NA JANETH JOVIN, DAR ES SALAAM
RAIS wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Dk. Samia Suluhu Hassan amesema Tanzania na Namibia zimekubaliana kuongeza juhudi za kukuza ushirikiano wa kiuchumi kwa kutafuta njia madhubuti za kukuza biashara baina yao, ikiwa ni pamoja na kuwezesha uwepo wa miradi mikubwa ya uwekezaji kutoka pande zote mbili.
Akizungumza na Vyombo vya Habari Ikulu jijini Dar es Salaam mara baada ya mazungumzo rasmi na Rais wa Namibia Dk. Netumbo Nandi-Ndaitwah, Rais Dk. Samia alisisitiza umuhimu wa sekta binafsi katika kuchochea ajira kwa vijana na kupunguza umasikini.
Aidha, Marais hao walieleza dhamira ya kupanua ushirikiano katika maeneo ya elimu, utalii, mazingira, mifugo, uvuvi na nishati na kuweka msisitizo kwa sekta binafsi kuwekeza kwa kiwango kikubwa, tofauti na hali ilivyo sasa.
Rais Dk. Samia alibainisha kuwa biashara kati ya Tanzania na Namibia imeongezeka kutoka Sh. Bilioni 17 hadi bilioni 20 kati ya mwaka 2019 na 2023; hata hivyo, alisema kiwango hicho bado ni kidogo kulinganisha na fursa zilizopo na kuwataka wafanyabiashara wa nchi hizo mbili kuchangamkia fursa hizo.
Vilevile, Rais Dk. Samia aliikaribisha sekta binafsi ya Namibia kuja kuwekeza na kushirikiana na Tanzania katika sekta za uongezaji thamani wa mifugo, uvuvi na katika sekta ya utalii.
Katika utamaduni, Rais Dk. Samia alieleza kuwa Tanzania na Namibia zinatarajia kushirikiana katika seta ya elimu, ambapo Chuo Kikuu Huria cha Tanzania (OUT) kitashirikiana na Chuo cha Triumphant cha Namibia kufundisha lugha ya Kiswahili kama njia ya kukuza uhusiano, urafiki na mshikamano wa kijamii.
Rais Dk. Samia alihitimisha kwa kumhakikishia Rais Dk. Nandi-Ndaitwah kuwa Tanzania itaendelea kuwa mshirika wa karibu na mshauri wa kuaminika katika uongozi wake, akisema urafiki kati ya nchi hizo una mizizi ya kihistoria na utaendelea kuimarika kwa manufaa ya sasa na vizazi vijavyo.
Kwa upande wake, Rais Dk. Nandi-Ndaitwah alieleza kuwa hivi karibuni Serikali ya Namibia itatuma Mawaziri wa sekta za viwanda na biashara kuja Tanzania kwa lengo la kupata ujuzi na kujifunza programu za maendeleo na kuimarisha uhusiano wa kiuchumi.
Rais Dk. Nandi-Ndaitwah pia ameonesha furaha yake ya kualikwa kuzungumza katika Chuo Kikuu cha Dar es Salaam (UDSM) leo na ameeleza kuwa atatumia fursa hiyo kuwahamasisha wanafunzi kushiriki katika fursa za uongozi.
Viongozi hao wawili walikubaliana pia kuhusu umuhimu wa kuendeleza nishati mchanganyiko, zikiwemo nishati jadidifu na gesi, kwa lengo la kuhakikisha upatikanaji wa nishati ya uhakika kwa maendeleo ya viwanda na jamii katika ukanda nchi za Kusini mwa bara la Afrika.
Rais Dk.Nandi-Ndaitwah alipokelewa Ikulu jana na Rais Dk.Samia ikiwa ni sehemu ya ziara yake ya kiserikali ya siku mbili hapa nchini, ambapo anatarajia kuhitimisha ziara hiyo leo.