NA MWANDISHI WETU,DAR ES SALAAM
ASASI za Kiraia nchini kupitia Shirika la The Foundation for Civil Society (FCS), imeiomba Serikali iangazie katika kuhakikisha makundi maalumu yanawezeshwa kufikia miundombinu ya kidigitali ili waweze kushiriki katika michakato ya maendeleo na kujiimarisha kiuchumi.
Hayo yamesemwa na Meneja Programu wa FCS, Nasim Losai katika mkutano wa kitaifa wa watu wenye ulemavu, Madiwani na Wadau, uliofanyika Agosti 12, 2024 jijini Dar es salaam.
Losai amesema kuwa mkutano huo umejikita katika kuangazia ushiriki wa watu wenye ulemavu katika maendeleo, uchumi na kijamii, huku ukiangazia matumizi ya takwimu za sensa katika kuboresha mipango ya Halmashauri za Wilaya na ngazi za Kata.
Aidha, ameeleza kuwa Serikali imekuwa Sikivu katika kuhakikisha makundi maalum yanafikiwa na kuwezeshwa katika shughuli za kiuchumi na kujiongezea kipato, nakwamba FCS wamekuwa wakIisadia serikali katika kuunga mkono juhudi hizo kutokana na zoefu wao wa zaidi ya miaka 20 ya kufanya kazi na jamii.
“FCS tuna zaidi ya miak 20 tumekuwa tukisaidia serikali hasa katika shughuli za jamii na kutetea watu wenye ulemavu na michakato ya kiserikali, hasa kwenye majengo mengi miundombinu imebadilika na kazi kubwa imefanywa na FCS pamoja na makundi haya” amesema Losai.
Kwa upande wake Mshauri wa Kitaalamu masuala ya watu wenye ulemavu Tanzania Peter charlse, amesema mkutano huo umejumuisha watu mwenye ulemavu zaidi ya 600 kutoka ndani ya Jiji la Dar es salaam wakiwepo Madiwani 60 wa Viti Maalumu na wale wa kuteuliwa.
Amesema kuwa malengo ya mkutano huo ni kuwajengea uelewa watu wenye ulemavu katika masuala mbalimbali na kuangazia zaidi eneo la uchumi na kuona fursa zipi walemavu wameweza kushirikishwa na ambazo wanaziweza.
“Ushirikishwaji wa watu wenye ulemavu bado ni mdogo ndio maana tumewaalika madiwani ili kuangalia changamoto zilizopo na kuwajengea ili kuyaingiza katika mipango yao ya maendeleo kupitia Mabaraza yao ndani ya Halmashauri” amesema.
Naye Mwenyekiti wa Chama cha Walemavu Tanzania Hamadi Komboza, amesema changamoto kubwa kwa watu wenye ulemavu ni masuala ya ajira, huku akimuomba kamshina wa kazi na vyama vyenye ulemavu kufanya ukaguzi kwenye Mashirika na Taasisi ambazo zinapaswa kuajiri watu wenye ulemavu lakini bado hazijatekeleza na kwamba msukumo zaidi unahitajika.
Katibu Mkuu Shirikisho laVyama vya Watu Wenye Ulemavu Tanzania, Jonas Lubalo ameishukuru taasisi ya Ikupa Trust Fund kwa kuendelea kuchangia na kutoa huduma kwa watu wenye ulemavu katika maeneo mbalimbali hapa nchini.