NA JANETH JOVIN, DAR ES SALAAM
WITO umetolewa kwa wanafunzi wanaokwenda kusoma nje ya nchi kutumia fursa wanazopewa kwa nidhamu, bidii na kuzingatia maadili, ili wakirejea walete mchango chanya kwa maendeleo ya Taifa.
Wito huo umetolewa leo Januari 30,2026 katika hafla ya kuwaaga wanafunzi 16 kati ya 50 wa programu ya Samia Scholarship Extended DS/AI, iliyoandaliwa na Wizara ya Elimu, Sayansi na Teknolojia,na Waziri wa Elimu, Sayansi na Teknolojia, Profesa Adolf Mkenda.
Profesa Mkenda amewasisitiza wanafunzi hao kuwa mabalozi wa nchi na kuhakikisha wanajifunza kwa bidii, wanaheshimu sheria za nchi wanazoenda
“Mkatumie maarifa mtakayopata kuleta suluhisho la changamoto za maendeleo hapa nchini ili kupata mabadiliko chanya kulingana na dira ya maendeleo ya 2050”,Amesema Prof. Mkenda.
Profesa Mkenda amesema programu ya Samia Scholarship ni matokeo ya dhamira ya Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Dkt. Samia Suluhu Hassan, ya kuwekeza kwenye sayansi, teknolojia na rasilimali watu, hususan kwa vijana, ili kuandaa kizazi chenye uwezo wa kushindana kimataifa.
Kwa upande wake Katibu Mkuu wa Wizara ya Elimu, Profesa Nombo, amesema serikali itaendelea kuwekeza kwenye programu za kimkakati kama Samia Scholarship Extended DS/AI, kwa kuwa zinasaidia kujenga msingi wa maendeleo ya muda mrefu kupitia sayansi na teknolojia.
Profesa Nombo amewataka wanafunzi kuzingatia kuwa wao ni mfano kwa vijana wengine waliopo mashuleni, na kwamba nafasi hizo zinapatikana kwa misingi ya ushindani wa kitaaluma (merit-based), hivyo wanafunzi wajitahidi katika masomo hasa ya sayansi na TEHAMA.
Amesema uwepo wa taasisi kama Nelson Mandela Institute of Science and Technology umechangia kwa kiasi kikubwa kuwajengea wanafunzi ujuzi wa kitaaluma na maisha, ikiwemo financial management na stadi za karne ya 21.
Mmoja wa wanufaika wa programu hiyo, Malaika Florence, amesema mafunzo ya awali waliyopata kupitia boot camp yamewajengea uwezo mkubwa katika masuala ya usimamizi wa fedha, matumizi ya teknolojia na kujiamini katika mazingira ya kimataifa.
Amesema awali wengi wao walikuwa hawana ujuzi wa msingi wa matumizi ya kompyuta, lakini sasa wamejifunza stadi za kisasa ikiwemo uandishi wa codes, matumizi ya lugha mbalimbali za programu kama Python na Java, pamoja na mbinu za kujifunza kwa kujitegemea.
Malaika ameongeza kuwa wamejifunza pia sera za uhamiaji, namna ya kuishi na watu wa tamaduni tofauti, pamoja na umuhimu wa kujenga mitandao ya kitaaluma, akisisitiza kuwa “maisha ni watu” na mafanikio yanahitaji ushirikiano.
Naye Aswile Simon, ambaye amepata nafasi ya kwenda kusoma katika Chuo Kikuu cha Johannesburg nchini Afrika Kusini, amemshukuru Rais Samia kwa kuanzisha programu hiyo, akisema pasipo uongozi wake vijana wengi wasingeweza kupata fursa adimu kama hiyo.
Aswile amesema wanafunzi wanatambua imani kubwa waliyopewa na Taifa, hivyo wana wajibu wa kusoma kwa bidii na kurejea nchini wakiwa na maarifa yatakayosaidia kuendeleza sekta ya teknolojia, uchumi wa kidijitali na ubunifu.
Sambamba na hayo wanafunzi wote nchini wameaswa kuchangamkia masomo ya sayansi na teknolojia, huku serikali ikiombwa kuendelea kupanua wigo wa programu za ufadhili wa masomo ili kuzalisha wataalamu wengi watakaoliwezesha Taifa kufikia malengo ya maendeleo ya muda mrefu.






