NA MWANDISHI WETU, SHINYANGA
OFISI ya Madini ya Mkoa wa Shinyanga imeandika historia mpya ya mafanikio baada ya kuvuka kwa kishindo lengo la Makusanyo ya Maduhuli kwa kipindi cha Julai hadi Desemba 2025, baada ya kufanikiwa kukusanya Sh. Bilioni 22.66 kati ya Sh. Bilioni 32 walizopangawia kukusanya katika Mwaka wa Fedha wa 2025/2026 na ikiwa ni sawa na ufanisi ya asilimia 71 kwa lengo la mwaka mzima. Hatua inayodhihirisha nguvu ya mshikamano na uwajibikaji kazini.
Hatua hiyo ilibainishwa Desemba 30, 2025 na Ofisa Madini Mkazi wa Mkoa wa Shinyanga Mhandisi Noel Odera, wakati akitoa taarifa ya Mkoa huo wa Kimadini mbele ya Naibu Katibu Mkuu Wizara ya Madini Msafiri Mbibo alipotembelea Ofisi ya RMO Shinyanga kukagua shughuli za madini mkoani humo.
Mhandisi Odera alisema kuwa, Mkoa wa Kimadini wa Shinyanga umepangiwa kukusanya jumla ya Shilingi Bilioni 32 katika mwaka mzima wa fedha 2025/2026 na kwamba, hadi kufikia tarehe 24 Desemba 2025, Ofisi imefanikiwa kukusanya Shilingi 22,667,691,491.01 sawa na asilimia 142 ya lengo la kipindi cha Julai hadi Desemba 2025, na kufikia asilimia 71 ya lengo la mwaka mzima ndani ya miezi sita pekee.
Kwa upande wake, Naibu Katibu Mkuu wa Wizara ya Madini, Msafiri Mbibo, alipongeza kwa dhati Uongozi na Watumishi wa Ofisi ya Madini Mkoa wa Shinyanga kwa mafanikio hayo makubwa, na kusisitiza kuwa mafanikio hayo yametokana na mshikamano, nidhamu ya kazi na ushirikiano mzuri miongoni mwa watumishi.
“Team work yenu imeleta tija halisi. Msiivunje timu na huu umoja, ari hii iendelezwe na kuimarishwa zaidi kwa kuwa ndiyo msingi wa mafanikio haya ya makusanyo mazuri, na Serikali inajivunia sana kuwa na watumishi wenye kiwango cha ufanisi kama hiki” alisisitiza Mbibo.
Nao Watumishi wa Ofisi ya Madini Mkoa wa Shinyanga walieleza kuongezewa ari na morali, huku wakiahidi kuendeleza kasi ya ukusanyaji maduhuli kwa kuzingatia misingi ya uwajibikaji, uadilifu na utoaji wa huduma bora kwa wadau wa sekta ya madini.
Mafanikio hayo yanaonesha kwa vitendo kuwa mshikamano kazini, usimamizi madhubuti na uwazi katika utekelezaji wa majukumu vinaweza kuleta matokeo chanya kwa Taifa, hususan katika kuimarisha mapato ya Serikali na kuchangia maendeleo endelevu ya Sekta ya Madini nchini.






