#Watuhumiwa 35 watiwa mbaroni akiwemo raia wa Uganda
NA MWANDISHI WETU, DAR ES SALAAM
MAMLAKA ya Kupambana na Kudhibiti Madawa ya Kulevya (DCEA) kwakushirikiana na vyombo vingine vya dola, wamefanikiwa kuzuia tani 14 za kemikali bashirifu zilizokuwa ziingizwe nchini kinyume cha sheria.
Akizungumza na Waandishi wa Habari jijini Dar es Salaam, Mkurugenzi Mtendaji wa DCEA Kamishna Jenerali Aretas Lyimo alisema hadi sasa operesheni hiyo pia imefanikiwa kuyashikilia magari saba, pikipiki tano na bajaji moja vilivyohusika kwenye uhalifu huo.
"DCEA imekamata kemikali hizo pamoja na watuhumiwa 35 akiwemo raia mmoja wa Uganda kupitia operesheni zilizofanyika katika katika mikoa ya Dar es Salaam, Shinyanga, Tabora, Tanga, Songwe, Mbeya na Arusha ambapo pia wamefanikiwa kukamata pakti 10 za pipi zenye uzito wa gramu 174.77 zilizotengenezwa kwa kutumia bangi kukamata kilogramu 4,568 za dawa mbalimbali za kulevya na kuteketeza ekari 178 za mashamba ya bangi,"alisema Kamishna Lyimo.
Alisema pia kwa kushirikiana na Bodi ya Kimataifa ya Kudhibiti Dawa za Kulevya Duniani (INCB) na mamlaka nyingine za udhibiti, DCEA ilibaini na kuzuia kilogramu 4,000 za kemikali aina ya 1-Boc-4-piperidone na kilogramu 10,000 za kemikali aina ya Acetic anhydride zilizokuwa ziingizwe nchini kutokea bara la Asia bila kuwa na vielelezo vinavyoonesha matumizi ya kemikali hizo.
"Endapo kemikali hizi zingeingizwa nchini na kuchepushwa zingeweza kutumika kutengeneza dawa za kulevya aina ya fentanyl na heroin". alisema
Alisema Mathalani, kilogramu 4,000 za kemikali aina ya 1-Boc-4-piperidone zinaweza kutengeneza kilogramu 8,000 za dawa za kulevya aina ya fentanyl.
Alisema pamoja na hayo amesema kuwa matumizi ya kiasi hicho cha dawa za fentanyl ambazo zingezalishwa zingeweza kusababisha vifo kwa watumiaji bilioni nne (4) ikizingatiwa kwamba, kilogramu moja (1) ya dawa hizo inaweza kusababisha vifo kwa watu 500,000 kutegemea na uzito, afya, na historia ya mtumiaji (miligramu mbili (2) inaweza kusababisha kifo kwa mtu mmoja).
Aidha, gari aina ya Mercedes Benz iliyokuwa ikisafirisha pipi hizo kutoka Afrika Kusini nayo ilikamatwa. Pia, mkoani humo zilikamatwa kilo 1,658 za bangi aina ya skanka na kilo 128.7 zilizokuwa zikiingizwa kutoka Malawi.
Kwa upande wa jijini Dar es Salaam, operesheni iliyoendeshwa katika kata ya Chanika ilikamata kilo 220.67 za bangi aina ya skanka zilizofichwa chooni, na kilo 11 nyingine zilipatikana katika eneo la ukaguzi wa mizigo bandarini kuelekea Zanzibar.
Alisema katika mikoa ya Arusha, Tanga, na Manyara zilikamatwa kilo 733.74 za methamphetamine, kilo 91.62 za heroin, kilo 692.84 za mirungi kutoka Kenya na kilo 115.05 za bangi, pamoja na kuteketeza ekari mbili za mashamba ya bangi. Mkoani Tabora wilaya ya Uyui na Nzega, kilo 845 za bangi zilipatikana na ekari 176 za mashamba ya bangi zilibomolewa. Shinyanga na Kahama walinaswa na kilo 98.35 za bangi.
Alieleza kuwa mafanikio haya yametokana na ushirikiano wa karibu na taasisi za ndani na nje ya nchi, na yamezuia athari kubwa kiafya, kijamii, kiuchumi na kimazingira ambazo zingeletwa na dawa hizo mitaani. Hii ni pamoja na kuokoa maisha ya mamilioni ya vijana ambao wangepotea kutokana na matumizi ya dawa hizo.
Naye Mkurugenzi Msaidizi Idara ya Uchunguzi kutoka Mamlaka ya Kudhibiti na Kupambana na Rushwa (PCCB),Thobias Ndalo alisema madawa ya kulenya ni tatizo kubwa magenge hayo na mengine ya uhalifu yanatumia kiasi kikubwa cha fedha katika uingizaji uagizaji was dawa hizi.
"Magenge haya yanafanikiwa kwa sababu ya nguvu ya fedha,hii inaonekana kunakuwa na viashiria vya rushwa sisi ni jukumu letu kuhakikisha watumishi wote wa umma waliohusika kusaidia magenge haya tutahakikisha tunawafuatilia.
"Dawa za kulevya zinadhoofisha vijana na kuchangia mmomonyoko wa maadili,pia zinatakatisha fedha kuingiza fedha chafu na kuhatarisha usalama wananchi wanakosa imani kwa serikali,"alisema Ndalo