NA JANETH JOVIN,DAR ES SALAAM
RAIS Dk.Samia Suluhu Hassan amewaongoza mamia ya waombolezaji kuaga mwili wa aliyekuwa Mbunge wa Kigamboni na Mkurugenzi Mteule wa Shirika la Afya Duniani (WHO) Marehemu Faustine Ndugulile huku akisisitiza kuwa Tanzania inaweka mikakati madhubuti ili kuhakikisha wanapatikana watanzania wengi zaidi wataoshindania nafasi mbalimbali za kimataifa.
Akizungumza katika Viwanja vya Karimjee jijini Dar es Salaam leo, Rais Samia amesema marehemu Ndugulile alipata nafasi ya kuiwakilisha Tanzania katika shirika la WHO, hivyo katika kuimarisha ushiriki wa Tanzania ni adhma ya serikali kuhakikisha inaweka kila aina ya nguvu ili watanzania wengi waweze kuwakilisha nchi katika nafasi za kimataifa.
“Ndugulile katika safari yake ya mwisho ameweka heshima kubwa kwa nchi kwa kupata nafasi WHO, tunasema Mungu amechukua amana yake lakini kwetu sisi ni kwenda mbele, tutarejea tena kwenye ushindani ya nafasi hiyo, tutatafuta mtanzania mwenye sifa zinazoweza kushindana na ulimwengu na tutaingia tena na tutaweza kuchukua ili kuweka heshima ya nchi yetu,” amesema Rais Samia na kuongeza
“Ndugu yetu Ndugulile alikuwa mwumini wa majumui wa Afrika na dunia kwa ujumla na kutokana na imani yake hiyo ndiyo ilimsukumu kwenda kugombea WHO na serikali ikamuunga mkono, lakini kama tunavyoaambiwa kwenye methali za kiswahili mwanadamu upati unachotaka bali unapata majaliwa, tulichokuwa tunataka ndugu yetu huyu aliwakilishe shirika na Tanzania lakini kwa Mungu ametupa jina lake leo tunamuaga ndugu yetu,” amesema
Naye Halima Mdee Mwakilishi wa Wabunge wachache bungeni, amesema marehemu Ndugulile alikuwa mtu asiyeyumbishwa na alisimama kidete katika kuwatetea wananchi wake na Taifa kwa ujumla bila kujali gharama.
Amesema Ndugulile alikuwa mtu ambaye alipambana kwa ajili ya kile alichokiamini na mtu aliyekuwa na msimamo ili kuinua na kulisaidia Taifa.
“Ndugulile alikuwa wa moto wala si baridi au uvuguvugu, kama jambo ni jeupe atasema ni jeupe na kama ni bluu basi atasema bluu. alipambana kwa kile alichokiamini, Taifa lilimuamini na kumchagua kuwa mwakilishi wa Tanzania WHO Kanda ya Afrika na akashinda,” amesema Mdee
Kwa upande wake mtoto wa marehemu Ndugulile, Martha Ndugulile amesema kuwa watamkumbuka daima baba yao kwani alikuwa shujaa na mtu bora katika familia kwa kuwalea kwenye malezi sahihi.
“Baba alikuwa anapenda muziki hasa wimbo wa msanii Prof, Jay wa ‘Hapo vipi’ daima tutamkumbuka kwa namna ambavyo alitulea katika malezi bora na sahihi, aliipenda familia yake kwa ujumla na ndio maana tunamwita shujaa,” amesema Martha