NA FLORAH AMON, DAR ES SALAAM
SERIKALI imetoa kiasi cha Sh.Bilioni 54.5 kwa ajili ya ujenzi wa barabara ya Kilwa pamoja na Daraja la Mto Mzinga.

Hatua hiyo ya Serikali inakuja ili kupunguza adha ya foleni ambayo imekuwa kero ya muda mrefu kwa wananchi wanaosafiri kutoka Wilaya na mikoa ya Kusini mwa Jiji la Dar es Salaam.

Mradi huu ni sehemu ya juhudi za serikali kuboresha miundombinu ya usafiri na kurahisisha shughuli za kiuchumi katika jiji hilo.
Wananchi wa maeneo ya Mzinga na Kongowe wameeleza kuwa foleni katika eneo hilo imekuwa changamoto kubwa, hasa nyakati za asubuhi na jioni, kutokana na ufinyu wa barabara na wingi wa magari yanayotumia njia hiyo nakuongeza kuwa mara nyingi husafiri kwa zaidi ya saa mbili kutoka Kongowe hadi Mbagala Rangi tatu, hali inayopunguza tija katika shughuli zao za kila siku.

Kufuatia malalamiko hayo, Mkuu wa Mkoa wa Dar es Salaam, Albert Chalamila, akiambatana na Meneja wa Wakala wa Barabara Tanzania (TANROADS) Mkoa wa Dar es Salaam, Mhandisi Alinanuswe Kyamba, walitembelea eneo hilo kujionea hali halisi.

Katika ziara hiyo, viongozi hao waliahidi kuwa serikali imepanga kujenga barabara hiyo kwa kiwango cha lami na kuwa na njia sita ili kuongeza uwezo wa kupitisha magari mengi kwa wakati mmoja.

Mhandisi Kyamba amebainisha kuwa ujenzi wa kipande cha barabara kuanzia Kongowe hadi Mbagala Rangi Tatu chenye urefu wa kilomita 3.8 utaanza mara moja, na mradi huo unatarajiwa kukamilika ndani ya kipindi cha miezi 15.

Ameongeza kuwa mradi huo utajumuisha pia ujenzi wa mifereji ya kupitisha maji ya mvua na taa za barabarani ili kuhakikisha usalama wa watumiaji wa barabara.

Kwa upande wake, Mkuu wa Mkoa Chalamila amesema serikali ya Mkoa itasimamia kwa karibu utekelezaji wa mradi huo kuhakikisha unakamilika kwa wakati na kwa ubora unaotakiwa.
Amesisitiza kuwa miradi ya namna hiyo ni kielelezo cha dhamira ya serikali ya awamu ya sita chini ya Rais Samia Suluhu Hassan ya kuboresha huduma za usafiri na kurahisisha maisha ya wananchi.
Mbali na mradi wa Mto Mzinga, Chalamila pia ametembelea miradi mingine ya ujenzi wa madaraja katika maeneo ya Tungi na Nguva wilayani Kigamboni, pamoja na Kigogo na Jangwani, yenye lengo la kupunguza changamoto za mafuriko na kuboresha upitishaji wa magari katika maeneo hayo.

Ujenzi wa Daraja la Mto Mzinga unatarajiwa kuwa suluhisho la kudumu kwa changamoto ya foleni katika barabara ya Kilwa, ambayo ni lango kuu la kuunganisha Jiji la Dar es Salaam na mikoa ya Kusini.
Kukamilika kwa mradi huo kutarahisisha usafirishaji wa watu na bidhaa, kuongeza ufanisi wa shughuli za biashara, na kuchochea ukuaji wa uchumi wa mkoa huo na taifa kwa ujumla.

