*Azimio labeba malengo mbalimbali
*Latajwa kuwa suluhisho upatikanaji umeme wa uhakika barani Afrika
NA JANETH JOVIN, DAR ES SALAAM
JANUARI 27 na 28, 2025, Tanzania imeandika historia kubwa kwa kupata fursa ya kuwa wenyeji wa Mkutano wa Nishati wa Wakuu wa Nchi za Afrika (Mission 300) uliofanyika katika Ukumbi wa Kimataifa wa Mikutano wa Julius Nyerere.
Mkutano huo ulihudhuriwa na Wakuu wa Nchi na Serikali kutoka Burundi, Botswana, Congo, Comoros, Djibouti, Ethiopia, Gabon, Ghana, Guinea Bissau, Kenya, Lesotho, Liberia, Libya, Madagascar, Malawi, Mauritania, Nigeria, Sierra Leone, Somalia na Zambia.
Vile vile, ulihudhuriwa pia na Wawakilishi wa Wakuu wa Nchi na Serikali, Wakuu wa Mashirika ya Fedha ya Kimataifa, Mashirika ya Kimataifa, Sekta Binafsi na Asasi za Kiraia kwa lengo la kuongeza kasi ya usambazaji umeme barani Afrika ili kuwaunganisha watu milioni 300 na umeme katika kipindi cha miaka mitano ijayo.
Katika mkutano huo, Wakuu wa nchi Afrika wamepitisha na kusaini Azimio la Da es Salaam lenye malengo mbalimbali likiwemo la kutatua changamoto ya nishati na kutekeleza mpango wa matumizi ya nishati safi na ajenda ya ‘Mission 300’ inayolenga kupeleka umeme kwa waafrika milioni 300 inafikiwa ifikapo mwaka 2030.
Imeelezwa kuwa Azimio hilo ni mkataba wa pamoja wa wakuu hao wa nchi za Afrika ikiwemo Tanzania wa kuleta mageuzi makubwa katika sekta ya nishati kwa kuhakikisha nishati inakua toshelevu katika mataifa ya Afrika jambo ambalo litachochea uwekezaji na kuleta maendeleo.
Akisoma azmio hilo Januari 28,2025 jijini Dar es Salaam, Katibu wa Benki ya Maendeleo ya Afrika (AfDB), Profesa Vincent Nmehielle anasema wakuu hao wa nchi jana wamepokea azimio hilo la Dar es Salaam na kusaini huku wakipitisha vipengele ambavyo wameviahidi kupitia azimio hilo vitafanyiwa kazi.
Nmehielle anasema miongoni mwa vitu vilivyopo katika azmio hilo ni pamoja na marais na wakuu hao wa serikali kuwa wanatambua na kukubaliana ili kufikia lengo namba saba la maendeleo endelevu ya umoja wa mataifa kwaajili ya nishati kwa wote ya mwaka 2030 wanahitaji lengo la pamoja katika mnyororo mzima wa nishati.
Anasema pia wanahitaji mipango ya kuwa na mkataba wa pamoja wa nishati kwaajili ya kuhakikisha utekelezaji unafanyika hadi mwaka 2030 pamoja na kutambua ushirikiano wa kutafuta fedha na jitihada mbalimbali kwaajili ya agenda ya ‘mission 300’.
”Benki ya Maendeleo ya Afrika (AfDB) na Benki ya Dunia (WD) zimelenga kupitisha watu Milioni 250 kwaajili ya mradi huu lengo ni kuhakikisha umeme na nishati ya kupikia inawafikia watu wengi. AfDB imepongezwa kwa kutenga fedha na kufadhili miradi huu hadi mwaka 2030.
“Pia imepongezwa katika kuvutia zaidi mitaji ya sekta binafsi kwenye kuhakikisha wanapata fedha za kuleta mabadiliko katika mifumo ya nishati ya Afrika kwani wanatambua kuwa fedha hizo zinahitaji kutumika kikamilifu,”anasema.
Nmehielle anasema kipengele kingine kilichopo katika azimio hilo ni pamoja na kuimarisha na kuboresha miundombinu ya nishati na kufikisha umeme kwa waafrika kwa gharama ndogo, kuwekeza katika vyanzo mbalimbali vya umeme ikiwemo jua, maji pamoja na jotoardhi.
Pia anasema wakuu hao katika azimio hilo wamekubaliana kutekeleza ahadi zilizotolewa na AfDB ya fedha Dola Bilioni 2.6 kwaajili ya kusaidia miradi ya upatikanaji wa umeme barani Afrika na kuhakikisha wanatekeleza mpango wa maendeleo kwaajili ya malengo ya muda mrefu.
”Pia wamekubaliana kwa pamoja kutambua jitihada za Afrika kwaajili ya kupata umeme wa uhakika, utengamano wa kikanda pamoja na majukumu ya kimkakati ya Umoja wa Afrika (UN) kwaajili ya soko la pamoja la nishati na mpango kabambe kwaajili ya agenda ya nishati.
Anasema azimio hilo pia linatambua sekta binafsi inamchango mkubwa katika mnyororo mzima wa uzalishaji wa nishati kwaajili ya kufikia malengo ya nishati ikiwemo uzalishaji, usambazaji wa umeme na nishati safi ya kupikia na hivyo kutengeneza mazingira wezeshi kwa sekta binafsi wawekeze katika sekta ya nishati.
Aidha Nmehielle anasema kipengele kingine kilichopo katika azimio hilo ni kukubaliana na maono na dira ya kimataifa kwaajili ya kuhakikisha nishati ni sehemu muhimu ya kutokomeza umaskini, kuboresha afya, kuchochea ujenzi wa viwanda na kuimarisha maendeleo ya kiuchumi ya sekta mbalimbali Afrika.
Nmehielle anasisitiza kuwa Marais na Wakuu hao wa nchi wameahidi kufanya mambo mbalimbali kupitia azimio hilo ikiwemo kutekeleza malengo ya upatikanaji wa umeme na nishati safi ya kupikia, kuhakikisha upatikanaji wa mchanganyiko wa nishati kwaajili nishati safi.
Anasema pia kwa pamoja wamekubaliana kutekeleza hatua mbalimbali ikiwemo kuimarisha na kuboresha miundombinu ya uzalishaji wa umeme, usambazaji na kufikisha umeme kwa wateja kwa gharama ndogo na kuwa na mifumo ya gharama nafuu sio tu kwakuzingatia rasilimali za ndani ya nchi lakini pia kunufaika na vyanzo mbalimbali vya kimataifa.
Aliendelea kusema kipengele kingine ni kutoa vivutio kwa sekta binafsi kwa kutengeneza mazingira wezeshi kwa kuzingatia sera, mipango na miongozo rafiki kwaajili ya kupitia sekta binafsi katika kujikita kwenye chambuzi za faida na hasara kwenye kusaidia kuandaa sekta ya umeme Afrika.
”Kuhakikisha miundombinu ya umeme inafika kwa bei nafuu na endelevu kwa kupitia njia mbalimbali ikiwemo kurekebisha gharama mbalimbali za umeme, huduma za umeme zinapatikana kwa gharama ndogo na kwa muda muafaka na mapema zaidi na kuhakikisha kwamba kunakuwepo na taarifa za ukaguzi wa kifedha,” anasema na kuongeza
”Wamekubaliana kuchukua hatua madhubuti ya kuwezesha taasisi na kuzijengea uwezo wa utekelezaji kwa wakati, kuunganisha ushirikiano wa wadau pamoja na kuhakikisha uwepo wa usawa wa kijinsia ili umeme au nishati safi ipatikane kwa wanawake,” anasema
Anasema azimo hilo pia limehakikisha upatikanaji wa fursa na kutengeneza ujasiriamali wa sekta ya nishati, utengaji wa bajeti ndani ya nchi na kuunganisha na msaada wa kifedha kutoka kwa wadau wa kimataifa wa mashirika ya kibinadamu kutekeleza mipango huo.
Naye Rais wa Benki ya Maendeleo ya Afrika (AfDB) Dk. Akinumwi Adesina anasema ni muhimu Afrika kuweka nguvu za pamoja katika kutekeleza ajenda ya Mission 300 inayolenga kupeleka umeme kwa waafrika milioni 300 ifikapo mwaka 2030.
Hata hivyo anasisitiza kuwa Afrika inapaswa kuchukua mikopo ya riba nafuu na ya muda mrefu katika taasisi za fedha ili zisaidie kwenye kutekeleza mpango wa kuleta mapinduzi ya nishati barani Afrika.