*YAELEZA MATARAJIO YAKE MIAKA IJAYO
NA MWANDISHI WETU, DAR ES SALAAM
MAMLAKA ya Maabara ya Mkemia( MMS) imeeleza utekezaji wa majukumu na mafanikio yake kwa kipindi cha miaka minne cha awamu ya sita chini ya Uongozi wa Rais Dk. Samia Suluhu Hassan.
Aidha Mamlaka hiyo imebainisha matarajio yake kwa miaka ijayo.
Hayo yameeleza leo Alhamisi Julai 10,2025 na Mkurugenzi wa Mamlaka hiyo Dk.Fidelice Mafumiko wakati akizungumza na Wahariri wa Vyombo vya Habari jijini Dar es Salaam.
Dk.Mafumiko amesema Mamlaka hiyo imejikita katika Huduma za uchunguzi wa Kimaabara, Utoaji wa Ushahidi wa Kitaalam, na Usimamizi na Udhibiti wa Kemikali za Viwandani na Majumbani, ujenzi wa miundombinu wezeshi ya ofisi na maabara, uimarishaji wa matumizi ya TEHAMA katika utoaji na mafunzo kwa wadau.
Sambamba na hilo pia Dk.Mafumiko ameeleza kuwa Mamlaka yake imejikira katika kuimarisha Huduma za Uchunguzi wa Kimaabara , Ufanisi katika utoaji wa huduma za Uchunguzi na wa kimaabara
“Katika kipindi cha miaka minne cha Serikali ya awamu ya sita inayoongozwa na Mhe. Dk. Samia Suluhu Hassan, Rais wa Jamhuri wa Muungano wa Tanzania, uchunguzi wa Kisayansi wa kimaabara kwa sampuli/vielelezo umeongezeka kutoka sampuli 155,817 Mwaka Fedha 2021/2022 hadi kufikia sampuli 188,362 kwa mwaka wa Fedha 2023/2024, sawa na ongezeko la asilimia 21.”amefafanua Dk.Mafumiko
Kadhalika katika kipindi cha mwaka wa Fedha huu wa 2024/2025, kuanzia mwezi Julai hadi Mei 2025, sampuli 175,561 zilifanyiwa uchunguzi sawa na asilimia 92 ya lengo la kuchunguza sampuli 191,420.
Ameeleza kuwa ongezeko la sampuli zinazochunguzwa na Mkemia Mkuu wa Serikali linatokana na kuongezeka kwa uelewa wa wananchi na wadau wa Mamlaka na ubora wa huduma za uchunguzi zitolewazo na Mamlaka.
Aidha, ongezeko hili ni kutokana na ushirikiano na taasisi za serikali za udhibiti kama vile Mamlaka ya Kudhibiti na Kupambana na Madawa ya Kulenya (DCEA), Jeshi la Polisi na Mamlaka ya Mapato (TRA), wadau wa afya zikiwemo hospitali, Usalama mahali pa kazi (OSHA), Baraza la Taifa la Hifadhi na Usimamizi wa Mazingira (NEMC) na wadau wengine wanaotumia huduma za Mamlaka ili kupata uhakika wa ubora wa bidhaa zao.
Amesema mchango wa utoaji wa matokeo ya Uchunguzi wa Sampuli kwa wakati
Uchunguzi wa kisayansi wa kimaabara umekuwa na mchango mkubwa katika kusaidia:Kuchangia katika mnyororo wa Haki Jinai na hivyo kuwezesha utoaji wa haki stahiki katika vyombo vya maamuzi kwa mhusika na kwa wakati.
“Masuala ya kijamii kama vile uhalali wa wazazi kwa watoto, utatuzi wa migororo inayohusu mirathi. Utambuzi wa miili ya Wahanga iliyoharibika vibaya kutokana na majanga mbalimbali ikiwemo ajali za majini, magari, kuangukiwa na majengo, moto, ndege, n.k. Matibabu kwa wagonjwa wanahohitaji huduma ya Kusafishwa figo: kwa kufanya uchunguzi wa sampuli za maji tiba yanayotumika kwa wagonjwa wanaohitaji kusafisha figo.
“Kupandikizwa figo kwa kufanya uchunguzi wa kimaabara kubainisha uhusiano uliopo kati ya mtoaji na mpokeaji wa figo kabla ya upandikizaji kufanyika. Utambuzi wa jinsi tata kwa kufanya uchunguzi wa kisayansi wa kimaabara na kutoa ushauri stahiki kwa Madaktari Bingwa kwa lengo la kutoa matibabu kwa wagonjwa wenye changamoto ya jinsi”
Kuhusu utambuzi wa sumu kabla ya kifo kutokea (Antemorterm) Dk.Mafumiko ameeleza kwa kubainisha kuwa sumu kwa wagonjwa wanaodhaniwa kuvuta, kunywa au kula chakula chenye sumu ili kupata tiba sahihi na kwa wakati. Utambuzi wa sumu baada ya kifo kutokea (Postmorterm): kwa kubanisha sumu iliyosababisha kifo kwa waathirika.
“Usalama na ubora wa bidhaa za viwandani na chakula, dawa (dawa za kisasa na dawa asili), mazingira, usalama mahala pa kazi kwa lengo la kuhakikisha afya ya jamii na mazingira inalindwa.
” Uwekezaji katika mitambo na vifaa vya kisasa vya uchunguzi
Serikali ya awamu ya sita inayoongozwa na Mhe. Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Dk.Samia Suluhu Hassan, imeiwezesha Mamlaka kununua mitambo na vifaa vya kisasa kwa ajili ya kuendelea kuboresha huduma za uchunguzi wa kisayansi wa kimaabara.
“Uwekezaji katika ununuzi wa mitambo ya uchunguzi wa kimaabara umeongezeka kwa asilimia 23.6, kutoka Shilingi Bilioni 13.6 kwa mwaka wa fedha 2017/2018 hadi 2021/2022 hadi kufikia thamani ya jumla ya Shilingi Bilioni 17.8 kwa mwaka wa Fedha 2024/2025 kwa kuongeza mitambo mikubwa Kumi na Sita (16) na midogo 274.
” Ununuzi wa mitambo hii umeendelea kuimarisha uchunguzi wa kimaabara na kuendelea kutoa huduma bora za uchunguzi wa Kisayansi wa kimaabara kwa wananchi kwa ufanisi zaidi.
” Utoaji wa Huduma za Kimaabara katika Viwango vya Kimataifa
Katika kipindi cha Serikali ya awamu ya sita inayoongozwa na Mhe. Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Dkt. Samia Suluhu Hassan Mamlaka imefanikiwa kuendelea kutoa huduma za Uchunguzi wa Kimaabara na matokeo yake kukubalika katika ngazi na Viwango vya kitaifa na Kimataifa. Kukubalika huko kwa matokeo ya uchunguzi kunatokana na Mamlaka kutekeleza mifumo miwili ya ubora na umahiri ya kimataifa, ambayo ni Ithibati ya Mifumo ya Usimamizi wa Ubora (ISO 9001:2015) ya uendeshaji wa shughuli za Mamlaka uliyohuishwa kwa mara nne mfululizo na mfumo wa Ithibati katika Umahiri wa uchunguzi wa kimaabara (ISO 17025:2027). “amejinasibu Dk.Mafumiko
Amesema katika kipindi cha miaka mine cha Serikali ya awamu ya sita pekee, Mamlaka imefanikiwa kupata ithibati katika Umahiri wa uchunguzi wa kimaabara (ISO 17025:2027) kwenye maabara zake sita (6) ambazo ni: Maabara ya Vinasaba vya Binadamu, Mikrobiologia, Sayansi Jinai Toksikologia, Mazingira, na Kanda ya Ziwa – Mwanza. ikiwemo maabara ya Chakula.
“Mafanikio haya ni makubwa na muhimu kwa kuwa, kunaifanya Mamlaka kukidhi matakwa ya Kisheria na mifumo ya Ubora katika ngazi ya kitaifa na kimataifa.
” Mamlaka inatekeleza jukumu la usimamizi na udhibiti wa kemikali kupitia utekelezaji wa Sheria ya Usimamizi na Udhibiti wa Kemikali za Viwandani na Majumbani, Sheria Na. 3. ya Mwaka 2003. Lengo la Sheria hii ni kulinda afya na mazingira dhidi ya madhara ya kemikali.
” Aidha, utekelezaji wa sheria hii unafanyika kupitia usajili wa wadau, ukaguzi wa maghala na maeneo ambapo kemikali zinatumika, ukaguzi wa maeneo ya mipaka ambapo mizigo yote ikiwemo kemikali zinapitia, na utoaji vibali vya kuingiza au kusafirisha kemikali ndani na nje ya nchi. ”
Pia Dk.Mafumiko amesema kwa upande wa Usajili wa Wadau ,Mamlaka imeendelea kufanya maboresho ya kuharakisha mchakato wa usajili wa kampuni zinazojihusisha na biashara ya kemikali. Katika kipindi cha miaka minne ya Serikali ya awamu ya sita kumekuwa na ukuaji wa biashara kwa wadau wanaojihusisha na biashara ya kemikali, ambapo wadau waliosajiliwa wameongezeka kutoka Wadau 2,125 Mwaka 2021 hadi Wadau 3835 kufikia Juni, 2025 sawa na ongezeko la asilimia 81 la wadau waliosajiliwa.
Kuhusu Ukaguzi wa Maghala Dk.Mafumiko amesema katika kuhakikisha kuwa kemikali zinatumika kwa usalama na kwa kufuata taratibu zote zinazohitajika ili kulinda afya ya binadamu na mazingira, na pia ili kuhakikisha kuwa kemikali zinazoingizwa nchini ni zile ambazo zinaruhusiwa kisheria kuingia nchini, Mamlaka hufanya ukaguzi wa mara kwa mara kwenye maghala yanayohifadhi kemikali na maeneo ya mipaka. Hivyo, katika kipindi cha miaka minne (4) cha Serikali ya awamu ya sita (6), Mamlaka imefanya ukaguzi wa maghala 8,521 ya kuhifadhia kemikali sawa na asilimia 119 ya lengo la kukagua maghala 7,160.
Fauka ya hayo Dk.Mafumiko ametanabaisha kuwa Mamlaka imeweza kudhibiti uingizaji na usafirishaji wa kemikali hatarishi na zile zinazodhibitiwa chini ya mikataba ya kimataifa ili kulinda afya ya binadamu, mazingira na usalama wa nchi kwa kutoa vibali vya kuingiza na kusafirisha kemikali hizo. Katika kipindi cha miaka minne (4) cha Serikali ya awamu ya sita (6), kumekuwa na ongezeko la vibali vya uingizaji wa kemikali kutoka vibali 40,270 kwa Mwaka wa Fedha 2020/2021 hadi vibali 67,200 kufikia kwa Mwaka wa Fedha 2024/2025 sawa na ongezeko la asilimia 40 ya vibali vilivyotolewa.
” Ongezeko hili la vibali limetokana na kuwepo kwa mazingira mazuri ya biashara na uwekezaji yaliyowekwa na Serikali ya awamu ya sita, wadau kuongeza uelewa wa Sheria, Kanuni na Miongozo mbalimbali inayosimamia shughuli za kemikali kwa kujengea uelewa wa matumizi sahihi ya mifumo ya TEHAMA inayotumika katika uombaji wa usajili na vibali.
“Kuwezesha Biashara ya Kemikali
Katika kipindi cha miaka minne (4) cha uongozi wa Serikali ya awamu ya sita, Mamlaka imeendelea kuchangia uboreshaji wa mazingira ya biashara ya kemikali nchini hasa zile za kimkakati zinazotumika kwenye uchimbaji na uchenjuaji wa madini hapa nchini na nchi jirani zikiwemo Zambia na Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo, ambapo:
Kemikali ya Ammonium Nitrate ambayo hutumika katika ulipuaji wa miamba wakati wa uchimbaji madini nchini na nchi za Zambia na Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo imeongezeka kutoka Tani 135,445 Mwaka Fedha 2021/2022 hadi Tani 461,777.42 kufikia Juni 2025 sawa na ongezeko la asilimia 241.”
Aidha, Mamlaka imewezesha zaidi ya asilimia 80 ya shehena ya Ammonium Nitrate iliyoingizwa nchini kupitia bandari ya Tanga na hivyo kuongeza thamani ya uwekezaji uliofanywa na Serikali ya awamu ya sita kwa kuongeza kina cha bandari hiyo. Kemikali ya Salfa ambayo hutumika katika mchakato wa uchimbaji na uchenjuaji wa madini ya shaba katika nchi za Zambia na Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo, ambayo uingizwaji wake hupitia bandari ya Dar es Salaam imeongezeka kutoka tani 396,982 Mwaka Fedha 2021/2022 hadi tani 1,867,104.72 kufikia Juni, 2025 sawa na ongezeko la asilimia 370.32.
“Kemikali ya Sodium Cyanide ambayo hutumika katika uchenjuaji wa madini ya dhahabu nchini na nchi za Zambia na Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo ambayo uingizwaji wake hupitia bandari ya Dar es Salaam imeongezeka kutoka Tani 41,461 Mwaka Fedha 2021/2022 na Tani 63,103.4 kufikia Juni, 2025 sawa na ongezeko la asilimia 52.20.
“Sababu za kuongezeka kwa uingizaji wa kemikali hizo kupitia Bandari ya Dar es Salaam na Tanga ni pamoja na maboresho ya miundombinu ya bandari na mahusiano mazuri kati ya nchi yetu na nchi Jirani yaliyowekwa na Serikali ya awamu ya sita chini ya uongozi wa Mhe. Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Dk Samia Suluhu Hassan.”
Vile vile kupitia mpango wa elimu kwa umma unaotekelezwa na Mamlaka kwa wadau wa biashara ya kemikali kumekuwa na ongezeko kubwa la wadau wanaotimiza matakwa ya Sheria ya usimamizi na udhibiti wa kemikali.
Aidha, Jengo hilo lina uwezo wa kuhudumia maabara tano (5) ambapo kwa sasa maabara tatu (3) zinafanya kazi baada ya ununuzi na usimikaji wa mitambo ya uchunguzi wa kimaabara ya kisasa kukamilika. Maabara hizo ni: maabara ya uchunguzi wa Vinasaba vya Binadamu, maabara ya uchunguzi wa Vinasaba vya Wanyama pori na maabara ya Sayansi Jinai Kemia na Toksikolojia.
Akitaja matarajio ya MMS,Dk.Mafumiko amesema Mamlaka hiyo itaendelea kuimarisha huduma za Uchunguzi wa Kisayansi wa kimaabara kwa sampuli na utoaji matokeo ya uchunguzi kwa wakati, ikiwemo: ununuzi wa Mitambo ya uchunguzi ili kukabiliana na changamoto ya kukua na mabadiliko ya Sayansi na Teknolojia.
Pia itaendelea kuimarisha Usimamizi na Udhibiti wa Kemikali za Viwandani na Majumbani kwa kuimarisha matumizi ya TEHAMA.Kuendelea kukamilisha miundombinu wezeshi kwa kujenga majengo yake ya Ofisi na Maabara katika Kanda kwa lengo la kusogeza huduma zitolewazo na Mamlaka karibu na wananchi.
“Kuendelea kuimarisha matumizi ya TEHAMA na kuifanya kuwa MAMLAKA JANJA katika: Usimamizi na Udhibiti wa Kemikali za Viwandani na Majumbani. kuboresha matumizi ya TEHAMA katika usimamizi na menejimenti ya taarifa za maabara ili kutoa matokeo kwa haraka na kwa usahihi zaidi.
“Kuboresha mifumo ya pamoja ya Serikali katika kuongeza ufanisi katika usimamizi wa Fedha, usimamizi wa rasilimali watu, na mifumo ya uratibu wa majukumu, mamlaka itapata fursa ya kupunguza makosa ya kibinadamu na kuongeza kasi ya utekelezaji wa majukumu na itasaidia kufikia malengo kwa haraka zaidi na kwa ufanisi zaidi.Kuwezesha upatikanaji na ubadilishanaji wa Taarifa kwa kuwezesha mifumo kusomana na kubadilishana taarifa na Taasisi zingine ikiwemo Haki Jinai.
“Kuendelea kuimarisha usalama wa data na taarifa ili kulinda taarifa za serikali na wadau.Kuendelea kutoa elimu kwa umma na wadau wa shughuli za Mamlaka ili kuviwezesha vyombo vya utoaji wa Haki, huduma ya afya na Mazingira.
Ikumbukwe kwamba MMS ni mojawapo ya taasisi za Serikali iliyoanzishwa chini ya Sheria ya Mamlaka ya Maabara ya Mkemia Mkuu wa Serikali, Sheria Na. 8 ya mwaka 2016. Kabla ya hapo, taasisi hii ilikuwa ni mojawapo ya Wakala na Serikali chini ya Sheria ya Wakala za Serikali Na. 30 ya Mwaka 1997 ikitokea kuwa mojawapo ya Idara ndani ya Wizara ya Afya.