NA MWANDISHI WETU,DODOMA
WAZIRI MKUU, Kassim Majaliwa amesema kuwa madereva wa Serikali wanawajibu wa kufanya kazi kwa weledi na nidhamu ya hali ya juu ikiwemo ukaguzi wa gari kabla na baada ya safari, kujaza na kutunza kikamilifu taarifa za safari na matengenezo.
Amewataka Madereva na Wasimamizi wahakikishe usalama wa vyombo vya usafiri, abiria, mizigo na nyaraka za Serikali pamoja na kutumia vifaa vya kisasa vya usalama, na kujiepusha na tabia zinazoweza kuhatarisha maisha, mali na siri za Serikali.
Ameyasema hayo leo (Jumanne, Septemba 2, 2025) alipofungua Mkutano wa Chama cha Madereva wa Serikali Tanzania (CMST), jijini Dodoma.
Amesema chama hicho kimekuwa nguzo muhimu katika kuboresha huduma za udereva Serikalini na kuchangia maendeleo ya Taifa kwa ujumla.
Pia, Waziri Mkuu amewahakikishia madereva hao kuwa Serikali inaendelea kufanyia kazi changamoto mbalimbali zinazowakabili madereva ili kuendelea kuimarisha mazingira ya kazi na ustawi wa madereva wa Serikali kote nchini.
“Changamoto mlizowasilisha ni mwendelezo wa kazi kubwa iliyopo mbele yetu, na kwa ushirikiano kati ya Serikali, Waajiri na Chama cha Madereva, tutaendelea kusonga mbele kwa hatua madhubuti ili kuboresha kada hii muhimu kwa manufaa ya Taifa letu.”
Pia, Waziri Mkuu amewataka waajiri wahakikishe stahiki za madereva zinalipwa kwa wakati, mafunzo ya mara kwa mara yanafanyika, miundo ya ajira inatekelezwa ipasavyo na wanapewa kipaumbele katika motisha mbalimbali.
Kwa upande wake, Waziri wa Ujenzi, Abdallah Ulega amesema madereva ni mhimili muhimu katika utekelezaji wa majukumu ya kila siku ya Serikali na nidhamu na uadilifu ndio msingi wa heshima wa kada hiyo.
“Sisi Serikali tutahakikisha ustawi wa madereva unakuwa kipaumbele chetu, wao wakiishi vizuri maana yake ni kwamba watafanya kazi zao kwa ufanisi mkubwa.”
Waziri Ulega amesema lengo la mkutano huo ni kujadili changamoto na kubadilisha uzoefu na kuimarisha mshikamano.
Naye, Katibu Mkuu wa CMST, Castro Nyabange amesema kuwa chama chicho kinampongeza kwa dhati Mheshimiwa Rais Dk.Samia Suluhu Hassan kwa hatua mbalimbali za kuboresha maslahi ya watumishi wa umma wakiwemo madereva.
“Upandishaji wa mishahara kwa watumishi umetugusa pia sisi madereva, awali sisi madereva wa Serikali tulikuwa na mishahara ya viwango vya chini sana, tunaahidi kufanya kazi bega kwa bega na Serikali kwa kuzingatia weledi katika utendaji.”
Mkutanao huo wenye kaulimbiu isemayo “Dereva wa Serikali, Epuka Ajali, Linda Gari Lako na Watumiaji Wengine wa Barabara na Oktoba Shiriki Uchaguzi Mkuu”.
Mkutano huo umehudhuriwa na Madereva wa Serikali zaidi ya 2,500 kutoka Tanzania Bara na Zanzibar.