NA JANETH JOVIN, DAR ES SALAAM
UTEKELEZAJI wa mradi wa kutathmini mapungufu na vikwazo vinavyozuia ushiriki wa wanawake katika operesheni za kulinda amani umeanza rasmi leo, kufuatia Jeshi la Wananchi wa Tanzania (JWTZ) kusaini mkataba wa mwaka mmoja na taasisi tatu zitakazotekeleza mradi huo.
Taasisi hizo ni Shirika la Umoja wa Mataifa la UN Women Tanzania, Chuo Kikuu cha Dar es Salaam (UDSM) na Ofisi ya Taifa ya Takwimu (NBS).
Akizungumza baada ya utiaji saini, Mnadhimu Mkuu wa JWTZ, Luteni Jenerali Salum Haji Othmani, amesema tathmini hiyo itatoa mapendekezo yatakayosaidia kuimarisha sera, mifumo ya kiutendaji na mazingira wezeshi ili kuongeza nafasi za wanawake, hususan katika ngazi za uongozi ndani ya misheni za kulinda amani.
Amesisitiza kuwa mradi huo pia utachambua michakato ya uchaguzi na uteuzi ili kubaini iwapo kuna mazingira yanayokwamisha wanawake kushiriki kikamilifu katika operesheni hizo.
“Ushirikiano wa taasisi hizi unaonesha dhamira ya dhati ya Tanzania katika kutekeleza ajenda ya Wanawake, Amani na Usalama,” amesema Luteni Jenerali Othmani.
Ameongeza kuwa ripoti ya mwisho ya tathmini hiyo inatarajiwa kutolewa Septemba mwaka huu.
Kwa mujibu wa mkataba huo, mradi huo ujulikanao kama Measuring Opportunities for Women in Peace Operations (MOWIP) unafadhiliwa na Mfuko wa Elsie Initiative kupitia UN Women Tanzania.
Lengo lake ni kubaini vikwazo vya kimfumo, kitamaduni, kiutendaji na kiusalama vinavyozuia ajira, uendelevu wa ajira, uteuzi, pamoja na uongozi wa wanawake katika vyombo vya ulinzi na usalama.
Mradi huo unaendana na Mpango wa Kitaifa wa Wanawake, Amani na Usalama (2025–2029) na unatarajiwa kuimarisha mifumo ya kitaifa ya utafiti na takwimu, sambamba na kukuza ushirikiano kati ya sekta ya ulinzi, taaluma na taasisi za masuala ya kijinsia.
Kwa upande wake, Mkuu wa Chuo cha Mafunzo ya Ulinzi wa Amani Tanzania (TPTC), Brigedia Jenerali George Itang’are, amesema mkataba huo utawezesha utekelezaji wa mradi huo huku maeneo muhimu yatakayochunguzwa yakijumuisha sifa zinazotumika katika kuwachagua wanawake kushiriki operesheni za ulinzi wa amani na iwapo zinakuwa kikwazo kwao.
Amesema pia mradi utaangalia kama mifumo ya uteuzi inatoa fursa sawa kwa wanawake, pamoja na kuchunguza changamoto za kifamilia zinazoweza kuathiri ushiriki wao.
“Tutakusanya maoni kutoka kwa wanawake waliowahi kushiriki operesheni za ulinzi wa amani na jamii zinazowazunguka ili kubaini iwapo mrejesho wa kijamii unachochea au unazuia ushiriki wao,” amesema.
Aidha, watafiti wanatarajia kubaini mifano bora ya utekelezaji na kuandaa mapendekezo yatakayoongeza ushiriki wenye tija wa wanawake katika shughuli za ulinzi wa amani.
Mwakilishi Mkazi wa UN Women nchini, Katherine Gifford, ameipongeza Tanzania kwa kuanza rasmi mradi huo akisema ni hatua muhimu katika kuimarisha ushirikishwaji wa kijinsia katika juhudi za kulinda amani na usalama kimataifa.
Amesema mradi huo ni mfano wa ubia uliojengwa juu ya misingi ya heshima, utaalamu na dhamira ya pamoja, huku akitaja mchango wa muda mrefu wa Tanzania katika operesheni za kulinda amani za Umoja wa Mataifa na Umoja wa Afrika pamoja na juhudi za kuongeza ushiriki wa wanawake katika misheni hizo.
Mtakwimu Mkuu wa Serikali, Dk. Amina Msengwa, amesema ushirikiano huo ni hatua muhimu kwa utawala shirikishi na mipango ya taifa, akibainisha kuwa upanuzi wa ukusanyaji wa takwimu utaimarisha maamuzi na kutoa msingi wa kupima maendeleo ya baadaye.
Naye Naibu Makamu Mkuu wa Chuo Kikuu cha Dar es Salaam (Taaluma),Profesa Rose Upor, amesema ushirikiano huo unatumia ipasavyo rasilimali za kitaaluma, miundombinu na teknolojia ya kitaifa ili kuboresha mbinu za utafiti na kuongeza mwonekano wake,huku akisisitiza kuwa ni muungano wa muda mrefu unaoendana na vipaumbele vya taifa na viwango vya juu vya maadili ya utafiti.

















