NA JANETH JOVIN,DAR ES SALAAM
KATIKA kipindi cha miaka mitano ya uongozi wa Rais Dk. Samia Suluhu Hassan, Serikali imefanya mageuzi makubwa yaliyowanufaisha moja kwa moja vijana wa Kitanzania, hususan katika sekta za elimu, ujuzi, ajira na uwezeshaji wa kiuchumi, hatua zilizofungua fursa mpya za maendeleo kwa kizazi cha sasa na kijacho.
Hayo yamebainishwa jijini Dar es Salaam leo Januari 27, 2026 na Mratibu wa Taasisi ya Together for Samia, Gulatone Masiga wakati wa maadhimisho ya kumbukizi ya kuzaliwa kwa Rais Samia yaliyoandaliwa na taasisi hiyo.
Masiga amesema miongoni mwa mafanikio makubwa ya Rais Samia ni ujenzi wa vyuo vya ufundi na ujuzi katika zaidi ya wilaya 62 nchini, jambo ambalo limefungua fursa kwa maelfu ya vijana kupata maarifa ya vitendo yanayowawezesha kujiajiri na kushindana katika soko la ajira.
“Rais Samia amewekeza kwa vitendo kwenye kizazi cha sasa na kijacho. Vyuo hivi vya ufundi vimekuwa chachu ya kuwapa vijana ujuzi unaohitajika katika dunia ya sasa,” amesema Masiga.
Ameongeza kuwa Rais Samia amefanya mageuzi makubwa katika sekta ya elimu kwa kuja na mtaala mpya unaolenga kuhakikisha wanafunzi wanaomaliza elimu ya msingi na sekondari wanakuwa na maarifa na stadi zinazowawezesha kujiajiri na kuanzisha shughuli za kiuchumi.
Aidha, Masiga amesema Rais Samia ameendelea kuwekeza katika sekta ya nishati, hatua iliyosaidia kuchochea maendeleo ya viwanda, biashara na uwekezaji unaowanufaisha vijana moja kwa moja.
Kwa upande wake, Mwanzilishi na Mkurugenzi wa Taasisi ya Vijana Innovations, Dorcas Mshiu, amesema ameungana na Watanzania kuadhimisha siku ya kumbukizi ya kuzaliwa kwa Rais Samia kwa kutambua mchango wake mkubwa katika kufungua fursa za kiuchumi kwa vijana.
Mshiu amesema kupitia Wizara ya Viwanda na Biashara, vijana wengi wameanza kusajili biashara zao rasmi, hali inayoonesha kuwa mazingira ya biashara nchini yameendelea kufunguka na mipaka imekuwa rafiki zaidi kwa wawekezaji wa ndani na nje.
“Hii ni ishara kwamba nchi imefunguka kiuchumi na vijana wamepewa nafasi ya kuwa sehemu ya maendeleo ya Taifa,” amesema Mshiu.
Ameongeza kuwa Rais Samia ametengeneza mkakati maalum wa mikopo yenye riba ya asilimia 4 kwa vijana, ambao umekuwa msaada mkubwa kwa vijana waliyojikita katika kujiajiri na ujasiriamali.
“Mikopo hii imewawezesha vijana wengi kufungua biashara, kuongeza kipato na kujikwamua kimaisha,” amesema.
Naye Nathaniel Maseke, mshiriki wa maadhimisho ya kumbukizi ya kuzaliwa kwa Rais Samia, amesema anaendelea kumuombea Rais ili aendelee kuwaongoza Watanzania, hususan vijana, katika misingi ya umoja, mshikamano na bidii katika kazi.
“Tunaamini kupitia uongozi wake, vijana wataendelea kuhamasishwa kushikamana, kufanya kazi kwa bidii na kushiriki kikamilifu katika ujenzi wa Taifa,” amesema Maseke.
Maadhimisho hayo yamekuwa fursa kwa vijana na viongozi mbalimbali kutafakari safari ya uongozi wa Rais Samia na mchango wake katika kulijenga Taifa lenye fursa, mshikamano na matumaini kwa kizazi cha sasa na kijacho.


