NA JANETH JOVIN, DEMOKRASIA
RAIS Samia Suluhu Hassan amesema kuwa ukosefu wa maadili, rushwa na ubadhirifu ndani ya Jeshi la Polisi unadhohofisha mapambano dhidi ya uhalifu nchini.
Amesema maadili ndani ya Jeshi la Polisi ni suala nyeti na la msingi na kwamba kila mmoja kuanzia ngazi ya juu hadi askari mdogo anapaswa kuwa mfano wa kuigwa na askari mwenzake na jamii kwa ujumla.
Rais Samia ameyasema hayo leo Juni 9,2025 jijini Dar es Salaam katika Sherehe ya kufunga Kozi ya Maofisa na Wakaguzi Wasaidizi wa Jeshi la Polisi katika Chuo cha Taaluma ya Polisi.
Amesema ukosefu wa maadili,rushwa na ubadhirifu unadhohofisha sana mapambano dhidi ya uhalifu kwasababu askari akiwa sehemu ya hao hawatakuwa na nguvu ya kushughulikia mambo ya uhalifu ndani ya nchi.
Rais Samia amesisitiza kuwa endapo hawatakuwa na maadili ndani ya jeshi hilo hawatakuwa na nguvu ya kupambana na uhalifu na wahalifu.
”Hivyo kasimamieni imara mdhihirishe nidhamu,uadilifu na uzalendo wa kweli ili kupunguza malalamiko, kulinda taswira njema ya Jeshi letu la Polisi na kujenga imani kwa wananchi.
”Nendeni mkayazingatie na kutekeleza kwa vitendo yale yote mliyofundishwa kwa kipindi cha miezi tisa mlichokuwa hapa Chuoni,nyie ndio mnaoenda kuwa wakuu wa Intelejensia, baadhi yenu kwenda kufanya kazi kwa kushirikisha jamii kwenye kile Vitengo vya Polisi jamii, wengine Operation za kijamii,wengine Uchunguzi wa kisayansi ya jinai,Usalama barabarani ngazi za mikoa na wilaya,wapo watakao kuwa wakuu wa vituo vya Polisi, wapelelezi na wasaidizi wa wakuu wa Idara na vitengo mbalimbali jipangeni kikazi,” amesema