NA JANETH JOVIN, DAR ES SALAAM
MKURUGENZI wa Utawala wa Kampuni ya Superdoll, Jamal Bayser, amekipongeza Chuo cha Usafirishaji cha Taifa (NIT) kwa kufanya vizuri katika uzalishaji wa wahitimu wenye ujuzi na ubora unaokidhi mahitaji ya soko la ajira, hususan wale wanaojiunga na makampuni mbalimbali ya usafirishaji nchini.
Bayser alitoa pongezi hizo jana jijini Dar es Salaam wakati wa Kongamano la 12 la Wahitimu wa NIT, lililowakutanisha wadau mbalimbali wa sekta ya usafirishaji, ikiwa ni sehemu ya maadhimisho ya miaka 50 ya kuanzishwa kwa chuo hicho.
Amesema kama mdau wa sekta hiyo, anaona tofauti kubwa ya ubora wa wahitimu wa sasa ukilinganishwa na miaka ya nyuma.
“Tunaipongeza NIT kwa kazi kubwa wanayoifanya katika kuimarisha sekta ya usafirishaji. Chuo kinazalisha wahitimu wengi katika kada mbalimbali, na sisi tuliopo kwenye sekta hii tunashuhudia kwa vitendo ubora wa wanafunzi wanaohitimu kutoka hapa,” amesema Bayser.
Ameongeza kuwa mabadiliko yaliyofanywa na chuo hicho yanaonekana wazi na yana matumaini makubwa kwa wadau wa sekta ya usafirishaji, akisema kuwa kiwango cha wahitimu wa sasa kimepanda kwa kiasi kikubwa ikilinganishwa na miaka iliyopita.
Akitoa ushauri,Bayser amesisitiza umuhimu wa kuimarisha zaidi eneo la teknolojia, akieleza kuwa ni mhimili muhimu katika kuibua bunifu na ugunduzi utakaosaidia kuleta matokeo chanya katika sekta ya usafirishaji.
Ameeleza kuwa kadri siku zinavyokwenda, kazi kubwa inaendelea kufanyika chuoni hapo, na wahitimu wanaotoka NIT kwa sasa wana viwango vya juu vya utendaji katika maeneo mbalimbali ya kazi.
Kwa upande wake, Mkuu wa Chuo cha NIT, Dk. Prosper Mgaya, amesema kufanyika kwa kongamano hilo kunatokana na maelekezo ya Serikali yanayotaka vyuo kuwa na mahusiano ya karibu na sekta wanazozihudumia ili mafunzo yatolewayo yaendane na mahitaji halisi ya soko la ajira.
Dk. Mgaya amesema kupitia kongamano hilo, chuo kimewasilisha mada na maonesho ya bunifu mbalimbali zilizobuniwa na wanafunzi, kwa lengo la kuibua na kuendeleza vipaji vinavyoweza kutoa suluhisho kwa changamoto zinazowakabili Watanzania.
“Kupitia kongamano hili, tumeona bunifu nyingi zenye tija ambazo zimebuniwa na wanafunzi wetu. Kila mwaka chuo huangalia bunifu zinazolenga kutatua matatizo ya jamii, kisha kuzifanyia maboresho kwa usimamizi wa walimu wetu,” amesema Dk. Mgaya.
Ameongeza kuwa jukumu kubwa la chuo ni kuhakikisha linazalisha wahitimu mahiri, hususan madereva na wataalamu wa usafirishaji barabarani, kwa kutoa mafunzo yenye ubora na yanayoendana na mazingira halisi ya kazi.




