FLORAH AMON,DAR ES SALAAM
KATIKA kuunga mkono jitihada za Serikali kuboresha elimu na kuongeza taarifa jumuishi za kifedha kwa wananchi, Benki ya Azania imezindua huduma mbili mpya—Boom Advance na Salary Advance—zilizolenga kupunguza changamoto za kifedha kwa wanafunzi na wafanyakazi.
Ofisa Mwandamizi wa Idara ya Masoko wa benki hiyo, Elizabeth Nyattega, ameeleza kuwa huduma ya Boom Advance imetengenezwa mahsusi kwa wanafunzi wa elimu ya juu wanaopokea mikopo ya Bodi ya Mikopo ya Elimu ya Juu (HESLB).
Amesema huduma hiyo inawawezesha wanavyuo kupata mkopo wa muda wenye masharti nafuu bila kusubiri fedha za HESLB kuingia kwenye akaunti, hivyo kuwasaidia kujikimu wakati wakisubiri malipo rasmi.
Kwa upande wa wafanyakazi, Nyattega amesema huduma ya Salary Advance inawasaidia kupata sehemu ya mshahara kabla ya tarehe ya kawaida ya malipo ili kutatua mahitaji ya haraka ya kifedha.
“Mkopo hulipwa mara tu mshahara unapowasili, kwa riba nafuu ya asilimia tano, na mteja anaweza kukopa hadi nusu ya mshahara wake,” ameeleza, akiongeza kuwa mteja pia anaruhusiwa kukopa hadi asilimia 50 ya Boom au mshahara.
Huduma zote, amesema, zinapatikana kirahisi kupitia simu kwa kubofya *150*75#, pamoja na Azania Bank Mobile App na Internet Banking, jambo linalolenga kuimarisha upatikanaji wa huduma kidigitali.
Nyattega ameongeza kuwa maboresho yanayoendelea kwenye mifumo ya kidigitali yameiwezesha Benki ya Azania kutunukiwa Tuzo ya Ubora Kidigitali Afrika Mashariki 2025 katika Africa Bank 4.0 Award 2025, iliyotolewa na taasisi ya kimataifa ya BII Finance.




