NA MWANDISHI WETU, PRETORIA, AFRIKA KUSINI
MKUTANO wa siku mbili wa Baraza la Mawaziri la Jumuiya ya Maendeleo Kusini mwa Afrika (SADC) umehitimishwa jijini Pretoria, Afrika Kusini Machi 13, 2026.
Madhumuni ya mkutano huo yalikuwa ni kupanua kasi ya mtangamano wa kikanda kwa ajili ya kuharakisha maendeleo ili kutengeneza ajira, kuimarisha usalama wa chakula na upatikanaji wa nishati kwa wananchi.
Ujumbe wa Tanzania katika Mkutano huo uliongozwa na Naibu Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki Dk.Ngwaru Maghembe ambaye aliambatana na Naibu Waziri wa Fedha Laurent Luswetula.
Katika hotuba yake ya kufunga, Mwenyekiti wa Mkutano huo ambaye ni Waziri wa Uhusiano wa Kimataifa na Ushirikiano wa Afrika Kusini,Ronald Lamola alisisitiza umuhimu wa nchi wanachama kuwa na umoja na mshikamano ili kutekeleza kwa ukamilifu yale yaliyojadiliwa katika mkutano huo.
Katika majadiliano hayo, pamoja na mambo mengine, Mawaziri walisisitiza umuhimu wa kuharakisha utekelezaji wa miradi ya kikanda hasa ujenzi wa miundombinu ya usafirishaji, nishati safi na kuongeza kasi ya uwekezaji katika viwanda.
Aidha, Mawaziri walijadili utekelezaji wa bajeti ya SADC ya mwaka wa fedha 2025/2026 na kuandaa bajeti ya mwaka wa fedha 2026/2027.
Katika mkutano huo, nchi wanachama zilitahadharishwa kuhusu kuongezeka kwa taharuki katika siasa za ulimwengu na vita zinazoendelea Mashariki ya Kati, kuwa ni hatarishi kwa uchumi wa nchi za SADC na dunia kwa ujumla.
Mkutano huo ulitanguliwa na vikao vya Kamati ya Makatibu Wakuu na Kamati ya Fedha ambavyo vilikuwa na jukumu la kuandaa ajenda za mkutano na ripoti mbalimbali za utekelezaji.








