NA MWANDISHI WETU,DAR ES SALAAM
TAASISI ya Moyo Jakaya Kikwete (JKCI) itashirikiana na Shirika la Kimataifa linalojishughulisha na huduma za kibinadamu la Humaniti lililopo nchini Canada katika kutoa huduma za matibabu ya moyo kwa watoto waliopo Visiwani Zanzibar.
Ushirikiano huo utawasaidia watoto wenye matatizo ya moyo waliopo Visiwani humo kupata huduma za matibabu kwa wakati na hivyo kuokoa maisha yao.
Hayo yamesemwa leo Agosti 9, 2025 na Mkurugenzi Mtendaji wa Taasisi hiyo Dk. Peter Kisenge wakati akizungumza na viongozi wa Shiriki hilo walipotembelea taasisi hiyo kwaajili ya kuona huduma za matibabu ya moyo zinazotolewa.
“Ninaishukuru Serikali ya awamu ya sita inayoongozwa na Mhe. Dk. Samia Suluhu Hassan kwa uwekezaji mkubwa uliofanyika katika Taasisi yetu, kupitia uwekezaji huu hawa wenzetu kutoka nchini Canada wameona waje kushirikiana na sisi katika kutoa huduma ya matibabu ya moyo kwa watoto waliopo Zanzibar”, amesema Dk. Kisenge.
Dk.Kisenge ambaye pia ni Daktari bingwa wa magonjwa ya moyo amesema wataalamu wa JKCI wamekuwa wakienda Visiwani Zanzibar kutoa huduma za matibabu ya moyo kwa watoto, kuwepo kwa ushirikiano huo kutawezesha kupatikana kwa huduma hizo mara kwa mara.
Kwa upande wake Mkurugenzi Mtendaji wa Shirika la Kimataifa la Humaniti Firaaz Azeez amesema mwaka 2024 akiwa na wataalamu kutoka Shirika la Muntada Aid la nchini Uingereza kupitia mradi wa Little Heart walifika katika Taasisi ya Moyo Jakaya Kikwete (JKCI) kwaajili ya kufanya upasuaji wa moyo kwa watoto na kujionea vifaa tiba vya kisasa na wataalamu wabobezi waliopo JKCI.
“JKCI ni kituo cha umahiri cha matibabu ya moyo katika nchi za Afrika ya Mashariki na Kati tumeona tushirikiane nao katika kutoa huduma za matibabu kibingwa ya moyo kwa watoto waliopo Zanzibar na nchi zingine za Afrika”.
“Tutashirikiana nao kwa kufanya upimaji, kutoa mafunzo kwa wataalamu wa afya waliopo Zanzibar na kutoa uelewa kwa umma kuhusu magonjwa ya moyo kwa watoto ili watoto wenye matatizo haya waweze kutambuliwa mapema na kupata huduma kwa wakati”, amesema Azeez.