* YAELEZA UMUHIMU WA WANANCHI KUJUA TAARIFA ZA UCHUMI NA FEDHA
*WAONESHA TAARIFA ZA UCHUMI TANGU NCHI IPATE UHURU
NA WAANDISHI WETU,DAR ES SALAAM
MFUMO wa Hazina ya Machapisho (Mof Repository) ni muhimu kwa wananchi katika kujua taarifa za uchumi na fedha kuanzia nchi ipate uhuru hadi sasa.
Hayo yamesemwa na Mkutubi Mwandamizi wa Kitengo cha Maktaba Wizara ya Fedha, Fredy Mpoma, alipokuwa akitoa elimu katika Banda la Wizara ya Fedha katika Maonesho ya 49 ya Kimataifa ya Biashara Dar es Salaam (Sabasaba) yanayoendelea katika Viwanja vya Sabasaba, Barabara ya Kilwa, jijini Dar es Salaam.
Mpoma alisema kuwa Mfumo huo ambao ni muhimu katika uhifadhi na upatikanaji wa taarifa za Wizara ya Fedha tangu uhuru unasaidia katika kuongeza ufahamu wa wapi uchumi umetoka na unakoelekea kupitia mtiririko wa taarifa mbalimbali.
Alibainisha machapisho yanayopatikana katika Mfumo huo kuwa ni Bajeti, Hali ya Uchumi, Deni la Taifa na Sheria ya fedha tangu uhuru.
Alisema machapisho hayo yanasaidia kuboresha utendaji na ufahamu wa masuala ya uchumi na kuwa na mipango yenye kuzingatia uhalisia kwa kutambua hatua kubwa iliyofikiwa na Serikali katika kuimarisha uchumi hadi sasa.
Alisema kuwa kizazi cha sasa hakina taarifa ya kutosha kuhusu mwenendo wa uchumi tangu uhuru, hivyo kupitia Mfumo huo ni wazi kwamba vijana wanaweza kuwa na hoja za msingi wanapo fuatilia maendeleo ya kiuchumi na hatua ambayo Tanzania imepiga ikilinganishwa na nchi nyingine hususani za Afrika.
Mpoma alisema kuwa hapo awali ilikuwa vigumu kwa taasisi za elimu ambazo zinajukumu la kufanya tafiti za kitaaluma kupata taarifa kwa usahihi na kwa wakati kuhusu hali ya uchumi na bajeti lakini kwa sasa kwa kutumia mfumo huo imerahisisha kupata taarifa katika kuboresha majukumu yao.
Aidha, ametoa rai kwa wananchi kutembelea Banda la Wizara ya Fedha katika maonesho hayo ili kupata taarifa za kina kuhusu mfumo huo ambao unaweza kupatikana kwa kutumia vifaa mbalimbali vya kielektroniki zikiwemo simu janja za mkononi.