NA MWANDISHI WETU,MOROGORO
WAKALA wa Usajili wa Biashara na Leseni (BRELA) imezindua Baraza la Wafanyakazi na kufanya kikao cha Kwanza cha Baraza hilo kwa mwaka wa Fedha 2024/2025 leo Februari06,2025 mkoani Morogoro.
Katika uzinduzi huo, Ofisa Mtendaji Mkuu na Mwenyekiti wa Baraza la Wafanyakazi wa Godfrey Nyaisa amewakumbusha Wajumbe wa Baraza kutekeleza majukumu yao ili kuleta tija na ufanisi mahali pa kazi.
Nyaisa alisema, “Baraza hili la Wafanyakazi wa BRELA lina jukumu la kipekee la kuchangia katika kuweka mazingira bora ya kazi yenye kuongeza tija, ushirikiano na maendeleo ya wafanyakazi, ambayo ndio uti wa mgongo wa mafanikio ya Taasisi. Tunapokutana hapa ni fursa ya kutafakari mafanikio, kujadili changamoto na kuweka mikakati ya pamoja kwa mustakabali wa Taasisi yetu.”
Ameendelea kueleza kuwa Baraza la Wafanyakazi lililozinduliwa litakuwa na jukumu la kuishauri Wakala kuhusu masuala mbalimbali yanayohusu maslahi ya Watumishi, utekelezaji wa mipango na makisio ya Mapato na matumizi ya Wakala, kupokea taarifa ya utekelezaji wa Wakala na kutoa ushauri, kudumisha ushirikiano kati ya watumishi na Wakala katika uendeshaji wa Wakala na kushauri kuhusu ustawi wa Wakala na Maendeleo ya Watumishi.
Pamoja na uzinduzi, Baraza hilo litafanya tathmini ya utekelezaji wa Bajeti ya Taasisi kwa kipindi cha nusu mwaka wa fedha 2024/2025 kwa kuangalia malengo yaliyopangwa, utekelezaji wa majukumu, changamoto zilizojitokeza wakati wa utekelezaji, mikakati ya kukabiliana na changamoto husika. Vile vile Baraza litajadili na kupitisha makadirio ya Bajeti ya Wakala kwa mwaka wa fedha 2025/2026.
Baraza pia lilifanya uchaguzi ambapo Peter Riwa, Ofisa Leseni Mwandamizi alichaguliwa kuwa Katibu na Gift Wazingwa, Ofisa Usajili alichaguliwa kuwa Katibu Msaidizi wa Baraza la Wafanyakazi. Ufunguzi na uchaguzi ulishuhudiwa na Brendan Maro, Dk. Hussein Mugyabuso kutoka Chama cha Wafanyakazi Tughe na Bi.Christina Matage kutoka Ofisi ya Waziri Mkuu – Kazi, Vijana, Ajira na Wenye Ulemavu.