NA JANETH JOVIN,DAR ES SALAAM
RAIS wa Tanzania, Dk.Samia Suluhu Hassan ametangaza Baraza la Mawaziri huku akiwafyeka baadhi ya Mawaziri saba waliokuwamo kwenye baraza lililopita.
Walioachwa na wizara zao walizoziongoza kwenye baraza lililopita ni aliyekuwa Naibu Waziri Mkuu na Waziri wa Nishati, Dk. Doto Biteko, Hussein Bashe (Kilimo), Innocent Bashungwa (Mambo ya Ndani).
Wengine waliotemwa ni Jenista Mhagama (Afya), Dk Seleman Jafo (Viwanda na Biashara), Dk Pindi Chana (Maliasili na Utalii) na Dk Damas Ndumbaro wa Katiba na Sheria.
Rais Samia ametangaza Baraza lake jipya la Mawaziri leo Novemba 17,2025 Ikulu ya Chamwino jijini Dodoma.
Hata hivyo Mawaziri wapya waliotangazwa ni Balozi Dk. Bashiru Ally ambaye ameteuliwa kuwa Waziri wa Mifugo na Uvuvi huku Naibu wake akiwa Ng’wasi Kamani.
Pia Rais Dk. Samia Suluhu Hassan amemteua Mbunge wa Jimbo la Rufiji, Mohamed Mchengerwa kuwa Waziri wa Afya na Naibu Waziri katika Wizara hiyo akiwa ni Dk. Florance Samizi.
Mawaziri wengine ni Adolf Mkenda ambaye ameteuliwa kuwa Waziri wa Elimu, Sayansi na Teknolojia huku Naibu wake akiwa Wanu Hafidh Amir.
Pia Balozi Khamis Omar ateuliwa kuwa Waziri wa Fedha huku Manaibu katika Wizara hiyo ni Laurent Luswetula na Mshamu Munde.
Wizara ya Ofisi ya Rais Menejimenti ya Utumishi wa Umma na Utawala Bora Waziri ni Ridhiwani Kikwete Naibu Waziri ni Regina Ndege huku Wizara ya Mipango na Uwekezaji Waziri ni Kitila Mkumbo na Naibu wake akiwa Pius Chaya.
Hata hivyo Rais Samia amemteua Joel Nanauka kuwa Waziri Ofisi ya Rais Maendeleo ya Vijana na kusema kwamba Wizara hiyo haitakuwa na Naibu Waziri kwa sababu ipo chini ya Ofisi ya Rais na watakuwepo wa kumsaidia.
Hamad Yusuph Masauni ameteuliwa kuwa Waziri Ofisi ya Makamu wa Rais Muungano na Mazingira huku Festo Dugange akiteuliwa kuwa Naibu Waziri katika Wizara hiyo. Kwa upande wa Ofisi ya Waziri Mkuu, Sera, Bunge, Utaratibu na Wenye Ulemavu Waziri ni William Lukuvi na Naibu Waziri akiwa Ummy Nderiananga.
Waziri Ofisi ya Waziri Mkuu – Kazi, Ajira na Mahusiano ni Deus Sangu huku Naibu Waziri akiwa Rahma Riadh Kisuo na kwa upande wa
Ofisi ya Waziri Mkuu – Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa (TAMISEMI), Waziri ni Prof. Riziki Shemdoe na Naibu Waziri (Elimu) Reuben Kwagilwa na Naibu Waziri (Afya) ni Dk. Jafar Rajab Seif.
Aidha kwa upande wa Wizara ya Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki, Waziri: ni Balozi Mahmoud Thabit Kombo na Naibu Waziri ni Dk. Ngwaru Maghembe pamoja na James Millya.
Wizara ya Mambo ya Ndani ya Nchi, Waziri ni Boniface Simbachawene huku Naibu Waziri akiwa Denis Londo, hata hivyo kwa upande wa Wizara ya Kilimo Waziri ni Daniel Chongolo na Naibu Waziri akiwa David Silinde.
Wizara ya Maji Rais Samia amemrudisha
Jumaa Aweso kuwa Waziri wa Wizara hiyo na
Naibu Waziri akiwa Kundo Mathew, Wizara ya Ulinzi na Jeshi la Kujenga Taifa, Waziri ni Dk. Rhimo Nyansaho na Waziri Wizara ya Ujenzi ni
Abdallah Ulega na Naibu Waziri akiwa Mhandisi Godfrey Kasekenya.
Wizara ya Uchukuzi Waziri ni Prof. Makame Mbarawa Mnyaa na Naibu Waziri akiwa David Kihenzile huku kwa upande wa Wizara ya Viwanda na Biashara, Waziri ni Judith Kapinga na Naibu Waziri akiwa Patrobas Katambi.
Kwa upande wa Wizara ya Mawasiliano na Teknolojia ya Habaril, Waziri ni Angellah Kairuki na Naibu Waziri akiwa Switbert Mkama huku
Wizara ya Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wanawake na Makundi Maalum, Waziri akiwa Dk. Dorothy Gwajima na Naibu Waziri ni Maryprisca Mahundi.
Wizara ya Ardhi, Nyumba na Maendeleo ya Makazi Waziri ni Dk. Leonard Akwilapo huku
Naibu Waziri akiwa Kaspar Mmuya na
Wizara ya Maliasili na Utalii Waziri ni Dk. Ashatu Kijaji na Naibu Waziri akiwa Hamad Chande.
Hata hivyo Rais Samia amemteua Palamagamba Kabudi kuwa Waziri wa Habari, Utamaduni, Sanaa na Michezo huku Manaibu wake wakiwa Hamisi Mwinjuma maarufu Mwana FA pamoja na Paul Makonda.
Rais Samia pia amembakisha Anthony Mavunde kuwa Waziri Wizara ya Madini huku Naibu Waziri katika Wizara hiyo akiwa Dk. Steven Kiruswa na Wizara ya Nishati, Waziri Deogratius John Ndejembi na Naibu Waziri ni Salome Makamba.
Na Wizara ya Katiba na Sheria, Waziri ni Juma Homera na Naibu Waziri akiwa Zainabu Athman Katimba.

