NA MWANDISHI WETU, GEITA
NAIBU Waziri Mkuu na Waziri wa Nishati, Dk. Doto Biteko, amesema ongezeko la shughuli za uchimbaji na uongezaji thamani madini limechochea mahitaji makubwa ya nishati ya umeme nchini, hali inayothibitisha kasi ya ukuaji wa sekta hiyo.
Amebainisha hayo, jana Septemba 28, 2025, wakati akihitimisha Maonesho ya 8 ya Teknolojia ya Madini yaliyofanyika mkoani Geita, katika Viwanja vya Dkt. Samia Suluhu Hassan Bombambili kuanzia Septemba 18 hadi 28 2025.
Dk. Biteko alisema Serikali inaendelea kupeleka nishati ya umeme kwenye maeneo ya uchimbaji pamoja na viwanda vya kusafisha na kuongeza thamani madini ili kuhakikisha uzalishaji hausimami na kuongeza tija.
“Ukuaji wa Sekta ya Madini unakwenda sambamba na ongezeko la mahitaji ya nishati ya umeme nchini, mfano hapa Geita megawati zaidi ya 30 zinatumika hapa tofauti na hapo awali. Serikali imejipanga kuhakikisha umeme unaendelea kufika kwenye migodi, maeneo ya wachimbaji wadogo na viwanda vya uongezaji thamani ili sekta iendelee kukua kwa kasi na kutoa ajira zaidi,” alisema Dk.Biteko.
Dk.Biteko aliongeza kuwa Sekta ya Madini imeendelea kuwa himilivu katika kipindi cha miaka minne na kwa sasa imejidhihirisha kama moja ya mihimili muhimu ya kiuchumi nchini.
Awali, alipokuwa akitembelea mabanda katika Maonesho hayo, Benki Kuu ya Tanzania (BoT) ilieleza kuwa tayari imenunua zaidi ya tani 10 za dhahabu zenye thamani ya Sh. Trilioni 2.5, ikiwa ni sehemu ya mkakati wa kuimarisha akiba ya taifa na kulinda uchumi dhidi ya misukosuko ya kimataifa.
Kwa upande wake, Naibu Katibu Mkuu wa Wizara ya Madini, Msafiri Mbibo, alisema tangu kuanzishwa kwake miaka minane iliyopita, Maonesho ya Teknolojia ya Madini Geita yameleta manufaa makubwa kwa Sekta na taifa kwa ujumla.
“Kupitia maonesho haya tumeona maboresho makubwa kwenye usalama wa migodi na shughuli za uchimbaji, ufanisi na ongezeko la tija katika uzalishaji, ubora wa biashara za madini, pamoja na kupungua kwa migogoro kati ya jamii na wawekezaji,” alisema Mbibo.
Naye, Mkuu wa Mkoa wa Geita, Martin Shigella, alisema maonesho hayo hayajanufaisha Tanzania pekee, bali hata nchi za jirani ambazo zimekuwa zikija kujifunza mbinu bora za usimamizi wa sekta na namna ya kufanya uchimbaji wenye mafanikio akitolea mfano nchi ya Malawi.