

NA MWANDISHI WETU, DODOMA
MENEJIMENTI ya Wizara ya Madini Oktoba 27, 2025 ilikutana na Wakuu wa Taasisi zake katika kikao kilicholenga kupokea taarifa ya ufuatiliaji na tathmini kwa majukumu yaliyotekelezwa na taasisi hizo katika kipindi cha Robo ya Kwanza ya Mwaka wa Fedha 2025/26.

<
Kwa upande wa STAMICO, pamoja na mambo mengine, taarifa ilieleza kuwa, zoezi la kusimika mitambo ya uzalishaji wa mkaa wa Rafiki Briquettes unaotokana na makaa ya mawe unaozalishwa na shirika hilo hivi karibuni itasimikwa katika mikoa ya Dodoma na Tabora. Tayari mitambo kama hiyo inaendelea na uzalishaji wa nishati hiyo jijini Dar es Salaam katika eneo la Kisarawe, Pwani na Kiwira mkoani Songwe.

Aidha, shirika hilo, lilisistiza kuhusu azma yake ya kuendeleza leseni zake za madini muhimu na mkakati zilizopo katika maeneo mbalimbali nchini ikiwa ni hatua ya kulifanya kuingia katika uwekezaji mkubwa.
Vilevile, ilielezwa kuwa, katika robo ya kwanza ya mwaka 2025/26 jumla ya kilo 2,356.413 zimesafishwa katika Kiwanda cha Kusafisha Dhahabu cha Mwanza Precious Metals Refinery chenye ubia na STAMICO kwa ajili ya Banki Kuu ya Tanzania. Ilielezwa kwamba, hadi sasa kiasi cha tani 12 za dhahabu tayari zimenunuliwa na benki hiyo kama amana kwa taifa tangu ilipoanza ununuzi rasmi wa dhahabu mwezi Oktoba, 2024.
Pia, pamoja na masuala mengine yaliyojadiliwa, taarifa ya GST kuhusu ununuzi wa helkopita kwa ajili ya shughuli za utafiti wa kina wa madini nchini, ililezwa kwamba, taratibu za manunuzi zinaendelea. Katika bajeti yake ya mwaka 2025/26, Wizara kupitia GST iliahidi kununua helkopita ikiwa ni juhudi za kuhakikisha ifikapo mwaka 2030 angalau asilimia 50 ya nchi iwe imefanyiwa utafiti wa kina. Aidha, GST imeanza ujenzi wa maabara kubwa nchini na ya kisasa Mkoani Dodoma na kwa ajili ya upimaji wa sampuli mbalimbali nchini. Mara maabara hiyo itakapokamilika italeta ufanisi mkubwa katika shughuli za upimaji sampuli.
Kwa upande wa Kituo cha Jemolojia Tanzania (TGC) pamoja na juhudi zinazoendelea za kukiimarisha kituo hicho kwa kujengwa miundombinu ya majengo, taarifa ya kituo ilileza kwamba, kimefungua duka maalum la kuuza bidhaa za mapambo ya vito na usonara katika eneo la Kituo cha Mikutano cha Kimataifa cha AICC, jijini Arusha.
Hivyo kufanya idadi ya maduka hayo kuwa mawili, ukijumuisha na duka lililopo uwanja wa Ndege wa Kimataifa Kilimanjaro ( KIA).

