa za soko huru barani Afrika pamoja na masoko ya Ulaya na Asia, jambo linaloongeza mauzo na mapato ya Taifa.
Amesisitiza kuwa juhudi hizo zinalenga kujenga uchumi imara na shindani, unaotegemea viwanda vyenye tija na biashara endelevu, huku maandalizi ya mkakati wa kitaifa wa mauzo ya nje yakikamilishwa.



