NA MWANDISHI WETU,NKASI,RUKWA
WAKULIMA nchini wametakiwa kuzingatia kanuni sahihi za matumizi ya mbolea ili kulinda afya ya udongo na kuongeza uzalishaji wa mazao katika mashamba yao.
Wito huo umetolewa na Maofisa udhibiti ubora kutoka Mamlaka ya Udhibiti wa Mbolea Tanzania (TFRA) wakati wa mafunzo kwa wakulima pamoja na wanafunzi wa Shule ya Msingi Katawa yaliyofanyika katika Kijiji cha Kantawa, Kata ya Kipande, Wilaya ya Nkasi mkoani Rukwa.
Akizungumza katika mafunzo hayo,Ofisa kutoka TFRA, Henerico Renatus alisema matumizi yasiyo sahihi ya mbolea za chumvi chumvi yamekuwa miongoni mwa sababu zinazochangia kuharibika kwa udongo na kupungua kwa tija ya mazao kwa wakulima.
Alieleza kuwa baadhi ya wakulima hutumia mbolea nyingi bila kufuata ushauri wa kitaalamu, hali inayoweza kuathiri ubora wa udongo na uzalishaji wa mazao kwa muda mrefu.
“Matumizi yasiyo sahihi ya mbolea za chumvi chumvi yanaweza kuharibu udongo. Wakulima wanaweza kupata mavuno mazuri mwaka wa kwanza, lakini baadaye uzalishaji hupungua.
Wapo wanaotumia DAP, kisha kuongeza SA, CAN na hata kuchanganya aina nyingi za mbolea bila kufuata ushauri wa kitaalamu,” alisema.
Aliongeza kuwa matumizi ya mbolea kupita kiasi katika eneo moja kwa muda mrefu huathiri muundo wa udongo na kupunguza uwezo wake wa kuzalisha mazao kwa ufanisi.
“Mimea wakati mwingine huhitaji kiasi kidogo sana cha kirutubisho. Kwa mfano, gramu tano tu zinaweza kutosha kwa mmea mmoja, kiasi kinachoweza kulinganishwa na kifuniko cha chupa ya maji au soda.
Kiasi kikizidi, virutubisho vinaweza kupotea na hata kuharibu udongo,” alifafanua.
Katika mafunzo hayo, wakulima walipatiwa elimu kuhusu matumizi sahihi ya mbolea za ruzuku pamoja na umuhimu wa kupima afya ya udongo kabla ya kutumia mbolea, ili kuhakikisha matumizi sahihi ya virutubisho kulingana na mahitaji ya udongo.
Baada ya kupatiwa elimu hiyo, wakulima walishukuru serikali kwa kuendelea kutekeleza mpango wa ruzuku ya mbolea ambao umesaidia kupunguza gharama za pembejeo na kuongeza tija katika uzalishaji.
Mkulima wa zao la mahindi kutoka Kijiji cha Kantawa, Frenk Siwonike, alisema elimu waliyoipata imewasaidia kuelewa namna bora ya kutumia mbolea katika mashamba yao.
“Tunashukuru kupata elimu ya matumizi sahihi ya mbolea. Wakulima wengi hatukuwa na uelewa wa kutosha kuhusu namna bora ya kutumia mbolea. Tunaomba wataalam waendelee kututembelea mara kwa mara ili kutupatia elimu zaidi,” alisema.
Aliongeza kuwa mpango wa ruzuku ya mbolea umewawezesha wakulima wengi kuongeza ukubwa wa mashamba yao, tofauti na hapo awali ambapo gharama za pembejeo zilikuwa kubwa.
Aidha, wakulima hao waliwashukuru wadau wanaoshirikiana nao katika kuanzisha mashamba darasa na mashamba ya mfano, wakiwemo kampuni za mbegu za SeedCo na Zamseed, pamoja na makampuni ya mbolea na wadau wengine katika mnyororo wa pembejeo za kilimo.
Mafunzo hayo ni sehemu ya juhudi za TFRA katika kuwajengea uwezo wakulima kuhusu matumizi sahihi ya mbolea ili kuongeza tija ya mazao na kulinda rasilimali ya udongo kwa maendeleo endelevu ya kilimo nchini.






